Watanzania washauriwa kutumia taarifa za hali ya hewa kwenye mipango ya maendeleo
- Awamu ya pili ya Mpango wa Kimataifa wa Huduma za Hali ya Hewa (2018-2019) una lenga kuongeza ujasiri wa watu kuhusu maafa na mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi za Malawi na Tanzania.
- Wananchi watakiwa kuthamini na kutumia taarifa sahihi zinazotolewa na TMA
Serikali imewataka wananchi kufuatilia na kutumia kwa usahihi taarifa za hali hewa nchini katika mipango ya shughuli mbalimbali za maendeleo ili kuongeza tija na kuepuka maafa yanayoweza kutokea wasipochukua tahadhari.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Prof. Faustin Kamuzora amesema hali ya hewa ina watumiaji wengi na ni muhimu kila mtumiaji apate taarifa kuhusu mabadiliko yanayojitokeza ili kufanya maamuzi sahihi ya mipango ya maendeleo.
“Hali ya hewa ina watumiaji wengi, na ni bora kabisa kwamba kila mtumiaji aweze kupata hizo taarifa na kuweza kuzitumia kuliko kuwekeza bila kujua hali ya hewa itakuaje” amesema Prof. Kamuzora.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa awamu ya pili ya mradi wa kuboresha Awamu ya pili ya Mpango wa Kimataifa wa Huduma za Hali ya Hewa (GFCS) unaotekelezwa katika nchi za Africa , amewetaka pia wakulima kuiamini Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)katika utoaji wa taarifa za hali ya hewa, kwasababu imeboresha miundombinu na mifumo yake kwa zaidi ya asilimia zaidi ya asilimia 80.
Mfumo huo wa GFCS unakusudia kuziwezesha nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kuboresha na kuimarisha miundombinu ya hali ya hewa ili kuhakikisha inakuwa sehemu ya kukuza uchumi na shughuli za maendeleo katika nchi husika.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi amesema muamko wa watanzania katika kufuatilia taarifa za mabadiliko ya hali ya hewa na mazingira umeongezeka kutokana na jitihada za wadau mbalimbali kufanya kazi kwa pamoja na kuthamini maisha ya wananchi wa Tanzania.
“Moja ya mafanikio yaliyopatikana kwenye awamu ya kwanza , ni kwamba tumeweza kuwa na ushirikiano wa karibu zaidi na wadau watumiaji wa huduma za hali ya hewa na muamko wa watumiaji umeongezeka” amesema Dk Kijazi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu), Prof. Faustin Kamuzora (kulia) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Awamu ya pili ya Mpango wa Kimataifa wa Huduma za Hali ya Hewa leo jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi na Mkuu wa Programu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Erica Allis. Picha| TheHabari.
Tanzania na Malawi zimekuwa nchi za mwanzo barani Afrika kuanza kutekeleza programu ya pili ya GFCS na amewataka wadau kuendelea kushirikiana na TMA kuwafikia watanzania wengi kwa kuboresha mifumo ya utendaji wa hali ya hewa nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa GFCS, Fiipe Lucio amesema wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kutoa mafunzo na rasilimali mbalimbali ili kufanikisha awamu ya pili ya programu ya hali hewa.
Awamu ya pili ya GFCS ni mradi ulioendeshwa na shirika la Maendeleo ya Norway (NORAD).
Awamu ya pili ya Mpango wa Kimataifa wa Huduma za Hali ya Hewa (2018-2019) itajenga ufanisi wa awamu ya kwanza ya kwanza ya mwaka 2014-2017 yenye lengo la kuongeza ujasiri wa watu kuhusu maafa na mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi za Malawi na Tanzania.
Mradi utaendelea kuendeshwa na GFCS katika shirika la dunia la WMO na kutekelezwa katika ngazi ya kitaifa na wizara ya Afya, Shirika la Afya Duniani (WHO), Programu ya Chakula Duniani (WFP), Wizara ya kilimo na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).