Mvua kuanza kunyesha Dar, Pwani
- Ni baada ya kupitia vipindi virefu vya ukavu licha ya kuanza msimu wa masika.
- Mikoa mingine ni Tanga, Visiwa vya Zanzibar, Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
- Zitapungua tena kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Aprili.
Dar es Salaam. Baada ya baadhi ya mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikiwemo Dar es Salaam kupitia vipindi virefu vya ukavu licha ya kuanza msimu wa masika, mikoa hiyo itaanza kupata mvua kama kawaida, jambo linalotoa matumaini kwa wakulima kufaidika na kilimo.
Msimu wa mvua za masika ni mahususi kwa maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, mikoa ya Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).
Maeneo mengine yanayopata aina hizo za mvua ni ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
“Unyeshaji wa mvua unatarajiwa kuimarika katika baadhi ya maeneo mwishoni mwa mwezi Machi, 2022 na mwanzoni mwa mwezi Aprili, 2022,” imeeleza taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) iliyotolewa Machi 28 mwaka huu.
Baadhi ya maeneo ya mikoa iliyopitia vipindi virefu vya ukavu ni pamoja na Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Zanzibar, Manyara, Arusha na Kilimanjaro.
“Vipindi hivyo virefu vya ukavu vimesababishwa na matukio ya vimbunga hususan kimbunga Gombe kilichodumu kwa muda mrefu katika Bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji pamoja na kujitokeza kwa joto la bahari la chini ya wastani katika eneo la pwani ya Afrika Mashariki,” imeeleza TMA katika taarifa yake.
Soma zaidi:
- TMA yatahadharisha ujio mvua kubwa
- Watanzania washauriwa kutumia taarifa za hali ya hewa kwenye mipango ya maendeleo
- Ujio mfumo wa taifa wa hali ya hewa kuchochea ujenzi wa viwanda nchini
Hali hiyo imechangia pia Ukandamvua (ITCZ) kuendelea kusalia katika maeneo ya kusini mwa nchi ambapo kwa kawaida katika kipindi cha mwanzoni mwa mwezi Machi huanza kuelekea maeneo ya kaskazini mwa nchi.
Licha ya kuwa mvua hizo kunyesha vizuri katika kipindi hicho, TMA imesema mvua zitapungua tena kati ya wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Aprili hususani kwa katika mikoa hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Agnes Kijazi aliyekuwa akitoa utabiri wa mwelekeo za mvua msimu wa masika za Machi hadi Mei 2022 jijini Dar es Salaam Februari 17, 2022 alisema mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Aidha, kusalia kwa ukandamvua katika maeneo ya kusini kumesababisha mvua za msimu kuendelea kunyesha kwa kiwango cha kuridhisha katika baadhi ya maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka mikoa ya Mbeya, Iringa, Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Dk Hamza Kabelwa akitoa taarifa ya mwelekeo wa msimu wa mvua za masika katika kipindi cha Machi hadi Mei 2021 amesema maeneo mengi ya nyanda za juu kaskazini mashariki na ukanda wa Ziwa Viktoria yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.
Latest