Ifahamu mikoa 3 yenye watoto wengi waliodumaa Tanzania

February 7, 2023 2:28 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Mikoa hiyo ni Iringa, Njombe na Rukwa.
  • Waziri Ummy ataka uchunguzi zaidi kubaini chanzo cha tatizo hilo.

Dar es Salaam. Udumavu! Si jina geni, ni jambo linaloacha huzuni kwenye familia na jamii.

Kuanzia athari za kimaumbile, kiafya na kisaikolojia janga hilo limeendelea kuitesa Tanzania husani kwenye mikoa mitatu ambayo imetajwa kwenye ripoti ya Viashiria Muhimu vya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto (THDS-MIS) ya mwaka 2022,kuongoza kwa idadi ya watoto wenye udumavu.

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu aliyekuwa akizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo uliofanyika kwenye  Ofisi za Mtakwimu Mkuu wa Serikali Jijini Dodoma  leo Februari 7, 2023 ameitaja mikoa hiyo inayoongoza kuwa ni Iringa, Njombe na Rukwa.

“Mkoa wa Iringa una udumavu kwa asilimia  56.9,  Njombe asilimia 50.4 na mkoa wa Rukwa 49.8,” amesema Waziri Ummy.

Udumavu huo unawahusu watoto walio wa chini ya umri wa miaka mitano. 

Si mara ya kwanza kwa mikoa hiyo kutajwa kwenye Orodha ya mikoa inayoongoza kwa udumavu wa watoto, jambo linaloibua maswali mengi yasiyo na majibu izingatiwa kuwa mikoa hiyo inaongoza kwa uzalishaji wa chakula.


Soma zaidi


Kwa mujibu wa takwimu za Taarifa ya Hali ya Chakula Nchini kwa mwaka 2020/2021, inayotolewa na Wizara ya Kilimo, Iringa, Njombe  na Rukwa imeorodheshwa miongoni mwa mikoa yenye uzalishaji wa kutosheleza wa mazao ya chakula nchini. 

Mathalani mkoa wa Iringa ulizalisha tani 228 za mazao  ya nafaka huku ikiwa na utoshelevu wa mahitaji ya chakula kwenye mkoa huo kwa asilimia 139.

Kwa mujibu Waziri Ummy aliyekuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo amesema kuna haja ya kufanya uchunguzi kubaini chanzo cha idadi ya watoto wenye udumavu kung’ang’ania kileleni kwenye mikoa hiyo.

“Mikoa inayoongoza kwa udumavu mkali bahati mbaya imebaki kuwa ile ile ambayo ndiyo wazalishaji wakuu wa chakula, lazima tuchunguze tujue kuna nini,” amesema Ummy.

 Udumavu kwa jicho la kitaifa

Ripoti hiyo iliyozinduliwa leo imebainisha kupungua kwa idadi ya watoto wenye udumavu nchini kwa asilimia 4.

“Tumeshusha idadi ya watoto wenye udumavu kutoka asimia 34 kwenye utafiti wa mwaka 2014 mpaka asilimia 30 mwaka 2022,” amesema Waziri Ummy.

Kwa mujibu wa Waziri huyo asilimia hizo za watoto wenye udumavu ni sawa na watoto milioni 2.8 kati ya watoto  wenye umri chini ya miaka mitano milioni 9.4 waliopo nchini.

Kufuatia uwepo wa idadi hiyo ya watoto wenye udumavu, Waziri Ummy ameitaka mipango madhubuti kukabili tatizo hilo linaloendelea kuathiri watoto chini ya umri wa miaka mitano nchini.

Enable Notifications OK No thanks