Watu zaidi ya 125,000 wanakufa kwa kifafa kila mwaka
- Ni kutokana na kutokuwepo kwa matibabu ya uhakika.
- Zaidi ya watu milioni 50 wanaishi na ugonjwa huo duniani kote.
- WHO yatoia mwongozo wa matibabu.
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya (WHO) limeeleza kuwa inakadiriwa kuwa kila mwaka watu 125,000 hufariki dunia kutokana na ugonjwa wa kifafa huku likitoa mwongozo kupunguza athari za ugonjwa huo.
Kifafa kinashika nafasi ya tano kwenye magonjwa ya mishipa ya fahamu yanayosababisha ulemavu.
Huu ni ugonjwa ambao unasababishwa na seli za mishipa ya fahamu zilizopo kwenye ubongo kutoa umeme [impulses] mwingi kuliko kawaida kwenda kwenye misuli na sehemu nyingine za mwili, na matokeo yake mtu huanza kupata degedege ya mwili mzima, kukakamaa, kuanguka chini na kupoteza fahamu.
Taarifa iliyotolewa Desemba 12, 2022 na WHO jijini Geneva, nchini Uswisi imeeleza kuwa zaidi ya watu milioni 50 wanaishi na ugonjwa huo duniani kote.
Wagonjwa wengi wa kifafa hawapati matibabu ya kudhibiti ugonjwa huo na pengo hilo katika nchi za kipato cha chini ni asilimia 75 ilhali katika nchi za kipato cha kati ni asilimia 50.
“Pengo linatokana na kutokuweko kwa mifumo ya afya ya kutibu kifafa, mgao usio na uwiano wa huduma, kipaumbele kidogo kwa tiba dhidi ya kifafa na wagonjwa au jamaa zao kutosaka tiba kutokana na ukosefu wa uelewa na unyanyapaa,” imesema WHO ikieleza sababu za kutomaliza tatizo hilo.
Ingawa kifafa kinatibika, zaidi ya asilimia 70 ya wagonjwa wanaweza kuacha kupata kifaa iwapo watapata tiba sahihi ambayo gharama yake ni dola 5 (Sh11,669) kwa mwaka.
WHO inasema kifafa kina athari kwenye mwili na akili za mgonjwa ambapo takribani nusu ya watu wenye kifafa wana changamoto ya kiafya kimwili au kiakili inayohusiana na matokeo mabaya ya afya au ongezeko la mahitaji ya kiafya.
Zinazohusiana:
- Fanya haya kuboresha ulaji wa chakula
- Jinsi unavyoweza kuishinda sonona isiharibu maisha binafsi, kazi.
- Mambo yatakayokusaidia kupunguza hatari ya kupata saratani.
Duniani kote, kwa mujibu wa WHO, wagonjwa wa kifafa wanakabiliwa na unyanyapaa, kubaguliwa na haki zao za kibinadamu kukiukwa. Matokeo yake wanakumbwa na vikwazo vya kielimu, ajira na mara nyingi wanashindwa kushiriki katika maisha ya kijamii.
Mkurugenzi wa WHO anayehusika na masuala ya Afya ya Akili na Matumizi ya Madawa ya Kulevya, Dk Dévora Kestel, anasema, “kwa kuzingatia kuwa kifafa kina athari ya kibinafsi, kiafya, ujumuishwaji kiuchumi na kijamii kwa mgonjwa, hatua haipaswi kuwa nyingine yoyote ile zaidi ya ujumuishaji wa kina na ushiriki wa jamii.”
Ni kwa kutambua pengo na uwezo wa kutibu kifafa, WHO imeandaa mwongozo uliopatiwa jina Kuboresha Maisha ya watu wenye Kifafa ambao unalenga kujumuisha tiba ya kifafa kwenye mfumo wa afya ya msingi, ukitaja hatua za kuchukua.
Mwongozo wa kutibu Kifafa
- Kutoa huduma za kina katika ngazi zote hasa katika ngazi ya huduma ya msingi.
- Kuongeza uwezo wa kila mgonwa kupata dawa za kuzuia kifafa zinapatikana.
- Kukabili unyanyapaa na sheria na vitendo vya kibaguzi: Kuendeleza na kuheshimu haki za binadamu na ujumuishi wa kijamii kwa watu wenye kifafa, familia na wahudumu wao.
WHO inasema mwongozo huo unalenga kutumiwa na wadau mbalimbali na zikiwemo serikali, watunga sera, mameneja wa programu kwenye wizara za afya, hifadhi ya jamii, elimu na haki za binadamu ili kupanga upya na kuimarisha hatua na huduma zao dhidi ya kifafa.
Latest