Viongozi wa upinzani walalamikia kusuasua zoezi la kujiandikisha daftari la kupiga kura Mwanza
- Uchache wa vituo vya uandikishaji watajwa kuwa sababu.
- Uandikishaji wafikia asilimia 63 Mwanza.
Mwanza. Ikiwa zimebakia siku mbili kukamilika kwa zoezi la kujiandikisha katika daftari la kupiga kura la Serikali za Mitaa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani wamelalamikia kusuasua kwa zoezi hilo kunakochangiwa na uchache wa vituo vya uandikishaji.
Zoezi la uandikishaji katika daftari la kupiga kura la Serikali za Mitaa linaendelea nchi nzima, lilianza Oktoba 11 na litakamilika Oktoba 20 mwaka huu.
Idd Kasimu, Mwenyekiti wa Chama cha Union for Multi-Party Democracy Tanzania (UDM) Mkoa wa Mwanza aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Oktoba 18, 2024 amesema baadhi ya wananchi wanasuasua kushiriki kujiandikisha kupiga kura kutokana na Serikali kuwachagulia wawakilishi badala ya wale waliowachagua.
“Zipo sababu nyingi lakini hili la kuminywa kwa uhuru wa wananchi kuchagua viongozi wanaowataka inachangia zoezi hili kusuasua,” amesema Kassimu.
Mbali na madai hayo, viongozi hao wamelalamikia ucheleweshwaji wa taarifa kwenda kwa vyama vya siasa ili viweze kujiandaa ikiwemo kuweka wawakilishi katika kila kituo.
” Mfano taarifa ya zoezi la uandikishaji kwenye daftari hili la mpiga kura taarifa inakuja zimebaki siku tano na vyama vinatakiwa kupeleka mawakala jambo ambalo kwa vyama vichanga haviwezi kutimiza…hivyo ni vyema zoezi kama hili taarifa zije mapema ili kuvipa vyama kuandaa watu kwa ajili ya kusimamia,” amesema Hassan Mohamed, Katibu UMD.
Wananchama wa Chama cha UMD wakiwa kwenye picha ya pamojana baada ya mkutano na waandishi wa habari. Picha| Mariam John/ Nukta Africa.
Uandikishaji wafikia asilimia 63 Mwanza
Wakati viongozi hao wakilalamikia kusuasua kwa zoezi la kujiandikisha, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amesema zoezi la uandikishaji linakwenda vizuri na mpaka leo Oktoba 18, 2024 wamefanikiwa kuandikisha kwa asilimia 63.
Tofauti na malalamiko ya vyama hivyo Mtanda huyo amesema mawakala wa vyama vya siasa wapo vituoni kuhakiki zoezi hilo na hakuna chama ambacho kimezuiwa kupeleka mawakala wake.
” Hakuna chama ambacho kimezuiwa kupeleka mawakala vyama vyote vinaruhusiwa na nitoe wito kwa wasimamizi wa zoezi hilo la uchaguzi kuhakikisha wanazingatia kanuni na taratibu za uchaguzi,” amesema Mtanda