Kanda ya Ziwa yachukua hatua kukabiliana na tishio la ukame

November 5, 2021 6:22 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Baadhi ya mikoa itapata mvua chache na vipindi virefu vya ukavu.
  • Hali hiyo itapunguza kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini.
  • Wadau waanza kuchimba visima, kuvuna maji na kuhifadhi kwenye mabwawa.

Mwanza. Baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutabiri uwepo wa upungufu wa mvua katika baadhi ya maeneo ya nchi, wadau wa masuala ya maji wameanza kuchukua hatua kukabiliana na hali hiyo ikiwemo kuvuna maji ya mvua. 

TMA imesema mwelekeo wa mvua hizo za msimu zinazoanza Novemba, 2021 hadi Aprili, 2022 ni mahususi katika mikoa inayopata mvua mara moja kwa mwaka ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Rukwa, Songwe, Mbeya na Iringa ambapo mvua zitakuwa chini ya wastani hadi wastani.

Mikoa mingine ni Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na kusini mwa Morogoro ambapo mvua zitakuwa wastani hadi chini ya wastani. 

Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi amesema kutokana na upungufu wa mvua, kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini kinatarajiwa kupungua hususan katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za chini ya wastani.

“Hali hii inaweza kupunguza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali na kupelekea migogoro baina ya watumiaji wakubwa na wadogo,” amesema Dk Kijazi.

Dk Kijazi amesema wadau wanashauriwa kuzingatia matumizi endelevu ya maji katika shughuli za kuchakata madini, uzalishaji wa umeme, matumizi viwandani na majumbani.


Soma zaidi: 


kufuatia utabiri huo Bodi ya Bonde la Ziwa Victoria imeanza uchimbaji wa visima virefu na uandaaji wa mabwawa yatakayovuna maji ya mvua ili kukabiliana na upungufu wa maji.

Afisa Uhusiano wa Bonde la Ziwa Victoria, Perepetua Masaga amesema utekelezaji wa mipango hiyo ni sehemu ya mkakati wa bodi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo ukame.

“Tumepokea tahadhari hiyo na kwamba tahadhari hizi zinakuja ili kusaidia bodi kuweza kurekodi takwimu zetu za mvua za kila mwaka, bonde la ziwa lina misimu miwili ambayo ni Novemba hadi Januari na Machi hadi Juni, ambapo tunarekodi takwimu kujua maendeleo yapoje,” amesema Masaga

Amesema utabiri wa TMA utaongeza nguvu kwa bodi hiyo kuendelea kutoa elimu na kuishawishi jamii kuvuna maji ya mvua ili kuyatunza kwa matumizi ya baadaye.

Pia bodi inaendelea kufanya tathmini ya maji chini ya ardhi hususan maeneo ambayo yanakumbwa na ukame kila mwaka ikiwemo Wilaya za Itilima na Maswa mkoani Simiyu.

“Katika wilaya hizo tunao mpango wa kufanya ili kupata maji mengi zaidi kwa kuchimba visima virefu pamoja na mabwawa ili kuhifadhi maji mengi lakini pia kuhifadhi mazingira,” amesema Masaga.

Wananchi katika maeneo hayo yatakayopata mvua chache wametakiwa  kutunza mazingira kwa kuweka makingio na kuvuna maji ya mvua na kuyatumia kwa tahadhari ili kukabiliana na ukame.

Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Renatus Shihnu amewataka wananchi kutofanya shughuli yoyote ya kilimo na ufugaji kando ya vyanzo vya maji ili kulinda na kutunza vyanzo hivyo visikauke kutokana na kuwepo kwa tishio la ukame.

Amesema shughuli hizo zikifanyika  ndani ya vyanzo vya maji zinasababisha mchanga kuingia kwenye njia za maji hivyo kusababisha maji kutoonekana.

“Tunatoa wito kwa wananchi wasiendeleze shughuli za kilimo na ufugaji kwenye vyanzo vya maji na shughuli hizo ni vema zifanyike nje ya mita 60 ili kulinda na kuhifadhi mazingira,” amesema Shinu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW