BoT: Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 6 mwaka 2021
- Kamati ya Sera ya Fedha ya Bodi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yasema uchumi utaimarika zaidi mwaka huu.
- Hiyo ni kutokana na mwenendo wa kuridhisha wa hivi karibuni wa sekta muhimu za uchumi.
- Benki zatakiwa kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kuchochea uzalishaji na biashara.
Dar es Salaam. Kamati ya Sera ya Fedha ya Bodi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema uchumi wa Tanzania unatarajiwa kuimarika zaidi mwaka 2021 na kufikia kiwango cha ukuaji cha asilimia sita au zaidi kutokana na mwenendo wa kuridhisha wa hivi karibuni wa sekta muhimu za uchumi ikiwemo ujenzi na kilimo.
“Kamati ya Fedha imeridhia kwamba matarajio ya ukuaji wa uchumi kwa asilimia 5.5 kwa mwaka 2020 yatafikiwa. katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka jana, uchumi ulikua kwa asilimia 4.9,” inaeleza taarifa ya BoT kuhusu kikao cha kamati hiyo iliyotolewa mapema asubuhi leo.
Imesema mwenendo wa uchumi wa Tanzania umekuwa wa kuridhisha, licha ya changamoto za athari za ugonjwa wa COVID-19 kwenye uchumi wa dunia.
Viasharia vitakavyosaidia kuimarika kwa uchumi mwaka huu ni pamoja na mfumuko wa bei kuwa mdogo na tulivu, kupungua kwa riba za muda mfupi kwenye mikopo inayotolewa na benki na kuimarika kwa sekta ya nje kutokana na mauzo ya nje ya nchi.
Zinazohusiana:
- BOT: Marufuku kurusha hovyo noti
- BOT yashusha tena riba kwa benki za biashara Tanzania
- BoT yaaeleza sababu za kutumia jeshi kukagua maduka ya kubadilishia fedha Arusha
Taarifa hiyo pia imeeleza kuwa akiba ya fedha za kigeni imeendelea kutosheleza uwezo kugharamia huduma na bidhaa kutoka nje kwa zaidi ya miezi 5.6.
“Mwenendo wa utekelezaji wa bajeti ya Serikali unaendelea vizuri kutokana na kuimarika kwa mapato yatokanayo na kodi,” imeeleza taarifa hiyo inayopatikana katika tovuti ya BoT.
Aidha, kamati hiyo imeitaka BoT kuendelea kushirikisha mabenki na wadau wengine kuongeza mikopo kwa sekta binafsi kwa riba nafuu ili kuchagiza shughuli za uzalishaji na biashara.
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ilikadiria kuwa uchumi wa Tanzani utakua kwa asilimia 6.6 mwaka huu, huku Benki ya Dunia ikikadiriwa kuwa utakua kwa asilimia 5.5 kutoka asilimia 2.5 ya mwaka jana.
Latest