Fahamu ugonjwa wa shinikizo la damu unaowatesa wengi

June 27, 2025 12:02 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Wataalaumu wasema ni muuaji wa kimya kimya anayesababisha magonjwa ya moyo na vifo vingi.
  • Watu bilioni 1.3 wanakabiliwa na shinikizo la damu duniani.

Dar es Salaam. Si jambo geni kwa sasa kusikia mtu unayemfahamu akipoteza maisha kutokana na maradhi ya shinikizo la damu. Ugonjwa huu unaweza kumkumba mtu yoyote na wa hali yeyote duniani. 

Hii ni kwa sababu magonjwa mengi yanayohusiana na moyo kushindwa kufanya kazi, pamoja na vifo vingi vinavyotokana na magonjwa ya moyo au kiharusi, chanzo chake ni shinikizo la damu.

Kwa namna nyingine shinikizo la damu, hujulikana kama muuaji wa kimya kimya ‘silent killer’ kutokana na ukosefu wa dalili za wazi kwa wengi hadi madhara makubwa yanapotokea.

Kwa mujibu wa Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, Henry Mwandolela, kutoka Hospitali ya Heameda iliyopo Bunju, Dar es Salaam, shinikizo la damu ni nguvu inayotumika wakati moyo unaposukuma damu kupitia mishipa ya damu.

“Moyo ndio unafanya kazi ya kusukuma damu, na damu lazima ipite kwenye mishipa ya damu. Huwezi kupeleka damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye sehemu za mbali za mwili kama kichwa, mikono, miguu bila kuwa na shinikizo,” anasema Dk Mwandolela.

Vipimo na maana ya shinikizo la damu (Blood pressure)
Kwa kawaida, shinikizo la damu hupimwa kwa milimita za zebaki (mmHg), na kwa mtu mzima, vipimo vinavyokubalika ni kati ya 90/60 na 140/90 mmHg.

Namba ya juu (mfano, 140) inaashiria ukinzani wa mishipa ya damu wakati moyo unakaza kusukuma damu, wakati namba ya chini (mfano, 90) inaonyesha msukumo wa damu wakati moyo upo kwenye hali ya kupumzika.

Dk Mwandolela anaeleza kuwa shinikizo la juu likizidi 140/90 mara kwa mara, tunasema mtu ana tatizo la shinikizo la juu la damu. 

“Iwapo litashuka chini ya 90/60, tunasema mtu ana tatizo la kushuka kwa shinikizo la damu,” anasema. 

Usisubiri kichwa kuume au kifua kubana, pima shinikizo la damu mapema hasa kama unahangaika na uzito au maisha ya kukaa sana bila mazoezi. Picha/Canva

Hata hivyo, shinikizo la damu limegawanyika katika makundi mawili ambayo ni shinikizo la juu na shinikizo la chini.

Shinikizo la juu hutokea kwa watu wa umri mdogo wenye visababishi vinavyoweza kurekebishika, kama uvimbe kwenye figo, matatizo ya vichocheo vya mwili, na maambukizi. 

Kwa watu wazima, huathiriwa na mabadiliko ya mwili yanayokuja na umri mkubwa kama kutanuka kwa mishipa ya damu ambayo muda mwingi ipo katika hali ya kusinyaa. 

Shinikizo la chini hutokea ikiwa msukumo wa damu unakuwa mdogo kupita kiasi, hali inayosababisha mwili kushindwa kufanya kazi ipasavyo.

Tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu kwa mujibu wa Dk Mwandolela ndio tatizo kubwa linalosababisha magonjwa mengi ya moyo na kusababisha watu wengi kupoteza maisha.

Tatizo la kupanda kwa shinikizo la damu linaongoza kusababisha magonjwa ya moyo, vifo vingi, na uharibifu wa viungo muhimu kama ubongo, figo, macho, na mishipa ya damu.

“Msukumo mkubwa wa damu unaweza kuharibu viungo hivyo kwa sababu vinashindwa kuhimili hali hiyo,” amesema Dk Mwandolela.

Uzito, kitambo ni hatari kwa afya

Kuna vyanzo mbalimbali vya maradhi hayo yanayozidi kuongeza siku hadi siku ukiwemo uzito uliopitiliza.

Daktari Taphinez Machibya anaeleza katika chapisho lililochapishwa kwenye tovuti ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi  (Katavi Regional Refarral Hospital) kuwa shinikizo la damu husababishwa na vinasaba (Genetics), kitambi (Obesity), matumizi ya pombe, magonjwa ya figo (RENAL diseases), kisukari (Diabetes mellitus) na uvutaji sigara.

Kitambi si fahari, ni mzigo wa hatari unaoweza kukupeleka hospitali au kaburini. Picha/Canva.

Mtaalamu huyo wa afya anaeleza kuwa maisha ya hofu (Stressful life) husababisha kumwagwa kwa wingi vichocheo kama adrenaline & prostaglandins zinazoongeza mapigo ya moyo.

Vile vile, viashiria vinavyoweza kuongeza hatari ya kupata shinikizo la damu ni hali kama mimba (mara chache) ambayo inaweza kusababisha kifafa cha mimba (eclampsia) pamoja na magonjwa ya mfumo wa vichocheo (endocrine disorders) kama vile pheochromocytoma, Cushing’s disease, na thyrotoxicosis. 

Mimba ni baraka, lakini shinikizo la damu linaweza kuiweka hatarini hivyo linda maisha yako na ya mtoto. Picha/ Canva.

Magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo (Congenital heart diseases) na baadhi ya dawa zenye kichocheo cha estrogen za uzazi wa mpango (oral contraceptives, anabolic steroids, corticosteroids, anaeleza kuwa ni miongoni mwa viashiria vinavyoweza kuongeza hatari ya mtu kupata shinikizo la damu.

Ugonjwa huu hauathiri Watanzania pekee bali watu wengi duniani hupoteza maisha kwa sababu ya shinikizo la damu. 

Ni ugonjwa unaoathiri mamilioni

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2023 ilikadiria kuwa idadi ya watu wazima wenye shinikizo la damu iliongezeka mara mbili katika kipindi cha miongo mitatu, kutoka watu milioni 650 mwaka 1990 hadi bilioni 1.3 mwaka 2019.

WHO inaongeza kuwa athari za shinikizo la damu zimesababisha vifo milioni 10.8 vinavyoweza kuzuilika kila mwaka na miaka milioni 235 ya maisha yenye ulemavu. 

“Takriban mtu mmoja kati ya watu wazima watatu duniani ana shinikizo la damu, huku viwango vikiwa juu zaidi kwa wanaume walio chini ya miaka 50 na karibu sawa kwa wanaume na wanawake baada ya miaka 50,” ripoti hiyo ya WHO inaeleza.

Shinikizo la damu si tatizo lako peke yako ni janga la dunia. Usikubali kuwa sehemu ya takwimu za waliopoteza maisha bila kujua hali yao. Picha/ Canva.

Ripoti hiyo ya WHO inabainisha kuwa takriban nusu au karibia asilimia 46 ya watu wenye shinikizo la damu hawajawahi kugunduliwa. 

Kati ya waliogunduliwa, ni asilimia 42 pekee wanaopata matibabu huku nusu yao tu wakifanikiwa kudhibiti hali yao.

Ili kuendelea kuufahamu zaidi ugonjwa huu endelea kufuatilia Nukta Habari.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks