TMA yaotoa tahadhari mvua na radi siku 10 mfululizo

January 2, 2026 3:38 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Yawataka wananchi kuchukua tahadhari stahiki ili kuepuka hatari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya uwepo wa mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika maeneo mbalimbali ya nchi kuanzia Januari 1 hadi 10, 2026 ikiwataka wananchi kuchukua tahadhari.

Kwa mujibu wa taarifa ya TMA iliyotolewa leo Januari 2, 2026, mvua hizo zinatarajiwa kunyesha katika mikoa ya Ukanda wa Ziwa Viktoria ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara. 

“Mvua zinazoambatana na ngurumo za radi zinatarajiwa katika maeneo machache hususan katika kipindi cha siku tano za mwanzo” imeeleza taarifa hiyo.

Taaarifa hiyo ya TMA ni muendelezo wa tahadhari inayoendelea kutolewa kuanzia Desemba 11 mwaka jana ikichangiwa zaidi na mvua za msimu zilizotabiriwa kuanza Novemba 2025 hadi Aprili 2026. 

Kwa upande wa Magharibi mwa nchi, mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora inatarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo. 

Nyanda za Juu Kusini-Magharibi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa pia zinatarajiwa kupata mvua hizo katika maeneo macchache pamoja na mikoa ya nyanda za juu kaskazini.

“Nyanda za juu kaskazini mashariki, mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, itapata vipindi vya mvua vichache, hasa katika siku tano za mwanzo za Januari,” imesema taarifa ya TMA.

Vilevile, pwani ya kaskazini inayojumuisha mkoa wa Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, pwani ya Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba vinatarajiwa kupata vipindi vya mvua.

Kwa mujibu wa utabiri huo, mikoa ya Pwani ya Kusini, Mtwara na Lindi inatarajiwa kupata vipindi vya mvua vichache, huku Kanda ya Kusini inayojumuisha Ruvuma na maeneo ya kusini mwa Morogoro ikitarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo.

“Magharibi mwa nchi, mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora inatarajiwa kupata mvua zinazoambatana na ngurumo za radi katika baadhi ya maeneo,” imesema taarifa ya TMA.

TMA imewahimiza wananchi, hususan wakulima na wafugaji, kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuzingatia ratiba za mvua ili kuepuka hasara za mazao na mali, pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya athari za radi na mvua kubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks