Umemejua unavyowaokoa wafugaji na ukame Dodoma
- Unasaidia upatikanaji wa umeme kwenye birika la maji kwa saa 24.
- Wafugaji waelezea namna walivyoepuka migogoro, kutembea umbali mrefu.
- Kila mfugaji huchajiwa Sh70 kwa kila ng’ombe.
Dodoma. Umbali wa mita 700 hivi kutoka ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Leganga, kilichopo Kongwa mkoani Dodoma, kwenye birika la kunyweshea mifugo maji, kundi kubwa la mifugo linaingia hapa kunywa maji.
Katika birika hilo linaloendeshwa kwa kutumia nishati ya umeme, sehemu kubwa ya wanyama waliopo kwenye foleni ya kunywa maji hayo ni ng’ombe, mbuzi, na kondoo.
Umeme unaotumika kuendesha mtambo wa kujaza birika ni ule uliosambazwa na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) pamoja na nishati ya umeme jua iliyowekwa na Shirika lisilo la kiserikali la Elico Foundation, inayojihusisha na usambazaji wa miradi ya nishati jadidifu hususani maeneo ya vijijini.
Mifugo ikinywa maji katika birika linaloendeshwa na umeme kijiji cha Leganga, wilayani Kongwa. Picha l Esau Ng’umbi
Kutokana na umeme wa Rea kukatika mara kwa mara, mtambo wa umeme jua hutumika kama mbadala wa kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa saa 24 ili wafugaji wapate maji ya kunyweshea mifugo yao.
Uwepo wa birika hilo ni neema kwa wafugaji ambao ni nusu ya wakazi wa kijiji hicho kutokana na uhakika wa upatikanaji wa maji jambo linalosaidia mifugo yao kuzaliana kwa wingi na kunawiri.
Awali, maisha kwa wafugaji yalikuwa tofauti hapa. Wafugaji wote walilazimika kutembea zaidi ya saa moja kwenda kufuata maji katika rambo lililopo kijiji cha jirani cha Chitego ambako pamoja na kuwa maji yake hayakuwa salama kwa mifugo, mara kadhaa walijikuta katika migogoro ya wao kwa wao kutokana na wingi wa mifugo na uhaba wa maji.Kiputwaa Kanayaa, mfugaji wa Kijiji cha Leganga ameiambia Nukta Habari kuwa uwepo wa birika hilo kijijini kwao umepunguza muda waliokuwa wanatumia kunywesha mifugo.
“Tulipokuwa tunanywesha Chitego tulikuwa tunatumia muda mrefu sana, unaweza kupeleka ng’ombe saa 11 jioni ukapata maji saa mbili usiku, hapa tunapata raha kwa sababu haizidi saa moja, ng’ombe wako wanakuwa wameshakunywa maji,” amesema Kanayaa mwenye ng’ombe zaidi ya 150.
Kutokana na maji waliyokuwa wananywesha mifugo yao awali kuwa makali, Ngole Mgasha anasema kuwa mifugo yao ilikuwa inadhoofika kiafya kwa kukohoa mara kwa mara na kukonda jambo lililokuwa likiathiri hata bei ya mifugo wakati wa mnada.
“Hapa ni jirani, na maji ni masafi, hata ndama wanaweza kufika, afya za ng’ombe zimeimarika hata wakati wa mnada tunauza bei nzuri,” anasema Mgasha.
Mwenyekiti wa kijiji cha Leganga, Anderson Chiligo anasema kuwa birika hilo linanywesha zaidi ya ng’ombe 5,000 pamoja na mbuzi 7,000 kila siku kutoka kwa wafugaji wa jamii mbalimbali ikiwemo Wamasai, Wagogo na Wambulu.
Mifugo ni miongoni mwa sekta nyeti nchini Tanzania inayochangia usalama wa chakula kwa kiasi kikubwa, inachangia fedha za kigeni na ukuaji wa pato la Taifa.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ukuaji wa sekta ya mifugo kwa mwaka 2021 ulifikia asilimia 5.0 na kuchangia asilimia 7.0 kwenye pato la Taifa, jambo linaloonyesha umuhimu wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi nchini.
