Matumaini mapya baada ya ujenzi wa shule kukwama miaka mitatu Kigoma

August 26, 2021 1:43 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni shule ya sekondari inayojengwa katika kata ya Kipampa Manispaa ya Kigoma/Ujiji. 
  • Serikali yaeleza kuwa mwaka 2022 itakuwa imekamilika na kudahili wanafunzi.
  • Wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi watamani ingekamilika mapema.

Kigoma. Mzee Hussein Kasekeseke mkazi wa Kata ya Kipampa katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji bado anajiuliza ni nini kilikuwa kimekwamisha ujenzi wa shule ya sekondari aliyoshiriki mchakato wa kuijenga mwaka 2018. 

Mzee huyu na wakazi wenzie wa kata hiyo mkoani Kigoma walishiriki katika hatua za awali za ujenzi wa shule hiyo kwa michango na nguvu kazi wakiwa na matumaini kuwa ingeisha mapema na watoto wao kuanza kupata elimu. 

Miaka mitatu baadaye, majengo ya shule hiyo bado hayajakamilika. Hadi sasa kuta za madarasa bado ni fupi zisizozidi hata mita mbili kwenda juu. 

Majengo hayo yaliyojengwa karibu na Shule ya Msingi Ujiji yamezungukwa na nyasi kuonyesha kuwa ujenzi umesimama kwa muda mrefu.  

“Kulikuwa na msako mkali kwa wasiochanga…tukahamasisha watu kuchangia, walijitolea lakini hakuna lolote, wananchi wanasikitika,” anasema Kasekeseke (74) aliyekuwa kiongozi wa ulinzi shirikishi katika mtaa wao wakati wa kuhamasisha ujenzi wa shule hiyo.

“Wananchi walijitoa kweli kweli kila mtu alikuwa akichanga Sh3,000, walijitoa kwa hali na mali. Tunashindwa kuelewa kabisa nini kilitokea.”

Tofauti na miaka mitatu iliyopita, kwa sasa Kasekeseke hana nguvu tena ya kufuatilia kiundani masuala yaliyokwamisha ujenzi wa shule hiyo iliyopo mita 30 mbele ya makazi yake mtaa wa Kawawa. 

Tofauti na kata nyingine za Kigoma/Ujiji, Kipampa haina shule ya sekondari jambo linalofanya watoto wanaofaulu elimu ya msingi kwenda kusoma sekondari nyingine za manispaa hiyo ambazo baadhi zipo mbali na makazi yao. 

Mzee Hussein Kasekeseke mkazi wa Kata ya Kipampa katika Manispaa ya Kigoma/Ujiji mwenye shauku ya kuona kata yake inapata shule ya sekondari ili wanafunzi wapate eneo zuri wapate mazingira mazuri ya kusomea. Picha| Gift Mijoe.

Nini kilikwamisha ujenzi wa shule hiyo? 

Kumaliza tatizo hilo, wakazi wa kata hiyo walikubaliana kujenga shule hiyo baada ya vikao vya kuibua kero kufanyika huku mbinu ya uraghabishi ikitumika kushawishi watu wengi zaidi kushiriki ujenzi wa shule hiyo. 

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kipampa, Leonard Kajembe anasema vikao vya awali viliazimia shule hiyo ijengwe katika eneo hilo ila baadaye ilibainika kuwa hapatoshi licha ya kuwa ujenzi ulikuwa umeshaanza.

“Kipampa haina maeneo makubwa ya wazi kujenga shule hivyo kuna eneo la kilimo ambalo lilichaguliwa lililohitaji fidia lakini mkurugenzi alisema hana fidia. Diwani wetu alifanikiwa kupata mfadhili wa kulipa fidia lakini kiwango kilichotakiwa cha Sh200 milioni kilikuwa kikubwa sana,” anasema Kajembe. 

Kajembe, ambaye aliingia katika kata mwaka 2019, anasema baadaye vikao viliazimia kuwa badala ya mfadhili huyo kulipa fidia ni bora asaidie kujenga madarasa manne katika eneo la zamani ambalo tayari shughuli za ujenzi zilikuwa zimeshaanza. 

“Tunaamini hadi mwakani tutakuwa tayari na sekondari,” anasema. 

                       

Mchakato wa kusubiria kumaliza taratibu za kupata ardhi hiyo mpya ulichochea kwa kiwango kikubwa shule hiyo kukwama licha ya baadhi ya viongozi na wakazi wa eneo hilo kusema siasa ilichangia kukwamisha ujenzi wa shule hiyo. 

“Mkwamo wa jambo hili ilikuwa na issue (jambo) ya kisiasa,” anasema Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma/Ujiji, Frednand Fillimbi akieleza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kata zote zina shule za sekondari ikiwemo Kipampa.

Fillimbi anaeleza kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) na ACT Wazalendo walikuwa wakivutana kuhusu mradi huo jambo ambalo kwa sasa limeshaisha. 

