Namna akiba inavyoweza kusaidia wafanyabiashara wadogo wadogo
- Akiba ni msingi unaoweza kukuza biashara na kuwa kubwa zaidi.
- Moja ya msingi wa kuweka akiba ni kujiandaa na dharura zinazoweza kutokea kwenye uendeshaji wa biashara yako
Dar es Salaam. Kwenye biashara yoyote kuweka akiba kwa lengo la kuongeza kipato kikubwa zaidi ya kile unachoingiza ni moja ya mafanikio makubwa yanayoweza kukuza biashara kwa asilimia kubwa na hatimaye uchumi kuongezeka
Mchakato huu unaweza kuwa mgumu kwa wafanyabiashara wengi waliozoea kutumia faida wanayoingiza kujikimu na changamoto za maisha badala ya kuitumia kukuza na kuendeleza biashara hiyo.
Neema Makulu mmoja ya wafanyabiashara wa vifaa vya nyumbani katika soko la Kariakoo ameiambia www.nukta.co.tz namna ilivyo ngumu kwa wafanyabiashara wadogo kutumia faida kuweka akiba kwa ajili ya kukuza biashara zao akiwemo yeye kwa lengo la kukuza kipato chake cha baadae.
“Akiba ni msemo unaosemwa sana ila binafsi sijawahi kuutekeleza. Ni kitu cha kuamua na kuanza hakuna ugumu uliopo kwenye hilo.”Amesema Neema.
Inakujengea msingi wa matumizi mazuri ya pesa zako. Picha | Mtandao.
Wakati wafanyabiashara wengi wakiona ugumu katika kutekeleza jambo hilo, bado umuhimu wa kuweka akiba ni mkubwa na wenye manufaa kwa mfanyabiashara kwa ujumla wake.
Kwa mujibu wa Business Daily Africa akiba inakusaidia kupata kipato cha kukuza biashara yako zaidi. Hii ni moja ya manufaa makubwa yanayoweza kusaidia biashara ndogo kukua ni kutumia faida kukuza biashara kutoka hatua moja kwenda nyingine au kutoka chanzo kimoja cha mapato kupata chanzo zaidi ya kimoja kwenye biashara husika.
Inasaidia kuepuka vishawishi vya kupunguza mtaji au faida ya biashara kwa wakati fulani. Ni ukweli usiopingika kwamba kuna wakati kwenye biashara unaweza kupata gharama kubwa zinazoweza kupelekea kutumia pesa nyingi zinazoweza kuathiri faida au mtaji. Kwa kuwa na akiba unayoweka kila baada ya muda fulani, inakusaidia kutatua changamoto hizo bila kuathiri mtaji au faida.
- Mifumo ya kidijitali itakayowavusha wafanyabiashara 2020
- Kwanini wafanyabiashara wanawekeza katika matumizi ya mitandao ya kijamii?
Inakujengea msingi wa matumizi mazuri ya pesa zako, kwa kuwa uwekaji akiba ni mdogo kwa wafanyabiashara na wafanyakazi wengi. Hivyo, mtu kujitengenezea mazingira ya kudunduliza pesa na kuweka akiba inamjenga uwezo kutumia pesa kulingana na matumizi muhimu aliyonayo kwa wakati huo.
Kwa kuzingatia faida hizo, mfanyabiashara ana uwezo mkubwa wa kukua na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili biashara yake wakati wowote.