Maji sio bure
Pamoja na kwamba huduma ya maji inapatikana kwa saa 24 katika eneo hilo, huduma hiyo haitolewi bure. Wafugaji wanatakiwa kulipia Sh70 kwa kila ng’ombe mkubwa, ikiwa ni ahueni kidogo kutoka Sh100 kwa ng’ombe mmoja kunywa maji katika maeneo mengine nje ya kijiji chao.
“Kuanzia zamani tulikuwa tunalipia, tulianza na Sh30 na sasa tupo 70, sehemu nyingine wananywesha hadi Sh100 kwa ng’ombe mmoja kwa hiyo hapa ni nafuu,” anasema Kanayaa aliyekuwa ananywesha mifugo yake maji.
Umeme jua chanzo cha faraja
Upatikanaji wa uhakika wa maji kwenye birika hilo haukuja hivi hivi, kwa mujibu wa wafugaji wa Leganga, hali hiyo imechangiwa zaidi na uwepo wa mitambo ya umemejua inayosaidia uwepo wa nishati ya umeme muda wote kwa kuwa umeme uliowekwa awali na Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) umekuwa ukikatika mara kwa mara.
Denis Kasili ambaye ni msimamizi wa birika hilo anasema kukatika mara kwa mara kwa umeme wa Rea kijijini hapo ni miongoni mwa sababu zilizowafanya Elico Foundation kufunga mtambo wa umemejua ili kuwanusuru wafugaji na adha ya upatikanaji wa maji.
“Umeme wa Rea ulikuwa unakata sana, ndipo mwaka jana wakaja Elico kufunga mitambo ya umeme jua, toka wafunge hatujawahi kuwa na shida ya maji, umeme unapatikana muda wote, ukikatika wa Rea nawasha wa umeme jua,” anasema Kasili.
Baadhi ya maeneo nchini yamekuwa yakikabiliwa na ukosefu wa maji ya uhakika ambao miaka ya hivi karibuni umechagizwa na ukame na kuathiri ufanisi katika ufugaji.
Mwaka 2021 baadhi wafugaji walipoteza mifugo yao baada ya ukame kuathiri baadhi ya mikoa nchini ikiwemo Arusha, Simiyu na Manyara kutokana na kukosekana kwa malisho na maji.
Jambo hilo liliichochea Serikali kutenga Sh130 bilioni kwa ajili ya kuchimba visima, kukarabati na kujenga mabwawa katika maeneo yaliyoathirika zaidi.
Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kati ya mwezi Januari hadi Septemba 2021, jumla ya ng’ombe 1874 zilikufa kutokana na ukame Wilaya Kiteto pekee yake.
Mifugo ikiwa kwenye foleni ya kunywa maji kwenye birika linaloendeshwa na umeme jua pamoja na umeme wa Rea kijiji cha Leganga, Kongwa. Picha l Esau Ng’umbi
Luku bado changamoto
Licha ya huduma hiyo ya maji, wafugaji wa kijiji hicho wamebainisha kukutana na changamoto ya tokeni za umeme kuchukua muda mrefu pale unapoisha, jambo ambalo mwenyekiti wa kijiji hicho amekiri kuwa lipo na tayari ameshawasiliana na wahusika kulishughulikia.
Msimamizi wa miradi ya Elico Foundation Elikana Sehaba anasema wanakusudia kubadili mfumo wa ununuzi wa tokeni ili kuwaondolea usumbufu wa kusubiri muda mrefu watumiaji wake.
Kuhakikisha maeneo mengi yanapata huduma kama hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Elico Foundation, Sisty Basil anasema taasisi yake kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutatua changamoto za jamii kwa kutumia fursa zitokanazo na nishati endelevu.
“Kwa sasa tunatekeleza mradi mwingine wa uwezeshaji kiuchumi awamu ya pili, tunawagawia wananchi vifaa kama majokofu, mashine za kuunga vyuma pamoja na mashine za kujaza upepo halafu wao wanarejesha kidogo kidogo,” anasema Basil.