Simulizi ya mjasiriamali aliyesota miaka 14 kuanzisha kiwanda cha sabuni Mbeya

Daniel Samson 0737Hrs   Agosti 15, 2018 Ripoti Maalum
  •  Alianza safari ya kusaka maarifa na mtaji wa kutengeneza sabuni mwaka 2004.
  • Anaamini katika ubora na ubunifu wa soko.
  • Kiwanda hicho alichoanzisha kwa sasa kimeajiri watu wanane wa muda wote na kutoa fursa kwa wafanyabiashara wadogo wadogo.

Mbeya. Alikuwa na ndoto tangu mwaka 2004 ya kuja kumiliki kiwanda cha sabuni lakini hakuifikia ndoto hiyo kwa siku moja kwa kuwa alikuwa hafahamu kabisa hatua za kutengeneza bidhaa hiyo. 

Sasa Nuru Njumbo, mjasiriamali na mmiliki wa kiwanda kidogo cha Afri Soap cha kutengeneza sabuni za unga na miche wilayani Kyela katika mkoa Mbeya ameanza kuifikia ndoto hiyo baada ya miaka ya 14 ya mahangaiko ya kusaka maarifa na mtaji wa kutengeneza sabuni kwa kutumia mafuta ya mawese na mbosa.

“Hakuna kitu kisichowezekana, toka pale (mwaka 2004) nikawa nimepata wazo kumbe hiki kitu kinawezekana,” anasema Njumbo.

Njumbo amefanikiwa kufungua kampuni ya Ufunde and Associates ambayo inasimamia kiwanda hicho cha sabuni kilichopo eneo la Darajani Kata ya Ipyana nje kidogo ya mji wa Kyela.

Mafuta ya Mawese na mbosa ni zao la miti ya michikichi ambayo hulimwa katika wilaya hiyo na maeneo mengine nchini. Mafuta hayo yana uwezo wa kutengeneza sabuni ya maji, unga na mche.

Wakati anaanza kutengeneza sababuni hizo kwa mkono mwaka 2004 alikatishwa tamaa na watu kwamba asingeweza kuwa na kiwanda ambacho kingeajiri wafanyakazi wanaozalisha sabuni zenye ubora unaokidhi ushindani wa soko ndani na nje ya wilaya hiyo.

“Vijana wengi wapo hiki kitu wanakiona isipokuwa wana zile tabia za mazoea kwamba hiki kitu hakiwezi kufanyika hapa mpaka kifanyike sehemu nyingine,” anabainisha Njumbo na kuongeza kuwa utashi na matamanio aliyokuwa nayo ya kujiajiri na kumiliki kiwanda yaliweza kuzishinda fikra hasi alizokutanazo wakati wa akitimiza ndoto yake.

Mmiliki wa kiwanda cha kutengeneza sabuni cha Afri Soap, Nuru Njumbo akitoa maelekezo kwa wafanyakazi wake baada ya kumaliza uzalishaji. Picha| Daniel Samson.

Alianza kutengeneza sabuni baridi kwa mkono akiwa nyumbani mara tu baada ya kupata mafunzo kutoka kwa wakufunzi wake. Hata hivyo, uzalishaji ulikuwa mdogo kwa kuwa alikuwa anatengeneza miche 10 hadi 20 kwa siku kwa sababu ya kukosa malighafi na teknolojia ya kisasa ikiwemo mashine na rasilimali watu.

Hali hiyo ilimuongezea hamasa ya kutafuta mtaji na maarifa kuingia katika soko la ushindani kwa kutengeneza sabuni zenye ubora zitakazoweza kushindana na sabuni za viwanda vikubwa nchini. 

“Wakati ule tunafanya zile shughuli tukawa tunajaribu kuangalia namna ya kushindana kwenye soko. Tunapotengeneza sabuni ambayo haiko kwenye viwango mara nyingi mlaji anajua hii sabuni ni ya kienyeji,” anasema Njumbo.

Mwanzo mwa mwaka huu kampuni yake ilifanikiwa kununua mashine mbili kubwa ya kuchanganyia mafuta ya mawese na mbosa na ile inayotumika kuunganisha na kukata miche ya sabuni. 

“Kwa kutumia hizi mashine tumeweza kutengeneza sabuni ambazo zimeingia kwenye ushindani wa soko,” anasema.

 Shughuli ya uzalishaji sabuni ya miche ikiendelea kwenye kiwanda kidogo cha Afri Soap. PIcha| Daniel Samson.

Kwa sasa kiwanda hicho kimeajiri vijana wanane ambao wana uwezo wa kuzalisha miche 2,000 hadi 3,000 (sawa na katoni 200 hadi 300) kwa siku ambapo ni mara 200 zaidi ya teknolojia ya mkono aliyokuwa akitumia miaka 14 iliyopita.

Kiwanda cha Afri Soap kinachomilikiwa na mtanzania mzawa ni taswira halisi ya juhudi za Serikali za kuhamasisha wananchi kujenga viwanda vidogo vidogo ili kutumia rasilimali za kilimo kuongeza pato la Taifa na kutokomeza umaskini katika jamii.

Takwimu za Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji za mwaka 2018 zibainisha kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu, Tanzania ilikuwa na viwanda 53,876 vikiwemo vidogo vidogo 46,495 sawa na asilimia 86.3. Hii ina maana kuwa katika kila viwanda 100 vilivyopo nchini, 86 ni viwanda vidogovidogo.


