Haina kusubiri: Wanavijiji walivyoamua kupunguza wanafunzi 100 darasa moja
- Wakazi wa Mbogwe waanza mdogo mdogo kumaliza msongamano wa wanafunzi madarasani.
- Wachoka kuisubiria Serikali kuwatatulia matatizo yao.
- Darasa moja Shule ya Sekondari Masumbwe linabeba wanafunzi hadi 100.
Dar es Salaam. Wakiwa shuleni huwa wanatamani kama wangekaa kwa nafasi wapate hewa nzuri na usaidizi wa karibu wa walimu wao kama wenzao wenye madarasa mengi na walimu wa kutosha.
Baadhi ya wanafunzi wa Sekondari hii ya Masumbwe iliyopo wilaya ya Mbogwe mkoani Geita tangu waanze kidato cha kwanza hawajawahi kukaa chini ya wanafunzi 90 ndani ya darasa moja.
Happiness Shelembi, mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Masumbwe anasema msongamano wa wanafunzi katika darasa analosoma unatishia ufaulu wake katika masomo kwa sababu hapati maarifa inavyotakiwa.
“Madarasani tunakua wengi, tumebanana…hali ya darasani inakuwa ni joto huwezi kujisikia vizuri na kumsikiliza mwalimu huwa ni shida. Viti vipo vichache,” anasema Happiness mwenye umri wa miaka 17.
Happiness, ambaye mwaka huu atafanya mtihani wa kidato cha nne, ana wasiwasi kama atafanya vizuri katika mtihani huo kutokana na mazingira duni ya kujifunzia ikilinganishwa na wenzie wanaosoma shule binafsi zenye mahitaji yote muhimu.
Hata hivyo, huenda msongamano wa wanafunzi madarasani katika Shule ya Sekondari Masumbwe ukapungua siku za hivi karibuni baada ya wananchi kuanza kujenga madarasa mapya kumaliza tatizo hilo.
Shule hiyo, yenye takriban miaka 16 tangu ianzishwe, ina vyumba vya madarasa 21 vinavyotumiwa na wanafunzi 2,013 wakiwemo wavulana 969 wa kidato cha I hadi IV.
Kwa idadi hiyo ya wanafunzi, darasa moja linatumiwa na wastani wa wanafunzi 95. Wingi huo wa wanafunzi umefanya madarasa na walimu kuzidiwa kiasi cha kuhudumia wanafunzi mara mbili zaidi ya kiwango kinachotakiwa.
Uwiano huo hauko sawa ikilinganishwa na maelekezo ya Serikali ambayo yanataka darasa moja litumiwe na wanafunzi 45 ili kumsaidia mwalimu kuwafikia wanafunzi wote ili kurahisisha kazi ya ufundishaji.

Ili kukidhi mahitaji ya shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Masumbwe iliyopo Kata ya Nyakafuru wilayani Mbogwe, Yusuph Mguma anasema wanahitaji vyumba vya madarasa 40.
“Tuna upungufu wa vyumba 18,” anasema Mguma na kubainisha kuwa katika baadhi ya madarasa wanafunzi wanakaa hadi 100.
Kutimiza angalau mahitaji ya msingi ya wanafunzi hao, Mguma anasema wanafanya jitihada mbalimbali kuhakikisha wanatumia rasilimali zilizopo wakiwemo walimu 48 kufundisha hata kama darasa limefurika wanafunzi ili kutokuwakosesha kabisa maarifa wanayotakiwa kuyapata.
“Inaathiri zoezi zima la ujifunzaji na ufundishaji kwamba mwalimu analazimika kutumia mbinu moja tu ya kuhubiri, hawezi akatembea darasani kwa sababu ya msongamano mkubwa na kumuhudumia mwanafunzi mmoja mmoja,” anasema Mguma akiwa ofisini kwake hivi karibuni.
Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2010 inaitaka Serikali kuweka mazingira mazuri ya kusomea kwa ajili ya watoto ikiwemo ujenzi wa madarasa yanayokidhi mahitaji ya wanafunzi waliopo shuleni.
