Tanzania yaongeza bajeti maliasili, utalii kwa 3.4%
- Yaongezeka kwa asilimia 3.4 kulinganisha na Sh348.13 bilioni ya mwaka 2024/25.
- Kamati imeitaka Serikali kuboresha mfumo wa fidia kwa waathirika wa migongano na wanyamapori.
Dar es Salaam. Serikali imeongeza kidogo bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa asilimia 3.4 licha ya kuwepo kwa changamoto lukuki zinazoikabili sekta hiyo zikiwemo ujangili na migogoro kati ya binadamu na wanyamapori.
Bajeti ya mwaka ujao wa fedha unaoanza Julai 2025 imependekezwa kuwa Sh359.98 bilioni ikiwa ni ongezeko la Sh11.86 bilioni kutoka Sh348.13 bilioni zilizoidhinishwa na Bunge katika mwaka 2024/2025.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Pindi Chana aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni leo jijini Dodoma Mei 19, 2025, amewaambia wabunge kuwa kati ya fedha zilizoombwa Sh254.23 bilioni zimetengwa kwa matumizi ya kawaida, huku Sh105.74 bilioni zikielekezwa kwenye miradi ya maendeleo.

“Fedha za matumizi ya kawaida zinajumuisha Sh130.7 bilioni za mishahara na Shilingi Sh123.52 bilioni kwa matumizi mengineyo,” amesema Dk Chana.
Katika fedha za miradi ya maendeleo zinazotarajiwa, Sh32.48 bilioni zitatoka katika vyanzo vya ndani na Sh73.27 bilioni kutoka nje ya nchi.
Ili kuokoa maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu, Dk Chana amesema Serikali ilivuna wanyamapori 296 wakiwemo mamba 63, viboko 63, tembo 34, nyati 15, fisi 71, simba 10 na chui mmoja.
Wizara hiyo inaomba bajeti hiyo katika kipindi ambacho ina mahitaji makubwa ya kulinda maliasili ikiwemo misitu na wanyamapori kutoka kwa majangili na uvamizi wa maeneo ya uhifadhi kutoka kwa watu wanaosaka kufanya shughuli za kiuchumi na makazi.

‘Boresheni sheria ya TTB’
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imesema bajeti hiyo itasaidia utekelezaji wa ushauri wa Bunge ulioruhusu taasisi kama Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) kuanza kubaki na makusanyo yao badala ya kuyaingiza moja kwa moja kwenye mfuko mkuu wa Serikali.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Timotheo Mnzava amesema kamati imeshauri kuandaliwa sheria maalum itakayounda chombo huru cha usimamizi wa fedha hizo ili kuhakikisha matumizi yake yanakuwa na uwazi na tija kwa wananchi.
Kamati hiyo imeitaka Serikali kuboresha mfumo wa fidia kwa waathirika wa migongano na wanyamapori ili kuongeza uharaka na ufanisi wa malipo, pamoja na kuweka uzio wa umeme kwenye maeneo yanayoathirika zaidi na migongano hiyo.
Vilevile, imependekeza kufanyika kwa marekebisho ya sheria ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), ili kuipa uwezo zaidi wa kujitegemea na kuongeza ufanisi katika kutangaza vivutio vya utalii vya nchi yetu kimataifa.
Wizara kuendelea kutangaza utalii
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara itatekeleza vipaumbele mbalimbali vikiwemo kuendelea kutangaza utalii wa Tanzania kimataifa kupitia matangazo katika ligi za michezo maarufu, mashindano ya kimataifa, mashirika ya ndege, matamasha, misafara maalum ya utangazaji na mitandao ya kimataifa pamoja na vyombo vya habari.
Vipaumbele vingine ni kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati kama maeneo ya malikale, fukwe, mikutano, meli, michezo, tiba na utamaduni sambamba na kuboresha miundombinu ya utalii na uhifadhi ikiwemo barabara na viwanja vya ndege.

Dk Chana amesema wizara yake pia itaimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa rasilimali na shughuli za utalii, kulinda wanyamapori, misitu, nyuki na malikale, kuongeza uzalishaji wa mazao ya misitu na nyuki, pamoja na kuimarisha takwimu na tafiti za uhifadhi.
Latest



