Walivyojipanga kukabiliana na athari za mvua za vuli

September 14, 2021 8:37 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Mvua hizo zitakuwa chache na kuathiri ukuaji wa mazao.
  • Viongozi wajipanga kuto elimu kwa wakulima.
  • Wakulima watakiwa kulima mazao yanayostahimili ukame.

Mwanza. Siku chache baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)  kutoa utabiri wa msimu wa mvua za vuli zitakazopungua, wananchi wa Mkoa wa Mwanza wametakiwa kulima mazao yanayostahimili ukame huku wakitakiwa kufuata ushauri wa maafisa ugani katika maeneo yao.

Msimu wa mvua za vuli ambao huanza Oktoba na kuisha Desemba ni mahsusi kwa maeneo ya mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikiwemo Arusha, Manyara na Kilimanjaro, kaskazini mwa Mkoa wa Morogoro na visiwa vya Mafia.

Mikoa mingine ni Dar es Salaam, Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.

TMA katika taarifa iliyotolewa leo Septemba 2, 2021 ilisema kuwa mvua za vuli zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa kuambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi yanayopata mvua hizo, jambo linaweza kusababisha ukame.

Mbali na mvua za chini ya wastani hadi wastani zinazotarajiwa, vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa katika msimu wa vuli.

Kutokana na kusuasua kwa mvua hizo sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo zinaweza kuathirika iwapo wahusika hawatachukua tahadhari kukabiliana nazo.

Baada ya utabiri huo,  wakazi katika kijiji cha Identemya wilayani Misungwi katika Mkoa wa Mwanza wameiomba Serikali kutoa elimu ya mazao yayostahimili ukame ili kuwapunguzia hasara watakayopata katika kilimo. 

Mazao hayo ni pamoja na mtama, uwele, mbaazi, ulezi na muhogo na viazi vitamu.

Wakazi hao wamesema kwa misimu miwili mfululizo kumekuwa na mvua nyingi ambazo ziliwasaidia kulima aina tofauti ya mazao hivyo utabiri huo unaweza kuwa kikwazo kutokana na aina za mbegu walizonazo. 

Mkazi wa kijiji cha Identemya, Shija Shilighushela  amesema wataalam wa kilimo wanahitajika katika kipindi hiki ili kuwasaidia wakulima waweze kulima na kupata mazao ya chakula. 

“Utabiri huo unachanganya sana hususan sisi wakulima tunaotegemea mvua peke yake,  tunahofia kutopata mazao mengi ya chakula,  hivyo ni vema watuelimishe ni aina gani ya mbegu zinahitajika kwenye msimu huu,” amesema Shilighushela.

Watoto wa Manispaa ya Kigoma Ujiji wakibangua mbegu za michikichi kwa ajili kukamua mafuta ya mawese. Picha|Gift Mijoe. 

“Tunashukru TMA kwa kutuonyesha njia sasa tutatumia mwanga huo kuwasaidia wananchi, maofisa ugani na viongozi wengine wa kiserikali watakuwepo kutoa elimu hiyo,” amesema Kijika

Kijika pia amewataka wananchi kutumia ofisi ya ofisa kilimo kwa ajili ya kupata ushauri zaidi na kutumia mbegu bora zinazostahimili ukame.

“Wananchi pia waweke mbolea kwenye mashamba yao na wapande mbegu kulingana na utaalam wa ofisa kilimo,” amesema Kijika.

TMA ilisema katika msimu wa mvua za vuli za mwaka huu, kutakuwa na  upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza hasa mikoa ya nyanda za juu kaskazini na ukanda wa pwani ya kaskazini ambapo hali hii inaweza kuathiri ukuaji wa mazao. 

“Ongezeko la visumbufu vya mazao kama mchwa, viwavi jeshi, panya na magonjwa vinatarajiwa kujitokeza katika msimu na hivyo kuathiri mazao na uzalishaji kwa ujumla,” ilieleza TMA katika taarifa yake.

Wakulima wanashauriwa kupanda mbegu na mazao yanayoweza kukomaa ndani ya muda mfupi na yanayostahimili ukame na kutumia mbinu na teknolojia za kilimo himilivu za kuhifadhi maji.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW