Inawezekana: Mwalimu wa shule msingi, wenzie walivyoanzisha kiwanda cha ‘gypsum’ Tanzania
- Ni mwalimu Frank Maduka (31) mkazi wa Kata ya Usagara wilayani Misungwi mkoani Mwanza ambaye hufundisha elimu ya msingi.
- Kiwanda hicho chaanzishwa baada ya biashara ya mbogamboga kufeli.
- Vijana wenzie katika kikundi hicho wasema angalau kiwanda hicho kimewapatia ajira tofauti na awali.
Mwanza. Kuna watu wengi huishi nje ya ndoto zao. Baadhi hufanya vibaya kati baadhi ya mambo lakini huwa wazuri kwenye mengine ambayo siyo kipaumbele za kazi au masomo kwa wakati huo.
Hii ndiyo maana si ajabu yule aliyekuwa wa mwisho darasani ndiye akaja kuwa bosi wako baadaye.
Hata hivyo, baadhi licha ya kuendelea kufanya jambo fulani, bado wanaendelea na ndoto zao akiwemo Frank Maduka (31) mkazi wa Kata ya Usagara wilayani Misungwi mkoani Mwanza.
Kijana huyu ni mwalimu wa Shule ya Msingi Mwanjombo wilayani Misungwi ambaye anajaribu kuzihuisha ndoto zake ambazo hapo awali hazikuweza kutimia kwa kuanzisha kiwanda kidogo cha kutengeneza mikanda ya jasi kwa Kiingereza ‘Gypsum’ kwa ajili ya ujenzi na chaki.
Kiwanda hicho kilichopo eneo la Mawe matatu wilayani Misungwi, amekianzisha na kikundi cha wenzie wanane.
Maduka ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa kabla ya wazo hilo awali walijishughulisha na kilimo cha mbogamboga na matunda ambacho hakikuzaa matunda. Mafanikio hasi katika ukulima yalimfanya ageukie ufundi.
“Ni wazo alilokuja nalo mwanakikundi mwenzetu na tukaliona kuwa linafaa, tukaamua kutembelea moja ya kiwanda cha kutengeneza mikanda kilichopo mkoani Pwani kwa ajili ya kujifunza,” anasema Maduka.
Anasema baada ya wazo hilo kufanikiwa mwaka 2018 walianzisha kiwanda hicho ambacho kilizinduliwa na kiongozi wa mbio za mwenge mwaka 2019 baada ya kuridhishwa na utendaji wake.
Sehemu ya mtaji uliotumika kuanzisha kiwanda hicho ni Sh2 milioni ilitokana na biashara ya awali ya kikundi ya kuuza mbogamboga.
Fedha nyingine za kuanzishia kiwanda ukiachana na zile zilizotoka kwenye mbogamboga na matunda, zilitokana na michango yao wenyewe pamoja na mkopo kwa vikundi vya kina mama, vijana na walemavu.
Jumla ya fedha walizokusanya vijana hao zilisaidia kununua mashine ya chaki Sh11 milioni pamoja na vifaa vingine vya kutengenezea mikanda na maua mbalimbali, kununua kiwanja kwa ajili ya kiwanda hicho.
Tofauti na wengi ambao huwaza kuhusu viwanda vidogo, eneo la kiwanda hiki siyo kubwa sana.
Mfano, nyumba wanayotengenezea chaki ina chumba kimoja na sebule na ni kama nyumba hizi za kawaida za kuishi. Vijana hawa hawana mitambo mikubwa lakini kinachowebeba ni viwango vya ubora walivyothibitishwa na mamlaka ikiwemo Shirika la kuhusu viwanda vidogo (Sido).

Mmoja wa watengenezaji wa mikanda ya jipsam, Awadhi Haji akitengeneza mikanda ya jasi ambayo hutumika kwa ajili ya ujenzi. Picha na Mariam John.
Namna anavyomudu majukumu
Pamoja na kuwa ni mwanzilishi mwenza wa kiwanda hiki, kijana huyu ni mwalimu anayetakiwa kutumia muda wake kikamilifu kuwafundisha watoto wa elimu ya msingi. Mwalimu huyu mcheshi kidogo, hufundisha kuanzia darasa la kwanza hadi la saba masomo Hisabati na Jiografia
Maduka anasema anaweza kugawa muda wake na kutekeleza majukumu yake vizuri bila ya kuwa na changamoto za ufanisi katika maeneo yote mawili.
Ili kutimiza majukumu ya kiwandani, anaeleza kuwa mara zote hutumia muda wa jioni baada ya kutoka shuleni na kuingia kiwandani kukagua kazi ilivyoenda na siku za Jumamosi na Jumapili.
Anasema hiyo haiathiri shughuli za ufundishaji kwa kuwa anatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Zinazohusiana:
- Zana zitakazokusaidia kukuza biashara yako mtandaoni
- Simulizi ya mjasiriamali aliyesota miaka 14 kuanzisha kiwanda cha sabuni Mbeya
Vipi kuhusu uzalishaji?
Kwa siku, kiwanda hicho huzalisha mikanda 300 na bosi 100 za chaki. Bidhaa zote hizo kwa pamoja huuzwa kwenye maeneo mbalimbali wilayani Misungwi na nje ya wilaya.
Kwa upande wa utengenezaji wa mikanda ya jasi, Maduka anasema kwa siku wanazalisha mikanda 100 na wanasambaza kwenye maduka ya vifaa vya ujenzi huku wateja wao wakubwa ni wa wanaokamilisha nyumba zao, nyumba za taasisi na mashirika mbalimbali.
Awali uzalishaji ulikuwa uko chini kwa sababu wananchi wengi hawakupenda vitu vinavyozalishwa nchini, hata walipopeleka kwenye maduka ya vifaa vya ujenzi havikupokelewa moja kwa moja kwa kuwa waliaminishwa kuwa havina kiwango kile kinachostahili.
Lakini kutokana na kuungwa mkono na viongozi wa serikali ya wilaya ya Misungwi sasa bidhaa kutoka katika kiwanda cha kina Maduka zimeanza kukubalika na wa wengi wanaokamilisha ujenzi huenda kununua kwao.
Anasema zamani walikuwa wanazalisha mikanda 50 lakini ilikuwa inakaa mda mrefu bila kununuliwa licha ya kuwa bei ya mkanda mmoja ni Sh2,000, bei ya chini zaidi ya ile inayoingizwa kutoka nje ya nchi.
Mpango uliopo kwa sasa kuhusu kiwanda hicho ni kukiendelea kwa kuzalisha zaidi ili kupanua wigo pamoja na kuongeza ajira kwa vijana kwa ajili ya uzalishaji.
Kutokana shughuli kupanuka kidogo, kiwanda hicho kinatarajia kuajiri watano kwa ajili ya utengenezaji wa chaki pamoja na wasambazaji.
“Baada ya Serikali kutusajilia kiwanda chetu uongozi wa wilaya uliagiza shule zote zinunue chaki kwenye kiwanda hiki ingawa kwa sasa sio sana kama maagizo yalivyotolewa,” anasema Maduka.
Mauzo kwa sasa angalau yanatia matumaini kuliko ilivyokuwa awali, Maduka anasema, huku akigoma kueleza kiundani kiwango cha ukuaji mapato hayo.
Mwalimu Frank Maduka akionyesha moja ya mkanda wa jipsam uliotengenezwa ambapo mmoja huuzwa Kati ya Sh2000. Picha|Mariam John/Nukta.
Bado kuna mlima kufikia mafanikio
Upatikanaji wa malighafi kwa ajili ya kutengenezea bidhaa hizo ni magumu hususan kwenye ‘fiberglass’ (malighafi mahususi katika utengenezaji bidhaa za jasi) na vifungashio havipatikani hapa nchini na mara zote hupatikana nje ya nchi.
Anasema malighafi ya unga wa jasi yanapatikana hapa nchini na ni bora kama ule unaoingizwa kutoka nje.
Kuhusu ubora wa bidhaa hizo, Mwalimu Maduka anasema gypsum zinazotengenezwa hapo no bora na nzito kuliko zile zinazotengenezwa nje ya nchi ambapo nyingi huwa nyepesi kulingana na unga wanaotumia mwingi ukiwa umechakachuliwa.
Kuna matumaini ya kufika kileleni
Wanakikundi walioanzisha kiwanda hiki na Maduka wanasema kuwa mbali na kutoa huduma kwa jamii, kimewasaidia kupata ajira.
Awadhi Haji ni mmoja wa wanakikundi anasema toka ajiunge na kikundi hicho anasema amejihakikishia ajira iliyomsaidia kuendesha maisha yake tofauti na ilivyokuwa awali.
“Kutokana na shughuli hii naweza kupokea Sh200,000 tofauti na zamani ambapo kipato kilikuwa cha kusuasua,” anasema huku akibainisha kuwa matarajio yake ni kuwa tajiri mkubwa siku za mbeleni.
Latest