“Tumeshakubaliana shule ile ijengwe na mikakati thabiti ipo vizuri kuhakikisha inakamilishwa. Wananchi wazaliwa wa Kigoma wamethibitisha kufadhili ujenzi, wao watajenga vyumba vinne vya madarasa…watafikisha kwenye level (hatua) ya linta na sisi tutamalizia kwenye mwaka wa fedha unaokuja (2021/22),” anasema. 

Majengo ya shule ya sekondari iliyopo Kata ya Kipampa yaliyojengwa karibu na Shule ya Msingi Ujiji yakiwa yamezungukwa na nyasi kuonyesha kuwa ujenzi umesimama kwa muda mrefu. Picha| Gift Mijoe.

Matumaini mapya yanakuja, yanakata

Ahadi hizo za Serikali zinafanya watoto wa kata hii iliyopo kilomita chache kutoka katikati ya manispaa kuendelea kusubiri zaidi huku wanaomaliza darasa la saba wakiwa hawana matumaini ya kuanza kuitumia. 

Hata wanafunzi waliopo madarasa ya nyuma ya elimu ya msingi akiwemo Zena Shaban (10) anayesoma darasa la tano katika Shule ya Msingi Ujiji wana matumaini huenda wakasoma itakapokamilika.

“Nilikuwa napenda nikimaliza shule ya msingi nije nisome katika shule hii ya sekondari kwa kuwa ni karibu sana na nyumbani ila sidhani kama itakuwa imeisha,” anasema Rajab Adam, mwanafunzi mwingine wa Shule ya Msingi Ujiji. 

“Sioni kama kuna kitu kitaendelea hapa,” anasema mwanafunzi huyo huku akinyoosha mkono kwenye mapagala ya shule hiyo. 

Maumivu kwa wanaosoma mbali

Hadi sasa wanafunzi wa sekondari wanaotoka kata hiyo wanasoma shule za jirani ambazo baadhi hutumia hadi saa 2 kwenda shule.

“Tunapata tabu sana kwa kuwa unatakiwa uamke asubuhi sana uanze safari ya shule Saa 12 na unafika Saa 1 au 2 asubuhi. Kuna wakati unakuta kipindi cha kwanza au mitihani ya asubuhi imeshaanza na imeshanitokea kama mara saba hivi mwaka jana,” anasema Juma Salum, mwanafunzi wa Sekondari Rusimbi anayetokea kata ya Kipampa. 

Wazazi wa kata hiyo kwa sasa hawataki tena kusikia ahadi kwa kuwa baadhi watoto wao wamekosa fursa ya kuendelea na masomo licha ya kuwa walijitoa kuchangia maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo.

Ahadi tu sasa basi!  

Chiku Sadiki, mkazi wa Mtaa wa Kawawa anasema kuna watoto wengi walifaulu masomo elimu ya msingi miaka ya nyuma lakini ukosefu wa shule uliwafanya wakose fursa mapema ya kuanza kidato cha kwanza.

“Kuna wakati watoto wanafaulu ila wanakosa nafasi ya kusoma. Wale wanaobahatika kupata nafasi baadaye wanaanza masomo Mei au Juni wakati wenzao wameshajifunza kwa sehemu kubwa,” anasema Chiku (65). 

“Tunaomba Serikali imalizie shule hii kwa haraka.”

Watoto wengi katika manispaa hii wanategemea shule za umma baada ya takwimu za msingi za elimu Tanzania (BEST) mwaka 2020 zilizotolewa na Ofisi ya Rais-Tamisemi kuonyesha kuwa wanafunzi 12,940 kati ya 14,504 wa elimu ya sekondari walikuwa wakisoma katika shule hizo mwaka 2020. 

Wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za umma ni mara nane ya wale wanaosoma shule binafsi katika manispaa hiyo waliokuwa 1,564 mwaka 2020. 

Wanafunzi wote hao wanategemea shule za sekondari 20 za Serikali katika manispaa hiyo ambazo ni theluthi mbili au asilimia 66.7 ya shule 30 zilizopo. 

Manispaa ya Kigoma/Ujiji ndiyo halmashauri inayoongoza kwa idadi kubwa ya shule za umma za sekondari katika mkoa wa Kigoma uliokuwa na shule 140 mwaka jana. 

Wadau wengine wa maendeleo katika manispaa hiyo wanasema Serikali inapaswa kukamilisha mradi huo kwa wakati kwa kuwa ukiendelea kuchelewa utazidi kukatisha tamaa wananchi wa mkoa huo kujitoa kwa ajili ya maendeleo yao. 

Hamza Selemani, Katibu wa chama cha waraghabishi Manispaa ya Kigoma/Ujiji anasema walichangia sana kuhamasisha maendeleo katika ujenzi wa shule hiyo iliyokwama na kwamba itakuwa ni vema ikakamilishwa mapema ili wanafunzi waanze kujifunza. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW