Sintofahamu wafanya usafi wakigoma kushinikiza kulipwa mishahara Mwanza
- Hawajalipwa mishahara kwa zaidi ya miezi sita.
- Kampuni iliyowaajiri yatupa mpira kwa Ofisi ya Jiji Mwanza.
- Serikali yasema itachukua hatua wafanyakazi hao walipwe.
Mwanza. Wafanyakazi 60 wa kampuni ya usafi ya Green West ya jijini Mwanza, wamegoma kuendelea na shughuli ya usafi wakishikiza kampuni hiyo kuwalipa mishahara ya Sh50 milioni ambazo hawajalipwa kwa zaidi ya miezi sita sasa.
Wakizungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wafanyakazi hao ambao mgomo wao umedumu kwa wiki mbili sasa wamesema ni kwa muda sasa wamekuwa wakidai mishahara hiyo bila mafanikio.
“Kila tunapodai mishahara tunapewa ahadi isiyotimilika na sisi tuna familia tunatakiwa kula na kutekeleza majukumu mengine lakini hatulipwi mishahara yetu,” anasema Tatu Bituro, mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Tatu (62) ni mjane anayetegemewa na wajukuu wawili amesema amekuwa akifanya kazi kwenye kampuni hiyo kwa muda mrefu bila kupatiwa malipo yake hali inayosababisha ashindwe kuwahudumia wajukuu wake.
Amesema alianza kazi hiyo baada ya mumewe kufariki kwenye ajali ya Mv Nyerere iliyotokea mwaka 2018.
“Nimepanga chumba kimoja sina mtu ninayemtegemea. Ninategemewa na wajukuu wawili waende shule na wale hivyo ninashindwa namna ya kuwapatia mahitaji ya msingi kama chakula pamoja na mahitaji yao ya shule kutokana na kutokuwa na chanzo kingine cha kipato,” amesema Tatu.
Mfanyakazi mwingine Vedastus Jonathan ambaye ni dereva wa gari amesema wamejaribu kufuatilia stahiki zao hadi ngazi ya wilaya ambapo Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana aliiagiza kampuni hiyo kulipa stahiki zote ndani ya mwezi mmoja lakini bado kampuni hiyo ikazidi kukiuka agizo hilo.
Soma zaidi:
Akizungumzia changamoto hiyo, Meneja wa Kampuni ya Green West, Salum Madata amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kwamba na wao kama kampuni wanaidai Halmashauri ya Jiji la Mwanza zaidi ya Sh100 milioni ambazo hawajalipwa kwa muda mrefu.
Madata amesema tayari suala hilo wamelifikisha ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwa ajili ya hatua zaidi ambapo Mkuu wa Mkoa, John Mongella ameagiza kampuni hiyo ilipwe ili iweze kulipa wafanyakazi wake.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi amesema alipokea malalamiko ya wafanyakazi hao na kwamba tayari baadhi ya matatizo yameanza kutatuliwa ikiwa ni pamoja na kuagiza mamlaka nyingine kuchukua hatua.
Hali tete mitaani
Wafanya usafi hao wamekuwa watu muhimu katika kulifanya jiji hili kuwa safi na mwonekano mzuri. Hata hivyo kugoma kwao kunaweza kukawa na athari mbaya kwa mazingira hasa kuzagaa kwa taka kunakoweza kusababisha magonjwa kwa wananchi.
Nukta Habari imetembelea maeneo ambayo kampuni hiyo ilikuwa inakusanya taka ya Nyamagana, Igogo, Mkolani na Nyegezi na kushuhudia taka zikiwa zimezagaa mitaani, jambo ambalo siyo kawaida katika maeneo hayo.
Baadhi ya wananchi wanasema hali hiyo ikiendelea, afya zitakuwa reheni.
“Mazingira yamebadilika, taka zimeanz akusagaa mitaani. Tunahofia watoto wetu kupata magonjwa. Tunaomba Serikali itupatie ufumbuzi,” amesema Mbokwa Bugoma, mkazi wa jijini hapa.
Latest