Idadi ya watalii yaongezeka baada ya kushuka kwa miezi miwili mfululizo

- Idadi ya watalii walioingia nchini Oktoba ilikuwa 141,517 ikiongezeka kutoka 133,998 iliyorekodiwa Septemba.
- Mwaka 2022 kuvunja rekodi ya miaka miwili kupungua kwa watalii.
Dar es Salaam. Baada ya idadi ya watalii wanaoingia Tanzania kushuka kwa miezi miwili mfululizo, idadi hiyo imeanza kuongezeka tena, jambo linaloashiria kuwa kutakuwa na mwenendo mzuri wa ukuaji wa sekta ya utalii nchini siku zijazo.
Kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu za Oktoba 2022 (High Frequency Data), idadi ya watalii walioingia nchini Oktoba ilikuwa 141,517 ikiongezeka kutoka 133,998 iliyorekodiwa Septemba.
Hilo ni sawa na ongezeko la watalii 7,519 au asilimia 5.6.
Kuongezeka kwa idadi hiyo kumekuja baada ya idadi ya watalii kushuka miezi miwili mfululizo. Julai mwaka huu Tanzania ilirekodi watalii 166,736 na mwezi uliofuata wakapungua hadi 158,049 kabla hawajapungua zaidi hadi 133,998 mwezi Septemba.
Zinazohusiana:
- Maajabu ya visiwa 11 ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Rubondo
- Ndani ya Ifisi: Hifadhi ya wanyamapori inayotoa pumziko kwa wakazi wa Mbeya
- Ijue milima 10 mirefu zaidi Tanzania
Licha ya kuwa idadi ya watalii imekuwa ikipanda na kushuka tangu Januari, huenda mwaka 2022 utarekodi idadi kubwa ya watalii katika kipindi cha miaka miwili iliyopita baada kutoka katika athari za janga la Corona (Uviko-19).
Mwaka 2020, Tanzania ilipokea watalii 620,867 lakini mwaka uliofuata wakaongezeka hadi 922,692 na huenda wakaongezeka zaidi mwaka huu na kuvunja rekodi.
NBS inaeleza kuwa hadi kufikia Oktoba, watalii milioni 1.17 walikuwa wametembelea vivutio mbalimbali nchini tangu mwaka 2022 uanze.
Idadi hiyo iko juu ikilinganishwa na miaka miwili iliyopita huku nchi za Kenya, Burundi na Marekani zikiongoza kuingiza watalii wengi zaidi.
Miezi 10 iliyopita, Kenya imeingiza watalii 130,970 ikifuatiwa kwa mbali na Burundi (85,269) na Marekani watalii 83,025.
Tanzania imejiwekea malengo ya kufikia watalii milioni 5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025. Ili kufikia lengo hilo imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha utalii wa fukwe na mikutano na kujitangaza zaidi kimataifa ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Latest