Fanya haya kulinda afya kazini

August 20, 2019 9:47 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ushughulishe mwili wako kwa kutokukaa muda mrefu sehemu moja bali tembea na kujinyoosha. 
  • Pendelea kutumia ngazi kuliko lifti kama ofisi yako ni ya ghorofa. 
  • Ukiwa kwenye kiti kaaa mkao wa nyuzi 90 

Dar es Salaam. Licha ya watu wengi kupendelea kazi za maofisini, baadhi yao wameshindwa kufahamu changamoto ya kukaa sehemu moja kwa muda mrefu.

Sayansi inaeleza kuwa mtu akiwa amekaa anatumia nguvu chache kuliko akiwa kwenye mizunguko. Tafiti zimeunganisha tabia hiyo na matatizo mbalimbali ya afya yakiwemo magonjwa ya kisukari, kansa na hata kiharusi. Lakini kukaa muda mrefu sehemu moja kunasababisha maumivu ya mgongo kwa watu wengi. 

Ufanye nini kuepuka matatizo hayo wakati huo huo ukiendelea kutimiza majukumu yako unapokua ofisini? 

Mfiziotherapia, Dk Joshua Sultan ambaye ni mwanafunzi wa Chuo cha Tiba na Afya cha KCMC Moshi anasema kukaa kwa muda mrefu kunampelekea mtu kupata maumivu ya mgongo ambayo yanaweza kuzuirika kwa kukaa mkao mzuri. 

“Kukaa vizuri ni pamoja na kufuata mkao wa nyuzi 90 na kutoinamia sana vifaa vya kazi hasa simu na kompyuta pale mtu awapo kazini,” anasema Dk Sultan.

Namna nzuri ya kukaa unapokua ofisini. Picha|Mtandao.

Njia nyingine rahisi ili kuepuka matatizo yanayotokana na kukaa kwa muda mrefu ni pamoja na:

Tembelea wafanyakazi wenzako

Kawaida, mtu anapaswa kusimama walau nusu saa kwa kila saa ili kuimarisha afya yako. Hivyo ni kusema, ni vyema kutembelea wafanyakazi wenzako pale unapokuwa ofisini walau dakika 15 kila saa kwa kubadilishana mawazo na hata kuelekezana.

Penda kutumia ngazi badala ya lifti

Kama haujachoka na siyo mgonjwa, penda kutumia ngazi ili kuupa mazoezi mwili wako ikiwemo miguu na mgongo. Kwa kufanya hivyo itakusaidia kupunguza uhatarishi wa kupata kitambi, kisukari na hata kiharusi. Mazoezi haya yanafaa zaidi watu wanaofanya kazi kwenye ofisi za ghorofa. 


Zinazohusiana


Tembea iwapo mahala unakwenda sio mbali sana.

Kama unatumia usafiri wa daladala, siyo mbaya ukashuka kituo kimoja au viwili kabla wakati uendapo na unaporudi kutoka kazini. Hiyo itakusaidia kutumia chakula ambacho umekula mchana.  

Kufanya hivi ni rahisi kwani asubuhi na jioni jua sio kali kiasi cha kukutoa jasho. Hata hivyo, kufanya hili inategemea na usafi wa mazingira uliyopo ili usije kuchafuka kabla ya kufika kazini.

Simama na ujinyooshe.

Uwapo kazini, pata muda wa kusimama kila unapoweza na ujinyooshe viungo pale unapokuwa umekaa kwa muda mrefu. 

Dk Sultan amesema kuinama kidogo na kuzungusha shingo pamoja na kiuno ni kati ya mazoezi yanayofaa kukabiliana na madhara yanayoletwa na kukaa kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Sultan, mtu anaweza fanya mazoezi kadhaa pale awapo nyumbani akijumuisha na familia yake. Fuatilia muendelezo ya sehemu hii kwa mazoezi ya viungo ambayo mtu anaweza kufanya kwa muda wa dakika 15 hadi 30.

Enable Notifications OK No thanks