Kampuni tatu zafutiwa mikataba upimaji ardhi Mwanza

January 27, 2021 7:02 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kampuni za Edibm Land Engineering Constraction, Spatial Planning Vision na Geoid Geomatics Constraction Enterprises.
  • Kampuni hizo zimeshindwa kutimiza wajibu wao wakupima viwanja vya wananchi. 

Mwanza. Serikali  imevunja mikataba iliyoingia na kampuni  tatu  za upimaji wa ardhi mkoani Mwanza baada ya kushindwa kutekeleza kazi ya upimaji viwanja  katika baadhi ya kata za wilaya ya Nyamagana na Misungwi na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh152 milioni kwa wananchi na na halmashari hizo.

Kampuni zilizofutiwa kazi ni pamoja na Edibm Land Engineering Constraction ambayo ilipokea fedha zaidi ya Sh66 milioni kutoka kwa wananchi kwa ajili ya kupima  viwanja 1,550 badala yake  imepima viwanja 41. 

Kampuni hii ilitakiwa kutekeleza majukumu yake katika kata ya Kishiri wilayani Nyamagana.

Kampuni nyingine ni  Spatial Planning Vision iliyopokea zaidi ya Sh49 milioni kwa ajili ya kupima viwanja 3,650 katika maeneo ya Igumo na Nyang’anga  lakini mpaka sasa imepima viwanja 900.

Nayo Kampuni ya Geoid Geomatics Constraction Enterprises iliyokabidhiwa Sh37 milioni kupima viwanja 3,777 katika maeneo ya Mwasonge B, Seth Benjamin na Nyamwikumulo lakini haijafanikiwa.

“Serikali haiwezi kuvumilia makampuni ambayo hayatekelezi kazi kwa wakati  na yanamikataba ya muda mrefu na mengine zaidi ya miaka miwili, hatuwezi kuvumilia na ninaagiza vyombo vya dola vichukue hatua ili fedha za wananchi ziweze kurudi,” ameagiza  Naibu Waziri Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula’

Mabula ametoa maagizo hayo katika kikao cha pamoja kilichokutanisha  watendaji wa ardhi kutoka halmashari zote za mkoa wa Mwanza huku akiwataka watendaji hao kuhakikisha suala zima la ardhi linakwenda vizuri  na migogoro inatatuliwa.


Zinazohusiana:


Katika hatua nyingine  Naibu Waziri huyo  ametoa miezi mitatu kwa wataalam wa sekta hiyo, kuwafutia umiliki wa ardhi watu ambao waliokwisha kupata  hati ya maandishi (NOTICE) lakini wameshindwa kulipia kodi ya ardhi .

Amesema kwa kufanya hivyo kutasaidia kufikia lengo la Mkoa wa Mwanza kukusanya zaidi ya Sh15.2 bilioni ambapo hadi sasa wamefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh4.2 bilioni. 

Kaimu Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Mwanza, Elia Kamihanda amesema mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kila wilaya inakuwa na baraza la ardhi ili kurahisisha  upatikanaji wa huduma kwa mwananchi.

Katika kikao hicho pia kilikutanisha wadaiwa sugu wa ardhi 122 ambao walipewa siku 14 kuhakikisha wanalipa madeni yao kabla hatua zingine za kisheria hazijachukuliwa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW