Binti fanya haya kumsaidia mpenzi wako kutimiza malengo yake

February 29, 2020 7:08 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Unaweza kufanya hivyo kwa kumkumbusha kuweka akiba na hata kwa kumuonyesha vipaji vyake asivyoviona.
  • Kwa kumsaidia yeye, itakupatia amani pale utakapoona amefanikiwa huku ukiwa na mchango kwenye mafanikio yake.
  • Ni kweli unapenda vitu vizuri lakini siyo mbaya ukajinyima kwa muda.

Dar es Salaam. Ni kwanini nimeamua kuandika makala hii? Ni swali nililojihoji hata mimi kabla sijaanza kuandika nilichoandika.

Sababu kubwa ni hii “sasa mwanaume huna pesa mimi nakupeleka wapi?”  kauli hiyo imetoka kwa mwanadada mmoja aliyekuwa akiwasimulia wenzake juu ya hali ya mpenzi wake. 

Hali hiyo ilinipatia mawazo ya mchango wa mwanamke katia kumsaidia mpenzi wake wanapokuwa kwenye mahusiano.

Nimeongea na vijana wengi lakini jibu la Mike Goodwill limenivutia zaidi. Baada ya kumuuliza ni vipi anaweza kumridhisha mpenzi wake kiuchumi, alishika kichwa kana kwamba ameona Israeli anamfuata.

“Acha tu kaka, kuna muda mwingine ninakuwa sina pesa alafu shemeji yako naye anakupigia anashida na pesa. Ukimpa, siku ukiuliza aliitumia kufanya nini utachoka mzee. Kanunua mkoba!,” amesema Mike ambaye yeye na mpenzi wake wamedumu katika mahusiano kwa miaka mitatu sasa.

Kutokana na hali hiyo, haya ni baadhi ya mambo ambayo mwanamke anaweza kuyafanya ili amsaidie mpenzi wake kufikia malengo yake hasa pale anapokuwa hayuko vizuri kiuchumi. 

Muonyeshe uwezo wake

Sio uwezo huo ulioufikiria. Uwezo ninaozungumzia ni ule wa mambo ambayo hafahamu kama ana uwezo wa kuyafanya na yakamletea tija katika maisha.

Mara kadhaa, huenda mpenzi wako kuna jambo analifanya kujifurahisha lakini endapo akilichukulia suala hilo kwa makini, huenda likamtoa kimaisha.

“Mimi Brian anapenda sana kupiga picha. Picha ya simu tu lakini akikupiga, ni lazima watu wengi waisifie waseme ni nzuri.

“Nimemshauri mara nyingi akitumie kipaji chake. Nilitaka nimnunulie hata kamera ya kuanzia lakini baba yule ni mbishi,” amesema Elina ambaye amesema mpenzi wake ameng’ang’ania biashara ya nguo ambayo inamsumbua kila kukicha.

Kama akishindwa jambo fulani ambalo huenda umeona mwelekeo wake ni mzuri, mwambie “mwamba kaza” ili azidi kuitafuta riziki kwa ajili yenu.Picha|Mtandao.

Msaidie kutunza fedha

Ni kweli dada yangu unapenda vitu vizuri na hautaki fasheni yoyote ikupite. Lakini hiyo isiwe sababu ya wewe kumuumiza mpenzi wako kiuchumi na kumfanya akope kama Mike.

Siyo mbaya kama ukapunguza matumizi yako na kumsaidia mpenzi wako kuhifadhi pesa kwani akipata na wewe umepata.

Endapo akiingia kwenye madeni sababu yako kwa sababu zisizo na msingi, hawezi kuwa na amani na huenda hilo siyo jambo ambalo utafurahia.


Inayohusiana: 


Mpe moyo pale anapokata tamaa

Usiwe wa kwanza kumuunga mkono kuwa “hapa baba nilikwambia achana napo” na badala yake, mpatie faraja na mhimize kufanya kazi kwa juhudi zaidi ili afikie malengo yake.

Kama akishindwa jambo fulani ambalo huenda umeona mwelekeo wake ni mzuri, mwambie “mwamba kaza” ili azidi kuitafuta riziki kwa ajili yenu.

Siyo mbaya ukimsaidia pale anapokwama

Ni ngumu kwa wanaume wengi kukubali kuwa wamekwama na hivyo hata kupokea pesa za wapenzi wao inakuwa ngumu zaidi wakihofia kushusha heshima yao.

Lakini, kwa mahusiano ya karne hii, uwazi ndiyo kila kitu endapo unahitaji kulinda mahusiano yako na umpendaye. 

“Mahusiano yangu na mpenzi wangu ni ya uwazi. Sina pesa naweza muomba aniazime na kama yeye pia hana, ananiomba nimuazime. Tunasaidiana kwani maisha ndivyo yaendavyo,” amesema Michael Evans ambaye ni mtengenezaji wa programu za kompyuta.

Enable Notifications OK No thanks