Mateso ya muda mfupi: Msingi thabiti wa mafanikio yako

April 24, 2021 9:26 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Kutoa kafara usingizi na kuamka mapema ni kati ya vitu vya mpito utakavyokutana navyo.
  • Kuwa na uwezo wa kuipa muda biashara yako na kuiwekeza katika kujijenga itakupatia msingi imara.
  • Hata baada ya kufanikiwa, siyo vyema kudharau mawazo ya wengine juu ya unachokifanya.

Dar es Salaam. Nitatoboa lini? Ni kati ya maswali ambayo yanazunguka katika vichwa vya vijana wengi wenye miaka kati ya 23 hadi 35. Baadhi yao swali hilo huja baada ya kufanya juhudi kubwa kutafuta maendeleo na kwa baadhi yao, juhudi hushindwa kufua dafu.

Hilo husababisha msongo wa mawazo miongoni mwa vijana na wengine huingia katika mitego ya kutafuta njia za panya za kuyatafuta maendeleo ikiwemo kuzamia nchi za nje, kushiriki katika biashara haramu na hata wizi.

Katika makala zilizopita, vijana walisema sababu ya kukimbilia mafanikio ni pamoja na kuwa na majukumu katika umri mdogo, msukumo wa makundi rika na kuficha uhalisia yaani “faking it untill they make it” kama inavyosema kwa lugha ya “school bus”.

Hata hivyo, mafanikio yanahitaji silaha tatu endapo haujazaliwa katika familia ya kifalme au ambao utajiri wake siyo wa kusua sua. Silaha hizo ni mapambano ya muda mfupi, uvumilivu na unyenyekevu na maelezo yake ni kama ifuatavyo:

Nitatoboa lini? jibu ni kuwa utatoboa ukiwa mvumilivu, ukichapa kazi na ukiwa mnyenyekevu. Picha| New York Times.

Mapambano ya muda mfupi kwa ajili ya mafanikio ya muda mfupi

Siyo kwamba mapambano huisha katika maisha na kutafuta mafanikio. Hata watumishi wa umma waliostaafu nao huendelea na shughuli mbalimbali zikiwemo ufugaji na biashara.

Ndiyo maana ni ngumu kumuona baba yako ambaye ni mzima wa afya akiwa amekaa nyumbani bila kazi licha ya mafanikio aliyonayo.

Maana ya mapambano ya muda mfupi ni pamoja na siku kadha wa kadha za kuamka mapema, siku za kutoa kafara usingizi wako, siku za kupigwa na jua kali na siku za kupiga pasi ndefu.

Wakati wengine wakitafuta mafanikio ya muda mfupi, unaweza kuchagua kuwekeza muda wako mwingi na juhudi kujijenga kwa kujifunza undani wa kitu unachohitaji kukifanya ili unapoanza kukifanya usiwe mgeni.

Ni hayo mateso ya muda mfupi ambayo yatakuwa mafanikio yako katika siku zijazo. Hakikisha unajua unachokifanya na kuna uhalisia.


Uvumilivu ni silaha isiyoangusha

Baadhi hushindwa kufikia malengo yao siyo kwa kuwa hayawezekani, bali kwa kuwa wameyakatia tamaa mapema.

Hiyo huletwa na tabia ya kutaka kujaribu kila kitu. Utakuta mtu ni mchoraji wa miaka miwili, mhasibu wa mwaka mmoja, wakala wa viwanja kwa miezi sita na orodha inaendelea. Katika hatua hiyo, unaweza kujiuliza, hata mwajiri wako anapata wapi nguvu ya kukupandisha cheo au biashara yako inawezaje kufahamika?

Ni muhimu kuvumilia mwanzo wa kazi zako ili uyaone mafanikio kadri muda unavyoenda. Hata hivyo, ni muhimu pia kusoma dira ya biashara au kazi yako ili kujua muelekeo wake kama kuna dalili za kufanikiwa kwani wakati mwingine “Kusepa” ndio maamuzi mazuri unayoweza kufanya.


Soma zaidi:


Unyenyekevu ni funguo ya watu kuwa na imani na wewe

Kuna neno nimelisikia hivi karibuni kutoka kwa Mama Samia, alisema “kupandisha mabega”  ambayo ni sawa na kujiona kuwa umefika katika hicho unachokifanya, kutokutaka kusikiliza maelekezo ya watu wengine wakiwemo wakubwa zako kikazi na hata unaowasimamia. Kwa kifupi ni kiburi.

Katika shughuli unazozifanya, ni muhimu kutambua kuwa wazo la kila mtu lina maana kwani kila mtu ana uwezo wa kung’amua mambo kutoka katika mtazamo tofauti. Wakati wewe una uhakika na jambo fulani, wapo ambao walishawahi kuwa katika hali hiyo na haikufanikiwa.

Licha ya kuwa inashauriwa kutokusikiliza maneno ya watu lakini kwa ngazi ya taaluma na kazi, maneno  mengine ni muhimu kusikiliza. Hivyo pale unapopewa ushauri, usiuchukulie poa, pata muda fikiria, sikiliza maoni ya watu wengine na kisha fanya maamuzi.

Mbali na hayo yote, wakati ukiwa katika safari ya kutafuta mafanikio, ni muhimu kutafuta watu ambao wanaweza kukusahuri na kukukosoa bila kukuogopa ili usiwe kama mwenda safari asiyejua anapoelekea.

Bila shaka kazi unayoifanya, wapo waliowahi kuifanya hata kama kwa utofauti lakini walishawahi kuipitia hivyo wanaweza kukupa mawazo. Katika yote, usikose muda wa kuwajulia hali uwapendao wakiwemo wazazi, ndugu na kutengeneza marafiki kwani kuna uhai gani kusherekea mafanikio yako peke yako?

Hadi wiki ijayo, wako katika Utanzania, Rodgers George.

Enable Notifications OK No thanks