Haujachelewa kutimiza ndoto zako! Anza sasa

February 23, 2021 11:05 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Inahitaji kuwa na mipango madhubuti ya kukamilisha ndoto zako.
  • Subira ni jambo ambalo kila mwenye ndoto anatakiwa kuwa nalo kwani mafanikio  huja hatua kwa hatua.
  • Umri, muda na fedha zisiwe chanzo cha kupotea katika rada yako ya mafanikio.

Dar es Salaam. Kwa kawaida, kila mtu ana ndoto ambazo angependa kuzitimiza na kuziona zinakuwa halisi na siyo kubaki katika nadharia pekee. Wapo wanaopenda kuwa matajiri kifedha na wapo ambao ndoto zao ni kuwa na amani tu. Kila mtu na maono yake.

Hata hivyo, ndoto hizo hazifikiwi kwa kukaa na kuzisubiri zitimie kwani zitahitaji jitihada, nguvu na subira ili kuzitimiza. 

Hata hivyo, katika njia kuelekea kutimilika kwa ndoto, wengine wamejikuta wakikata tamaa mapema na kuishia njiani huku wengine wakifikiri kuwa uwezo wa kiuchumi, umri na “connection” ndiyo sababu ya ukomo wa ndoto zao.

Kabla haujakata kuzifikia tamaa ndoto zako, huenda dondoo hizi zikakufariji na kukupa nguvu mpya:

Mafanikio huja mdogo mdogo

Hakuna mtu yeyote ambaye aliyajenga mafanikio yake ndani ya siku moja. Kwa watu wote ambao unawatazama na kuwataja kama watu waliofanikiwa kimaisha ipo historia nyuma yao ambayo ni hatua ya kufikia hapo.

Nyuma ya waliofanikiwa ni kukosea, kudharauliwa na watu waliowazunguka na kukosolewa kwa mawazo yao lakini huenda kati ya mambo yaliyowafanikisha ni kuwa na matumaini juu ya jambo walilokuwa wakilifanya.

Mathalani tovuti ya www.uky.edu inaeleza kuwa, ilimchukua Thomas Edison kufeli mara 1,000 kabla hajafanikiwa kutengeneza balbu ya umeme. Nyuma ya mafanikio hayo, ni dhihaka kutoka kwa ndugu, walimu wake na hata waajiri wake wa awali.

Usitake kuanza na kikubwa, anza mdogo mdogo na hata ukifanikiwa, itakuwa rahisi kwako kurejea yote uliyopitia pale utakapokutana na changamoto. Picha| freepik.com

Muda, Umri, fedha visikuzuie kufikia malengo yako

Huenda “sina fedha” ikawa ni jibu ambalo utapata kutoka kwa vijana wengi ambao utawauliza kwanini hawajaamua kufuata malengo yao. Baadhi yao husubiri hadi wapate kifurushi kikubwa cha fedha ili waweze kuanza kuzitafuta ndoto zao.

Mathalan, wapo watu ambao huenda ukitafuta taarifa zao miaka 10 iliyopita, unaweza usizipate lakini kwa sasa wanafahamika na haimaanishi kuwa walikuwa hawafanyi chochote katika kipindi hicho.

Msanii Zuhura Soud (Zuchu), alisainiwa na lebo ya muziki ya Wasafi iliyo chini ya msanii Diamond Platnumz Aprili 8, 2020, hapo ndipo watu walianza kumfahamu msanii huyo na hadi sasa huenda ni kati ya wasanii wa kike ambao kazi zao zinasikilizwa zaidi.

Usilolijua ni kwamba, hata wakati akisubiri kwa takriban miaka minne kusainiwa katika lebo hiyo, Zuchu alikuwa akiendelea na mazoezi, akijifua na akirekodi baadhi ya kazi zake alizokuwa akizituma kipitia mitandao ya kijamii.


Soma zaidi


Nguvu ya uthubutu, utofauti

Siyo mbaya kuiga pale jambo linapoonekana kuwa zuri lakini kwanini uige kila kitu? Ni kweli umevutiwa na jinsi rafiki yako alivyofungua saluni yake ya wanaume na kuweka wadada wa kuosha nywele lakini wewe ukifungua saluni yako utaongeza nini cha ziada?

Katika kutafuta mafanikio, jaribu kuwa tofauti na hata kama unafanya kitu kile kile, jitahidi kuwa mbunifu na kukifanya kwa utofauti.

Kwa maoni yangu binafsi na ninaomba nisihukumiwe kwa hili, wapo vijana kadhaa walio na vipaji vya muziki ambao wamepotea wakiimba kama wasanii wakubwa wa muziki wa Bongofleva akiwemo Diamond, Harmonize na Alikiba.

Wamepoteza uhalisia wao kwa kutaka kuwa kama mtu mwingine ikiwa ni kwa kutaka mafanikio. Jambo hilo linafanya kutokuwepo ubunifu miongoni mwao.  

Zaidi ni kuwa, katika kila unachofanya usitegemee mteremko kama watu wengi wanavyodhani. Ni rahisi kumkuta mwanafunzi wa chuo kikuu akisema “Nitamaliza chuo, nitapata kazi, nitanunua gari na nitaanza kujenga nyumba yangu” na kumbe maisha hata hayako hivyo kwa wengi wetu.

Usichoke siku yako ipo, kile kizuri unachokiwaza utakipata. Komaa, wekeza zaidi mpaka ufikie kilele cha ndoto zako. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW