Fursa za uwekezaji zilizojificha sekta za kilimo, viwanda Tanzania
- Fursa hizo ni pamoja na uzalishaji wa mafuta, uongezaji thamani wa mazao yanayozalishwa nchini na ujenzi wa viwanda.
- Ili uwekezaji huo ufanikiwe, changamoto za mitaji, ardhi na teknolojia zinapaswa kutatuliwa.
- Serikali yasema itaendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Dar es Salaam. Kwa mkazi wa Kinyerezi mkoani Dar es Salaam Evelyn Oscar uwekezaji ni kuongeza uzalishaji katika kitu ambacho mtu anafanya hasa kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia ili kurahisisha shughuli za uzalishaji na kuongeza kiasi cha bidhaa zinazozalishwa.
“Ukitumia teknolojia, inamaanisha utazalisha kwa urahisi, na kwa wingi zaidi na hivyo kukuwezesha kuwa na soko kubwa unaloweza kulihudumia na kulilidhisha. Mimi natarajia keki zangu niziuze hata kimataifa kama wafanyabiashara wengine wakubwa,” amesema Oscar ambaye anaanza kufanya uwekezaji wake mdogo kwa kupika keki nyumbani.
Maendeleo ya nchi nyingi kiuchumi yanaendana na hali ya uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za afya, biashara, viwanda na miundombinu na namna wanachi wake kama Oscar wanavyochangamkia fursa katika kujikwamua kiuchumi na kuutokomeza umaskini.
“Natamani nione keki zangu madukani, mashereheni na hata kama sehemu ya chai kwa familia,” amesema mpishi huyo ambaye mchango wake katika sekta ya kilimo na ufugaji hususan zao la ngano, siagi, na sukari unatarajia kuongezeka siku hadi siku.
Oscar huenda ni miongoni mwa Watanzania wachache ambao mtazamo wao juu ya uwekezaji unajumuisha sura pana ukiwemo mchango wao badala ya kuona ni masuala ya watu wenye mabilioni pekee.
Hata hivyo, wadau wa uwekezaji wanaeleza kuwa mtu yeyote anaweza kuwekeza ilimradi ana mtaji na uelewa na kitu anachohitaji kuwekeza.
Mwanzilishi wa Taasisi ya Accountable Africa, Thierry Dongala, ambao ni waandaaji wa kongamano la wawekezaji Tanzania amesema uwekezaji unaweza kuanza na watu ndani ya nchi na kuwahusisha wale walio nje ya nchi.
“Tumeanzisha jukwaa hili ili kuona uwekezaji nchini Tanzania unakua. Ni sehemu ya kuhakikisha kuwa Afrika inakua katika sekta ya viwanda na kuitendea haki sekta ya kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa Waafrika wengi,” anaeleza Dongala.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uwekezaj Profesa Kitila Mkumbo (kushoto) amewasisitiza Watanzania waliopo ughaibuni ambao wana mitaji ya kuwekeza waje kuwekeza nchini kwao. Picha| Rodgers George
Kuna fursa zipi za uwekezaji nchini Tanzania?
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uwekezaj Profesa Kitila Mkumbo ametaja baadhi ya sehemu za uwekezaji ambazo mtu yeyote anaweza kufikiria kuzitazama na akatarajia faida kwa uhakika kutokana na uhitaji wa bidhaa mbalimbali kutoka katika sekta hizo.
Profesa Mkumbo aliliambia kongamano la Wawekezaji mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa miongoni mwa sekta zenye uhakika wa masoko nchini ni sekta za kilimo, mifugo pamoja na viwanda.
Prof Mkumbo anasema hadi sasa Tanzania ina uzalishaji mdogo wa mazao mbalimbali ambayo yanahitajika nchini ikiwemo mafuta ya kupikia ambapo nchi inalazimika kuingiza hadi asilimia 40 ya mafuta yanayohitajika.
Kiongozi huo anaeleza kuwa viwanda vya mafuta ya kupikia vilivyopo Tanzania vinazalisha mafuta kwa kiwango cha chini ya asilimia 30 hadi 40.
“Kuna viashiria vitano vinavyoifanya Tanzania kuwa nchi bora kwa kuwekeza. Hali ya kisiasa inayotabirika, uchumi unaokua kwa kasi, sheria zinazotekelezeka, uwepo wa vijana wengi walio na ujuzi pamoja na soko,” anasema waziri huyo na kuongeza,
“Kwa zaidi ya miaka 10 uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa wastani wa asilimia wa sita hadi saba mtawaliwa hata katika vipindi vigumu. Hata mfumuko wa bei umebaki katika kiwango kinachokubalika na wawekezaji,” amesema Prof Mkumbo.
Miongoni mwa viashiria ambavyo huchochea uwekezaji kutoka kwa wawekezaji wa ndani na nje ni ukuaji imara wa uchumi, mfumuko wa bei usioumiza, sheria na kanuni rafiki za kustawisha biashara zikiwemo taratibu na viwango rafiki vya kikodi visivyoangamiza mitaji ya wawekezaji.
TANGAZO
Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dk Akinwumi Adesina ameeleza kuwa Tanzania imebaki kuwa miongoni mwa nchi chache ambazo uchumi wake umeendelea kukua licha ya uwepo wa janga la Corona duniani na kwamba iwapo kuna mtu anataka kuwekeza basi Tanzania ni mahali sahihi.
AfDB inatarajia kuwa uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 6.6 mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 6.4 mwaka 2020.
Makisio hayo ya AfDB yapo ndani ya wigo wa matarajio ya ukuaji wa uchumi yalitolewa mwishoni mwa Januari na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Mkurugenzi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Japhet Justine anasema Watanzania wanahitaji kuzichangamkia fursa zilizopo katika kilimo kwa kuwa wapo wadau wa kuwasaidia kifedha na hata kimawazo.
Japhet anasema wapo watu wengi wanaoibuka na mawazo mazuri tu ya kuendeleza sekta ya kilimo lakini wanapohitajika kuyatolea ufafanuzi, wanapotea.
“Uwekezaji katika kilimo ni sanaa, kama hujui sanaa hiyo ni lazima utapotea. Kwa wabunifu wanaohitaji kuwekeza katika sekta ya kilimo, tengenezeni mawazo, yaleteni mezani tuyajiadili, ukiyatetea,wadau wa kukuwezesha wapo,” anasema Justine.
Soma zaidi:
- Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji
- Fursa lukuki kwa vijana kilimo cha “stroberi” Tanzania
- Maeneo matano ya kimkakati kuboresha kilimo 2019-2020
Maeneo mengine ya kuwekeza
Mkurugenzi wa Kukuza uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Anna Lyimo anasema mbali na sekta ya kilimo na mifugo ambazo zinahusisha uongezaji thamani mazao yanayozalishwa nchini yakiwemo kahawa, chai na mkonge, sekta nyingine zinazovutia uwekezaji ni pamoja na sekta ya utalii na uzalishaji wa dawa.
“Katika utalii, kuna uhitaji wa uwekezaji katika hoteli za kitalii, sehemu za mapumziko na viwanja vya michezo mbalimbai ikiwemo mchezo wa golf (gofu). Tutakapotilia mkazo kufanya biashara miongoni mwetu wenyewe (Afrika), kuna uhakika wa kuifanya Afrika kuwa ya viwanda,” anasema Lyimo.
Lymo anasisitiza kuwa katika sekta ya viwanda, kuna fursa za kuongeza thamani za bidhaa zinazozalishwa nchini kwa kuwa miundombinu ya usafirishaji inaendelea kuwekwa sawa ili kuhakikisha uwekezaji wenye tija.
“Kama TIC, ni jukwaa ambalo mwekezaji anaweza kuja na fedha zake nasi tukamshauri pa kuzipeleka na wapi atapata taarifa zote anazohitaji,” anaeleza mtalaamu huyo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Uwekezaj Profesa Kitila Mkumbo (wa pili kutoka kushoto) akiwa na wadau mbalimbali wa uwekezaji waliohudhuria Kongamano la Wawekezaji lililofanyika jijini Dar es Salaam Februari 24, 2021. Picha| B.A.M.
Namna ya kutokomeza changamoto za uwekezaji
Pamoja na kuwepo fursa lukuki za kuwekeza bado baadhi ya wadau wanaona kuna mambo mengi yanayotakiwa kuboreshwa kwa kuwa yanakwamisha jitihada za uwekezaji nchini.
Mkurugenzi wa kampuni ya Phema Agri inayojihusisha na ukusanyaji wa takwimu za wakulima nchini, Daniella Kwayu amesema wakulima wengi ni wale wanaolima katika ardhi ndogo ikiwemo ya hekta moja hadi tano na wanapata changamoto kujiendeleza jambo linalowapa ugumu kupata mikopo na kufikiwa na wawekezaji.
Mdau huyo wa kilimo anasema wawekezaji wengi wanakosa taarifa za uhakika wa masoko na hata wanapohitaji mazao kwa ajili ya kuzalisha bidhaa inakuwa ngumu kukusanya kutoka kwa wakulima.
Mbali na taarifa, baadhi ya wadau wanaeleza kuwa uelewa duni wa masuala ya kilimo miongoni mwa wakulima na ukosefu wa maeneo makubwa ya kilimo ni moja ya mambo yanayorudisha nyuma uwekezaji katika sekta hiyo inayotegemewa na wengi Tanzania.
“Tunatamani kuona tunaweka mtaji wetu na kufanya kazi kwa bidii kwenye ardhi ya Tanzania ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na hasa lile la kujitosheleza kwa mahitaji ya chakula katika kila mkoa kwa mtindo wa uwajibikaji endelevu” ameeleza Mwanzilishi wa Kampuni ya Reap inayojihusisha na masuala ya Kilimo, Peter Schuurs.
Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji ikiwemo kujenga miundombinu ya usafirishaji na kuviwezesha viwanda vya ndani kupata soko la bidhaa.
Latest
