Maabara inayobebeka inavyowainua kielimu wanafunzi Kanda ya Ziwa
- Inawawezesha wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi kwa njia rahisi.
- Imebuniwa na vijana wenye ndoto ya kukuza sekta ya teknolojia nchini.
- Wanafunzi shule za msingi wasema wameanza kupenda masomo ya sayansi.
Mwanza. Huenda muamka wa wanafunzi wa shule za msingi kusoma masomo ya sayansi ukaongezeka baada ya wabunifu kuendelea kubuni njia rahisi za kujifunza masomo hayo.
Masomo ya sayansi kwa kawaida huitaji kujifunza kwa vitendo na majaribio ili kupata matokeo mazuri ya kile mwanafunzi anachojifunza kwa nadharia.
Hata hivyo, uhaba wa walimu wa masomo hayo na maabara zenye vifaa, imekuwa kikwazo kwa wanafunzi wengi kutokubobea katika fani ya sayansi na teknolojia na hivyo kukimbilia kwenye masomo ya sanaa.
Katikati ya changamoto hizo, vijana wabunifu wanabuni njia rahisi kuwawezesha wanafunzi kujifunza masomo ya sayansi kwa ufanisi popote walipo bila hata kuhitaji jengo la maabara.
Hapa ndipo inakuja dhana ya ‘maabara inayotembea au kubebeka’. Ikiwa na maana kuwa mwanafunzi anaweza kubeba vifaa vya majaribio kwenye boksi.
Moja ya wabunifu hao ni Wilison Mabala, Mkurugenzi na mwanzilishi wa maabara inayobebeka ya MITz group iliyopo Nyakato jijini Mwanza.
Ni Mtanzania, baba wa watoto watatu, lengo lake ni kuona watoto wanajifunza kwa vitendo na si kukaririshwa masomo ya sayansi.
Baada ya kuhitimu chuo kikuu akichukua kozi ya uhandisi wa mawasiliano pepe aliona ipo haja ya kuwarahisishia wanafunzi wa shule za msingi kusoma masomo ya sayansi.
Mwaka 2019 ndio mwaka pekee wa safari ya kufikia matarajio yake, akiwa na wenzake walianza kazi ya kutengeneza maabara inayobebeka kwa kutumia teknolojia ya 3D na PCD ambazo zinachapisha kitu kama kilivyo.
Mpaka sasa kikundi hicho ambacho kimesajiliwa na kutambulika serikalini ikiwemo ofisi ya Waziri Mkuu, kimefanikiwa kutengeneza aina nane za vifaa ambavyo vinatumika katika shule za msingi na sekondari katika majaribio mbalimbali ya somo la fizikia.
Baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi mkoani Mwanza wakifanya majaribio ya kisayansi kwa kutumia vifaa vilivyotengenezwa katika maabara ya MITz. Picha | Mariam John.
Kazi kuu hapa ni kuhakikisha watoto hasa wa shule za msingi kuanzia darasa la tatu wanapata maarifa zaidi ya kutumia teknolojia kwa vitendo kuliko kukaririshwa.
“Tulifanya utafiti kidogo kwenye mitaala ya elimu ya msingi iliyopo kwa sasa na kubaini kuwa pamoja na mapungufu yaliyopo lakini bado walimu wanashindwa kuwafundisha wanafunzi kwa vitendo kutokana na kukosa teknolojia za kufundishia,” anasema Mabala
Katika ofisi ya MITz, wanafunzi wanafundishwa maarifa mbalimbali ya kutengeneza vitu vya umeme mwendo yakiwemo magari yanayojiendesha yenyewe na vitu vingine vingi.
“Kwa mfano shule nyingi za msingi hawafanyi mazoezi ya vitendo hivyo kupitia vifaa hivyo mwanafunzi anaweza kujifunza na kuongeza maarifa,” anasema Mabala.
Anasema katika ulimwengu huu, teknolojia inaweza kubadilisha maisha hivyo vijana wanaofundishwa leo, baada ya miaka 10 hadi 15 ijayo watakuwa ni vijana wa zao la hicho ambacho wanawafundisha leo.
Soma zaidi:
-
Kitendawili cha maabara shule za sekondari Mbeya
-
Kutana na Aneth David mwanasayansi anayechipukia Tanzania
-
Kutana na wanasayansi wa kike wanaotikisa mashindano ya ulimbwende Tanzania
Wanajivunia nini?
