Kitulo ‘Bustani ya Mungu’ fahari ya Nyanda za Juu Kusini

Daniel Mwingira 0911Hrs   Agosti 14, 2018 Safari
  • Ina maua aina 350 ambapo aina 40 hayapatikanani sehemu yoyote duniani
  • Imepakana na mikoa ya Njombe na Mbeya 

Dar es Salaam. Watu wengi wanadhani sehemu sahihi ya kutalii ni kaskazini mwa Tanzania yaani katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga ambako kunatajwa kuwa na vivutio vingi. 

Lakini milango imefunguliwa Nyanda za Juu Kusini, ambako kumesheheni vivutio vingi vya utalii ambavyo vikitumiwa vizuri vitaongeza mapato ya Taifa, ajira na uchumi wa mtu mmoja mmoja. 

Moja ya kivutio ambacho kinasifika kwa upekee wake ni ‘Bustani ya Mungu’ maarufu kama Hifadhi ya Taifa ya Kitulo ambayo ni ya 14 kuanzishwa hapa nchi mwaka 2005. Hifadhi hiyo ina ukubwa wa kilomita za mraba 365

Sehemu kubwa ya hifadhi hii ambayo kama zilivyo hifadhi zingine nchini Tanzania, inasimamiwa na kuratibiwa na Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), imetapakaa katika mikoa miwili ya Mbeya na Njombe. Eneo tengefu la hifadhi hii, limejumuisha safu za Kitulo na sehemu ya safu za milima ya Livingstone, ikiwa ni hifadhi ya kwanza kabisa kutambulika katika ukanda wa Kitropiki katika Afrika, kuwahi kuanzishwa kwa minajili ya utunzaji wa mimea asilia ambayo sehemu kubwa ni maua.

Utakayokutana nayo Hifadhi ya Kitulo

Fahari ya Hifadhi ya Kitulo ni ndege aina ya Tandawili machaka (Denhams Bustard) akiwa ni ndege anayeweza kuruka kutoka bara moja hadi jingine.

Kwa mujibu wa Hifadhi za Taifa (TANAPA),Ndege huyo hutumia hifadhi ya kitulo kama eneo pekee la kutagia mayai na kuzaliana kabla ya kwenda katika mabara mengine ya Ulaya, Australia na nchi ya jirani ya Afrika Kusini. 



Ukiwa Kitulo utapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo kupanda Mlima LivingStone ambao uko karibu na ziwa Nyasa, kupanda farasi, michezo ya gofu.  Sambamba na hilo watalii wanaotembelea hifadhi hiyo watapata upepo mwanana kutoka mwambao wa ziwa Zambwe na milio tofauti ya ndege wanaopamba hifadhi hiyo.   

Kinachoitofautisha Kitulo na hifadhi zingine ni uwepo wa Bustani ya Mungu ambayo ina aina 350 za maua ambapo aina zaidi ya 40 zinazojulikana kama "Orchids" hazipatikanani sehemu nyingine yoyote duniani isipokuwa katika hifadhi hiyo ambayo unaweza kuitumia kwa mapumziko ya mwisho ya mwaka.


Unafikaje Kitulo?

Na ukiachilia mbali tatizo la miundombinu ya kufika Kitulo kuwa sio ya ubora, bado ni rahisi sana kufika katika hifadhi hii, ambayo iko umbali wa takriban kilomita 110 tu kutoka yalipo makao makuu ya Mkoa wa Mbeya ambao ni kiungo cha nchi za Malawi na Zambia.

Kama utatumia usafiri wa ndege utatua uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Songwe ambapo ni kilomita 90 kama utapita mji wa Isyonje na 125 km kama utapita kati mji wa Chimala wilayani Mbarali. Lakini kwa wanaingilia mkoa wa Njombe ni kilomita 165 mpaka kufika Kitulo na utatumia barabara ya Ikonda hadi Makete. 

Inaelezwa kuwa hakuna mabasi rasmi yenye kufika sehemu hiyo ya hifadhi, kwasababu wakazi wa Mbeya bado hawana mwamko wa masuala ya utalii. Lakini kwa watu wenye nia ya kufika Hifadhi ya kitulo wanaweza kutumia usafiri wa kampuni za usafirishaji watalii  kama Gazelle Safaris ambazo zitakuchukua popote wakiwa Mbeya. 

 



Related Post