Hata hivyo uzalishaji  kiwanda cha Afri Soap haukidhi mahitaji ya soko la  wakazi wote wa Kyela kutokana na kukosekana kwa mtaji na malighafi za kutosha za mawese. Lakini changamoto hizo hazimzuii Njumbo kuendelea kubuni njia mbadala kuongeza uzalishaji kwa sababu bidhaa waliyoichagua ni sahihi.

“Hii sabuni mtu anaitumia toka anapozaliwa mpaka anapofariki, tumefikiri kitu ambacho hakitaisha leo kwenye soko na mahitaji yanaendelea kuwa makubwa kila siku,” Njumbo ameiambia Nukta.


Thamani ya uzalishaji sabuni za mawese

Kinachoipa thamani kiwanda hicho ni matumizi ya mafuta ya mawese na mbosa ambayo yanatokana na miti ya michikichi inayostawi zaidi katika wilaya hiyo, jambo linalotengeneza mnyororo wa thamani ya uzalishaji na soko kwa wakulima na wajasiriamali kama Njumbo.

Mafuta ya mawese yamezoeleka kutumiwa katika upishi wa vyakula lakini mafuta hayo yanahitajika kwa ngozi ya mwili wa binadamu ili kumpa afya na muonekano mzuri.

“Tunatumia mbosa na mawese kwasababu; kwanza mawese yana fati na vitamini inayoweza kurutubisha ngozi ya mwili na mbosa kazi yake inaongeza povu kama chumvi ndani ya mboga,” anafafanua Njumbo.

Sabuni hizo zinaweza kutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kufuria, kuogea, kuoshea vyombo kulingana na aina ya sabuni iliyotengenezwa ikizingatiwa kwamba kiwanda hicho kinatengeneza sabuni za mche, maji na zile za unga.

Vifaa na mashine zinazotumika kutengeneza sabani kiwandani hapo. Picha| Daniel Samson.

Akieleza jinsi sabuni hizo zinavyotengenezwa, Msimamizi wa uzalishaji, Jackson Lyemamu anasema sabuni hizo ni matokeo ya  mchanganyiko wa malighafi nne (mafuta ya mbosa, mawese, na caustic soda).

“Tunachukua mawese ambayo tayari yamechujwa kwenye mashine za wakulima, tunayachemsha tukiwa tunatafuta rangi ya sabuni tunayoitaka sisi kama ni ya kaki, nyeupe au njano. Baada ya hapo tunachanganya na mafuta ya mbosa ambayo ni kama asilimia tano kwa sababu yanatumika kama kionjo kuifanya sabuni iwe laini,” anaeleza Lyemamu na kuongeza kuwa

“Tukiweka kwenye mchanganyiko wetu tunachukua ‘caustic soda’ tunaitumia ikiwa bado ya moto tunachanganya na maji halafu tunamimina kwenye mashine ya mchanganyiko wa mawese na mbosa. Mashine hiyo huchanganya kwa dakika 10 na kuchemsha unakuwa uji ulio tayari kutumika. Baada ya hapo tunaimwaga kwenye turubai chini na muda wa dakika 15 inakuwa imeganda tunaikatakata kwenye vipande vidogo vidogo,” anaeleza Lyemamu.

Hatua ya mwisho ni kuvipitisha vipande hivyo kwenye mashine kutoa miche ya sabuni ambayo hukatwa kwa kipimo kinachohitajika tayari kwa kupangwa kwenye vifungashio na kupangwa kwenye maboksi na kupelekwa sokoni.

Pamoja na kwamba kuna upatikanaji mkubwa wa sababu nyingine zilizotengenezwa kisasa kutoka kwenye viwanda vikubwa chini katika eneo lao, wakazi wa Kyela wanapenda sabuni za Afri soap kwa kuwa zinawapa ufahari wa kuwa na kiwanda.

Mkazi wa Kyela, Loth Mwangamba ambaye anatumia sabuni hizo, anasema kiwanda hicho kitachochea kilimo cha michikichi na kuinua maisha ya wakulima wa zao hilo la biashara kwa sababu kinategemea zaidi mafuta ya zao hilo kuzalisha sabuni zenye ubora na bei inayoendana na soko.

Licha ya kuwa kiwanda hicho kinatumia malighafi inayopatikana Kyela, Njumbo anasema kuna wakati mawese huadimika kwa kuwa wakulima wa eneo hilo hawatumii teknolojia ya kisasa katika uzalishaji wa mafuta hayo.

Hata hivyo, wakulima wameiambia Nukta kuwa mawese hulimwa kama utamaduni tu na si kibiashara kwa kuyachanganya na mazao mengine jambo linalofanya washindwe kuzalisha zao kwa wingi na kusaidia kulisha kiwanda hicho kidogo.

Iwapo wangekuwa wanajua umuhimu wa mawese na kuwa na uhakika wa soko kama ilivyo sasa baada ya kuanzishwa kiwanda hicho, Charles Mwakajonga anasema kwa sasa mawese yanazalishwa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kama mafuta ya kupikia.

"Ila tupo tayari kuzalisha kwa wingi mawese iwapo vitakuja viwanda vingi zaidi na kutuhakikishia soko," anasema Mwakajonga.


Related Post