Fursa lukuki kwa vijana kilimo cha “stroberi” Tanzania

Rodgers George 0452Hrs   Februari 24, 2020 Ripoti Maalum
  • Vijana wenye changamoto za ajira watakia kuchangamkia ili kupata kipato. 
  • Wataalamu wa kilimo cha matunda hayo wamesema mahitaji na soko ni la uhakika.
  • Mbali na faida za kiuchumi, stroberi zina manufaa mengi kiafya.

Dar es Salaam. “Nyumbani wana shamba ambalo hawalitumii. Niliomba nianze kufanya heka heka zangu kwani nilikua nimechoka kukaa nyumbani bila kusahau uchovu wa kuzunguka maofisini kutafuta kazi pasipo mafanikio,” anaeleza Tekla Buyamba ambaye ameamua kuingia katika kilimo cha matunda ya stroberi kukabiliana na tatizo la kukosa ajira. 

Tekla anasema amejiajiri katika kilimo cha zao hilo la fukasidi (strawberry) ili kujipatia kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yake.

Fukasidi hustawi katika maeneo yenye joto la wastani, na hukua kwa haraka zaidi na uzalishaji kuongezeka linapolimwa kisasa zaidi ambapo hulimwa katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Iringa, Arusha, Kilimanjaro na kwa sehemu mkoani Pwani.

Matunda ya stroberi  yana matumizi mbalimbali kulingana na uhitaji wa mtumiaji, jamii na maeneo ikiwemo kuliwa kama tunda, ladha katika aina mbalimbali za vyakula, kuweka rangi, harufu na nakshi katika vipodozi na kutengeneza marashi. 

Wakati vijana wengi wakilalamika  juu ya ukosefu wa ajira, Tekla alitumia vizuri mtandao wake wa kijamii wa Instagram kupata maarifa na kuchukua hatua za kuanza kilimo hicho. 

Safari yake ambayo ilianza mwaka 2019 haikuwa rahisi kwani ilianza na mtaji wa Sh150,000 ambao aliupata baada ya kuuza simu yake na kuwekeza katika shamba dogo la matunda ya stroberi Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro.

Binti huyo mwenye stahada ya usimamizi wa ofisi ana matumaini makubwa ya kuvuna matunda hayo Aprili mwaka huu aliyolima Disemba ya mwaka 2019, anasema fedha atakazopata zitamsaidia kubadilisha maisha yake na kuongeza uzalishaji katika zao hilo. 

Hiyo siyo fursa kwa Tekla (27) peke yake, bali kwa vijana ambao bado wanasaka fursa za kujiajiri na kuajiriwa kuingia katika kilimo hicho ambacho kinaweza kulimwa hata katika eneo dogo lakini kikatoa mazao mengi. 

“Huwezi kukosa soko. Hakuna mtu anayejihusisha na “strawberries” ambaye nimekutana naye akisema kakosa soko,” Picha| Tanzania na Kilimo. 

Fursa zilizopo kwenye kilimo cha stroberi

Kutokana na umuhimu wa matunda hayo hasa kwa afya za watu, mahitaji yake yanaongezeka kila mwaka jambo linaloweza kuwafungulia fursa vijana wasio na ajira kuwekeza nguvu zao kulima zao hilo. 

Kwa mujibu wa tovuti ya Trige, tani milioni 9.2 za zao la stroberi zilivunwa mwaka 2017 na soko la zao hilo limeendelea kupanda kila mwaka ambapo hadi kufikia September 20, 2019, kilo moja ya matunda hayo iliuzwa kwa Sh8,135 kwa kilo moja katika soko la dunia.

China ndiyo inaongoza kwa uzalishaji wa zao hilo baada ya kuzalisha tani milioni 3.7 mwaka 2017 ikifuatiwa na Marekani iliyozalisha tani milioni 1.4. 

Trige imeainisha kuwa uzalishaji wa zao hilo umekuwa ukipanda mfululizo kwa miaka mitano iliyopita.

Mtaalamu na mshauri wa masuala ya kilimo, Daudi Mwakalinga ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa, matunda hayo kwa sasa soko lake ni la uhakika kwani uhitaji wake ni mkubwa Tanzania na nchi za nje. 

“Huwezi kukosa soko. Hakuna mtu anayejihusisha na “strawberries” ambaye nimekutana naye akisema kakosa soko,” amesisitiza Mwakalinga na kubainisha kuwa wazalishaji bado ni wachache hivyo ni fursa ya kuchangamkiwa na vijana. 

