Tanapa yatoa sababu wanyamapori kunasa kwenye tope Mikumi
- Yasema imesababishwa na ukame.
- Wanyama walionaswa waanza kunasuliwa.
- Serikali kujaza maji kwenye mabwawa ya wanyama.
Mwanza. Kufuatia kusambaa kwa video inayoonyesha baadhi ya wanyamapori kunasa katika tope katika hifadhi ya Taifa Mikumi, Serikali yasema ni kweli tukio hilo limetokea na inafanya jitihada za kuwanasua ikiwemo kujaza maji kwenye mabwawa yao.
Msemaji wa Shirika la Hifadhi la Taifa Tanzania (Tanapa), Pascal Shelutete amesema hali hiyo inatokana na changamoto ya ukame iliyoathiri maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na maeneo ya hifadhi za Taifa kutokana na kuchelewa kwa mvua na hivyo kusababisha upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali ya hifadhi.
Shelutete katika taarifa ya Tanapa iliyotolewa leo Desemba 1, 2021 amesema kuwa shirika limechukua hatua stahiki kukabiliana na hali hiyo ikiwemo mkakati wa dharura wa kujaza maji katika mabwawa yanayotumiw na wanyamapori ili kuwanasua wanyama walioazama.
“Mikakati mingine ya muda mrefu ni pamoja na kujenga mabwawa ya kisasa, kuondoa tope katika mabwawa pamoja na kuchimba visima virefu vitakavyotumia mfumo wa umemejua,” amesema Shelutete.
Hata hivyo, shirika hilo kwa kushirikiana na Serikali za mikoa na wilaya zinafanya jitihada za kuelimisha wananchi juu ya matumizi sahihi ya maji katika vyanzo vya maji na mito ili kuhakikisha wanyamapori wanapata maji.
aTanapa imebainisha kuwa mvua zilizonyesha Novemba 30, 2021 zimewezesha maji kiasi kujaa katika mabwawa husika na wanyama kurejea katika hali ya kawaida ya matumizi ya mabwawa.
Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) katika utabiri wake wa mvua za msimu wa vuli kwa mikoa inayopata vipindi viwili vya mvua kwa mwaka na ule wa mvua za masika kwa mikoa inayopata mvua mara moja kwa mwaka ilieleza kuwa mvua katika maeneo mengi zitakuwa chache na zitachelewa kuanza.
Pia Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi alieleza kuwa katika maeneo mengi kutakuwa na vipindi virefu vya ukavu vinavyosababisha kuongezeka kwa joto.
TMA ilitoa tahadhari kuwa hali hiyo inaweza kusababisha uhaba wa maji na kuathiri utendaji wa sekta mbalimbali ikiwemo afya, nishati na shughuli za uhifadhi wanyamapori.
Kukabiliana na hali hiyo, TMA ilishauri mamlaka husika kujipanga ikiwemo kuvuna maji na kuyahifadhi kwa matumizi ya baadaye.
Habari hii imeandikwa na Daniel Samson na Mariam John.