Pamoja na kufanikia kusajili kikundi chao, MITz group inajivunia kuwafundisha watoto zaidi ya 8,000 kutoka maeneo mbalimbali. Wapo ambao wanafanya vipindi katika shule zao na wengine hupata maarifa katika ofisi zao zilizopo Sido Nyakato jijini Mwanza.
Mbali na kufundisha mashuleni pia kikundi hicho kinajikita katika masuala ya utafiti ambayo inatambulika na ofisi ya Waziri Mkuu.
Viongozi wanafunzi waunga mkono juhudi
Baadhi ya wanafunzi waliozungumza na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wanasema vifaa vilivyobuniwa na kampuni hiyo vimerahisisha usomaji wao wa masomo ya sayansi.
Aloys Martin ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Winners anasema tofauti na zamani kwa sasa wanaweza kutengeneza vitu vingi vinavyotumia umeme.
“Sasa naweza kujifunza na kufanya kwa vitendo, hii itaongeza ufaulu kwenye masomo yangu, tunashukuru taasisi hiyo kwa kuja na wazo hili,” anasema Aloys
Mwanafunzi mwingine, Mariam Aron amesema pia wanafundishwa namna ya kutumia kompyuta kutengeneza vitu mbalimbali.
Maabara ya MITz hutoa fursa kwa wanafunzi wa shule za msingi kutumia ofisi yake kufanya majaribio ya kisayansi kwa kutumia vifaa vilivyotengenezwa kwa teknolojia rahisi. Picha | Mariam John.
Mwalimu wa shule ya msingi Winners ambayo ni moja ya shule zinazofundishwa na taasisi hiyo, Aron Mussa anasema kampuni hiyo itasaidia kukata mzizi wa wanafunzi wengi kukimbia masomo ya sayansi wakiamini kuwa ni masomo magumu.
Anasema kinachofanywa na kampuni hiyo ni ishara ya kuzalisha wanafunzi wengi wanaojua masomo ya sayansi.
“Na sio kujua tu watazalisha wanafunzi wengi wenye utaalam wa mambo yanayohusiana na sayansi hivyo kuwa na taifa ambalo watu wake wanaweza kujitengenezea vitu vyao wenyewe kuliko kuagiza nje,” anasisitiza Mussa.
Mwalimu huyo anasema kinachosababisha wanafunzi wengi washindwe kufanya vizuri kwenye masomo yao ya sayansi ni kukosa msingi mzuri wa masomo yao tangu wakiwa wadogo.
“Sasa mwanafunzi anaenda kujifunza kwa vitendo akiwa sekondari na tena anafundishwa namna ya kujibia mtihani lakini kwa sasa tutegemee kuwa na wanafunzi wengi wanaohitimu shule wakiwa na uwezo mkubwa wa kufanya vitu kwa vitendo lakini pia kuwa na idadi kubwa ya wanaopenda masomo ya sayansi,” anasema mwalimu huyo.
Wazazi nao hawakuwa nyuma kuzungumzia suala hilo wakieleza kuwa kulingana na mitaala ya elimu wanafunzi hawanabudi kuanza kusoma masomo hayo.
“Ni kweli kuwa wanafunzi wengi walikuwa wanakimbilia masomo ya sanaa kutokana na aina ya ufundishwaji wa masomo ya sayansi shuleni, lakini kwa kuwa hivi sasa msingi unaanzia shule za msingi utahamasisha wanafunzi wengi kujifunza kwa vitendo,” anasema Nehemia Jilala, mkazi wa Buhongwa Mwanza.
Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) mkoani Mwanza, Bakari Songwe anasema kitendo kilichofanywa na vijana hao ni cha kibunifu ambacho kitaisaidia jamii hasa wanafunzi kuweza kujifunza kwa vitendo.
“Ni ubunifu mkubwa ambao umekuja na vijana hao ambapo wanafunzi badala ya kujifunza kwa nadharia sasa wataweza kujifunza kwa vitendo na kuongeza maarifa zaidi kwenye masomo yao.
Sido ambayo ni mlezi wa MITz Group inaeleza tayari kikundi hicho kimetambuliwa na kusajiliwa na sasa kinakamilisha mambo kadhaa ili kiweze kuuza bidhaa zake ndani na nje ya nchi.
“Vifaa vinavyotengenezwa hapa vitasaidia katika kuongeza na kukuza uchumi wa nchi kwakuwa vitasaidia katika program za masomo ya sayansi hususani kemia na fizikia ambayo yanafundisha kuanzia shule ya msingi hadi sekondari,” anasema Songwe.
Latest