Hata hivyo, Mkuu wa shule hiyo, Mguma anasema upungufu huo wa madarasa haujaathiri sana ufaulu wa shule hiyo katika mitihani ya kitaifa kwa sababu wapo wanafunzi wenye uwezo mzuri na kati.
“Mfano mwaka jana kidato cha nne tulikuwa na zero 40 kati ya watoto 280. Pamoja na msongamano ule tuliweza kuwa na division one 11 (daraja la kwanza 11),” anasema mkuu huyo wa shule.
Moja ya darasa linalotumiwa na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Masumbwe likiwa na mdawati mengi ambayo inakuwa siyo rahisi kwa mwalimu kumfikia kila mwanafunzi. Picha| Gift Mijoe.
Wazazi waanza ‘mdogo mdogo’
Huenda kilio cha wanafunzi wa shule hiyo kikakauka hivi karibuni baada ya wadau wa elimu na wazazi wa kata ya Nyakafuru kuanza jitihada za kujenga madarasa mengine katika eneo hilo la shule bila kuisubiri Serikali.
Katibu wa mgodi wa madini ya dhahabu wa Nyakafuru uliopo Mbogwe, Steven Petro anasema yeye na wenzake wameamua kuwa sehemu ya kumaliza tatizo hilo kwa kujenga vyumba vya madarasa vinne na ofisi moja ya walimu shuleni hapo.
“Sisi siyo kwamba tunapata fedha nyingi sana ili tufanye haya, ni moyo wa kujitolea, moyo wa uzalendo tumeona kuna huduma za kijamii ambazo Serikali yetu inajitahidi kuzitekeleza lakini na sisi kama wananchi inatakiwa tushiriki kwenye kuisaidia ili iweze kufika mahali fulani ya kukidhi mahitaji ya jamii,” anasema Petro.
Petro anasema majengo hayo yaliyogharimu Sh172 milioni yatasaidia kupunguza uhaba wa madarasa shuleni hapo na hivyo kuinua elimu ya watoto wa Mbogwe.
“Kwa kiwango fulani itasaidia kupunguza tatizo la mbanano wa watoto katika madarasa machache yaliyopo hapa shuleni,” anasema Petro na kuongeza kuwa wanatengeneza madawati 500 yatakayotumiwa katika madarasa hayo waliyojenga.
Moyo huo wa kujitoa wa wakazi wa Mbogwe katika shughuli za maendeleo unatokana na dhana ya uraghabishi iliyojengeka katika fikra zao ambayo inahimiza wananchi kutekeleza miradi ya maendeleo bila kuisubiri Serikali.
“Huu mwamko siyo bure watu wameelimishwa umuhimu wa kujiletea maendeleo,” anasema Elias Kelela, Mwenyekiti wa Kijiji cha Masumbwe.
Ili kumaliza kabisa uhaba wa madarasa katika Shule ya Masumbwe, wakazi wa Nyakafuru wanaendelea kuchanga fedha na vifaa kujenga vyumba vya madarasa ili kukidhi mahitaji ya shule hiyo.
Uhaba wa madarasa ni tatizo ambalo linaikumba Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe. Takwimu zilizotolewa Idara ya Elimu wilayani humo zinaeleza kuwa hadi kufikia Juni mwaka huu shule za sekondari 16 za wilaya hiyo zilikuwa na madarasa 169 ambayo yanatumiwa na wanafunzi 98,071. Hadi sasa halmashauri hiyo ina upungufu wa madarasa 20.
Takwimu muhimu za elimu (BEST 2020) zilizotolewa na Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Geita ilikuwa madarasa 1,736 na kufanya uwiano wa darasa moja kuhudumia wastani wa wanafunzi 56, juu kidogo ya wastani wa wanafunzi 45 (1:45) unaopendekezwa na Serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbogwe, Pastory Mukaruka anasema ni kweli shule hiyo imekuwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi na Serikali imeanza kutatua changamoto hiyo kwa kujenga vyumba vya madarasa vipya kadri fedha zinavyopatikana.

Mukaruka anasema wataendelea kushirikiana na wananchi kumaliza tatizo hilo ili kuwawezesha wanafunzi kupata mazingira mazuri ya kusomea na kuwawezesha kufaulu.
Latest