“Miaka miwili iliyopita, matunda haya kwa nusu kilo yaliuzwa kwa Sh3,000 lakini sasa hivi nusu kilo ni kwa Sh5,000 hadi Sh6,000. Soko lipo,” amesema Mwakalinga. 

Kwa vijana ambao huenda hawapo katika maeneo ambayo wanaweza kulima zao hilo, bado wana fursa za kutengeneza sharubati (Juisi) au kutengeneza unga wa matunda hayo na kuwauzia wateja wao.

Siyo hayo tu, matunda haya pia yanatumika kutengeneza “ice cream” na pia hutumika kama chakula cha kusindikiza mlo kamili yaani “desert”.


Zinazohusiana


Mazingira ya ustawi wake

Mtaalam wa kilimo kutoka kampuni ya Holly Green Agric Group ltd, Lydia Gerald anaeleza kuwa stroberi inaweza kustawi vizuri kwenye udongo tifutifu wenye rutuba. 

Zao hili haliwezi kustahimili ukuaji kwenye udongo wenye chachu nyingi, hasa chokaa kwani mizizi yake huoza kwa urahisi.

Ili kuwa na mazao bora ambayo yatakuwezesha kupata soko la uhakika, Gerald anashauri kuzalisha kwenye nyumba maalumu ya kuzalishia mazao (green house). 

Mimea ya stroberi inahitaji maji mengi ili istawi vizuri, kama italimwa katika shamba la kawaida mkulima anatakiwa kuhakikisha anakuwa na mfumo mzuri wa umwagiliaji kabla ya kuanza kilimo cha zao hilo.

Mkulima wa matunda hayo wa mkoa wa Morogoro, Peter Msemo (@mr_berries) anabainisha ili matunda hayo yavunwe yanahitaji miezi minne ya kulima kabla ya mavuno.

Msemo ambaye ni mwalimu wa kilimo cha matunda ya stroberi anasema kwa mtu atakayeanza na miche 100 kama alivyofanya Buyamba, anatakiwa kutarajia hadi Sh 90,000 kwa wiki akianza kuvuna.

Msemo anasema miche 100 ndiyo kima kidogo kwa mtu anayehitaji kufanya kilimo biashara cha matunda hayo na miche hiyo huzaliana na kutoa miche mingine hivyo mkulima haja ya kununua mche tena.

Endapo ukiuhudumia mche mmoja vizuri, kila wiki unakupa matunda 7 mpaka 35 kutegemeana na hali ya hewa ikiwemo jua na huduma unayoipatia miche yako kitalaamu.

“Miche 100 ikakupa matunda 7 kwa kila mche mmoja (7x100) sawa sawa na matunda 700 kwa wiki moja,” anasema Msemo

Safari hiyo huenda hadi kwa miaka mitatu ambapo ndio maisha ya mche mmoja wa matunda hayo endapo utapata matunzo mazuri kila mwaka.

Siyo hayo tu, matunda haya pia yanatumika kutengeneza “ice cream” na pia hutumika kama chakula cha kusindikiza mlo kamili yaani “desert”. Picha|Mtandao.

Changamoto zake

Hata hivyo, siyo rahisi kufanikiwa katika kilimo hiki kama hujawekeza vya kutosha katika mbegu, madawa na teknolojia ya kisasa. 

Msemo anasema kilimo hiki kina changamoto kama kilimo kingine hasa endapo hautofuata masharti ya ulimaji wa matunda hayo.

Kwa kawaida, matunda haya huhitaji kumwagiliwa kwa njia ya matone, jambo linalohitaji kujua ni kiasi gani cha maji kinaenda kwa kila mche. 

kumwagilia kupita kiasi, unaweza kusababisha hali ya unyevu shambani mwako na kuishia kukabiliana na magonjwa ya fangasi.

“Wakulima wengi wanafanya makosa ya kuweka samadi au kuendelea kumwagilia shamba tena bila kutumia njia sahihi ya drip irrigation (matone). Katika kipindi cha mvua zinazonyesha bila kujua, samadi inapopata unyevu wa maji inavutia uzalianaji wa fangasi. 

“La kuzingatia ni udongo tifutifu tu na maji kwa wingi yasiyo ya chumvi wala magadi ili kuilinda mizizi isijeoza,” amesema  Msemo.

Ikiwa mkulima anazalisha stroberi kwenye eneo la wazi, stroberi inaweza kushambuliwa na magonjwa ya ukungu, pamoja na magonjwa yanayosababishwa na virusi mbalimbali ikiwemo vya mnyauko fusari. 

Katika makala ijayo tutaangazia kwa kina safari ya mafanikio ya Mr Berries kwenye kilimo cha stroberi kilivyobadilisha maisha yake.

Related Post