Zaidi ya Sh1 bilioni zitakavyobadilisha maisha ya wakulima wa pamba Tanzania

December 8, 2022 1:08 pm · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link

Naibu waziri wa Kilimo, Antony Mavunde akikabidhi vifaa vya kilimo kwa maofisa ugani wa wilaya za Magu, Misungwi na Kwimba kwa ajili ya kufuatilia kilimo cha pamba. Picha | Mariam John.


  • Ni wakulima wa Mkoa wa Mwanza ambao wamesogezewa mradi wa kujengewa uwezo.
  • Watawezeshwa kulima kisasa na kuongeza uzalishaji wa pamba.

Mwanza. Zaidi ya wakulima wadogo 9,000 wa zao la pamba mkoani Mwanza  wanatarajia kunufaika na mradi wa  uendelezaji wa zao hilo ili waweze kuzalisha tija na kufaidika na masoko ya kimataifa. 

Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) kilichopo Ukirigulu wilayani Misungwi,, Dk Paul Saidia amesema mradi huo uliopewa jina la  “Beyond The Cotton” umelenga kuwajengea uwezo  wakulima katika wilaya tatu za Misungwi, Kwimba na Magu ili waweze kuongeza uzalishaji wa pamba.

Amesema mbali na zao hilo pia mradi huo unatarajia kuongeza thamani ya mazao mengine yanayolimwa na wakulima ili kusaidia usalama wa chakula na lishe  kukabiliana na udumavu.

“Mradi huo wa kundeleza zao la pamba umefadhiliwa na Serikali ya Brazil kwa Dola za Marekani 629,000 (Sh1.5 bilioni), utatekelezwa katika wilaya tatu za Magu, Misungwi na Kwimba utawafikia wakulima wadogo 9,000,” amesema  Dk Saidia. 

Mbali na mradi huo pia Serikali imetoa vitendea kazi vitakavyowasaidia wataalamu wa kilimo waweze kuwafikia wakulima kutoa huduma za ugani kwa wakati pamoja na kuwarahisishia wakulima kutekeleza mradi huo.

Katibu Tawala Msadizi (Kilimo) Mkoa wa Mwanza, Emil Kasagala amesema wanaishukuru Serikali kuleta mradi wa kuendeleza zao la pamba chakula na lishe.

Kasagala amesema katika msimu huu, Mkoa wa Mwanza umelenga kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka tani 500 hadi 600.

“Tunaweza kufikia malengo hayo ikiwa tutakuwa na zana bora za uzalishaji hivyo ni matarajio yetu kuwa malengo ya Serikali na mradi yanafikiwa,” amesema. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi zana za kilimo na vyombo vya usafiri kwa maofisa ugani wa wilaya ya Magu, Misungwi na Kwimba, Naibu Waziri wa kilimo, Antony Mavunde amesema kilimo hakiwezi kuendelea bila utafiti, hivyo watafiti waendelee kufanya utafiti kubuni mbinu na kuja na teknolojia mbalimbali ili kukuza sekta ya kilimo.

Amesema kilimo kina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na kuwashauri wakulima wa zao la pamba na mengine ya chakula na lishe wafuate kanuni sahihi na kutumia zana na teknolojia kuongeza tija na ufanisi katika kazi.

Aidha, Mavunde ameitaka TARI kuendelea kutafuta miradi yenye tija ya aina hiyo na ambayo italeta matokeo yanayoshikika.

Vifaa vilivyokabidhiwa ni pikipiki tatu kila wilaya, zana za kulimia (rotary mashine), mashine rahisi moja ya kutengeneza nguo na mkaa mbadala.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW