Wizara ya Uchukuzi yaomba Sh2.746 trilioni kutekeleza vipaumbele nane
- Ni pamoja na kuimarisha usalama na mawasiliano kwenye usafiri na usafirishaji katika maziwa makuu nchini na uendelezaji na uendeshaji wa viwanja vya ndege.
Dar es salaam. Wizara ya Uchukuzi imeliomba Bunge liidhinishe bajeti ya Sh2.746 trilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele nane ikiwemo kuendelea na ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) katika ushoroba wa kati.
Waziri wa Uchukuzi Prof Makame Mbarawa aliyekuwa akiwasilisha maombi hayo bungeni leo Mei 15, 2025 amewaambia wabunge kuwa bajeti hiyo inajumuisha fedha kwa ajili ya mishahara ya watumishi, matumizi mengineyo na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya ndani na nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi, bajeti hiyo inaenda kutekeleza vipaumbele kama kununua vitendea kazi na kuboresha reli zilizopo, kuendelea kuboresha kampuni ya ndege Tanzania na kuboresha miundombinu na huduma katika bandari nchini .

Vipaumbele vingine ni kuimarisha usalama na mawasiliano kwenye usafiri na usafirishaji katika maziwa makuu nchini, uendelezaji na uendeshaji wa viwanja vya ndege.
“Kuendelea na ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli zilizopo na kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji,” anabainisha Prof Mbarawa.
Hata hivyo, bajeti inayoombwa imeongezeka kwa Sh16.8 bilioni ukilinganisha na mwaka wa fedha 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 0.61 ambapo wizara iliidhinishiwa jumla ya Sh2.729.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Selemani Kakoso, uchambuzi wa bajeti umebaini kuwa, fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida imeongezeka kwa asilimia 9.23 kutoka Sh114.74 bilioni mwaka 2024/25 hadi Sh125 bilioni mwaka huu.
Aidha, bajeti kwa ajili ya miradi ya maendeleo imeongezeka kutoka Sh2.61 trilioni hadi Sh2.62 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 0.23.

Miradi mbalimbali inayotaraijiwa kutekelezwa 2025/26
Prof Mbarawa amesema wizara yake pamoja na taasisi zilizo chini yake zitaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR na uboreshaji wa kampuni ya ndege Tanzania.
Pia, uboreshaji wa usalama wa usafiri na usafirishaji katika bahari na maziwa makuu, mradi wa uboreshaji wa bandari ya Dar es salaam, mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Mwanza mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Arusha mradi wa ujenzi wa kiwanda cha ndege cha Mtwara.
Vilevile, mradi wa ukarabati wa kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro na mradi wa ujenzi na uendelezaji wa viwanja vya ndege vya mikoa ya Lindi na Bukoba.
Latest



