INEC: Uchaguzi mkuu kufanyika Oktoba 29, 2025

July 26, 2025 11:58 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza rasmi kuwa uchaguzi mkuu wa Tanzania utafanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume hiyo Jaji Jacobs Mwambegele ,aliyekuwa akitangaza ratiba hiyo leo Julai 26, 2025 amesema ratiba hiyo imetolewa kwa mujibu wa mamlaka iliyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na sheria mbalimbali za uchaguzi.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, utoaji wa fomu za uteuzi kwa wagombea wa urais na makamu wa rais utafanyika kuanzia Agosti 9 hadi 27, wakati uteuzi rasmi wa wagombea utafanyika Agosti 27. 

Kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, kabla ya siku ya kupiga kura ambayo ni Oktoba 29, 2025 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

“Tarehe 28 Agosti 2025 hadi tarehe 27 Oktoba 2025, kitakuwa kipindi cha kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Zanzibar ili kupisha kura ya mapema,’’ amesema Jaji Mwambegele kabla ya siku ya kupiga kura ambayo ni Oktoba 29, 2025 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Aidha, tume hiyo imeeleza kuwa jumla ya wapiga kura milioni 37.7 wamejiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura kwa mwaka 2025, wakiwemo milioni 36.6 kutoka Tanzania Bara na milioni 1.4 kutoka Zanzibar.

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na wapiga kura milioni 29.8 waliojiandikisha mwaka 2020

Kati ya waliojiandikisha wanawake ni milioni 18.9  sawa na asilimia 50.31 na wanaume ni milioni 18.7  sawa na asilimia 49.69. 

Katika idadi ya waliojiandikisha watu wenye ulemavu 49,174 wamejiandikishwa, sawa na takribani asilimia 0.13 ya jumla ya wapiga kura.

INEC wamefafanua kuwa  jumla ya wapiga kura wapya milioni 7.6 wameandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura sawa na asilimia 136.79 ya makadirio ya awali ya kuandikisha wapiga kura milioni 5.5.

Hata hivyo, Jaji Mwambegele amesisitiza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 114 cha Sheria ya Uchaguzi namba 1 ya mwaka 2024, ni kosa la kisheria kujiandikisha zaidi ya mara moja. 

“Wapiga kura 8,703 wamebainika kujiandikisha zaidi ya mara moja, mkurugenzi wa uchaguzi katika hafla hii atakabidhi orodha hiyo kwa Jeshi la Polisi ili liendelee na hatua za kisheria,” ameeleza Jaji Mwambegele.

Uboreshaji wa daftari hilo ulifanyika kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ilianza Julai 20, 2024 hadi Machi 2025, na awamu ya pili ilifanyika kuanzia Mei 1 hadi Juni 25, 2025.

Jumla ya vyama 18 vya siasa vimeshiriki katika mchakato wa uchaguzi mwaka huu, vikiwemo Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chama cha ACT-Wazalendo, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA).

Kuelekea uchaguzi mkuu Octoba 29, 2025, INEC imebainisha kuwa vituo 99,991 vitatumika kupiga kura katika majimbo 272.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks