Filamu ya ‘Red Notice’: Kikulacho ki nguoni mwako
- Ni filamu inayohusu urafiki wa kuzungukana.
- Huku wizi na usaliti vikiwa ni sehemu ya maisha.
Dar es salaam. Siku zote binadamu tunapenda kuwaamini na kuwashirikisha watu wetu wa karibu mambo yetu mbalimbali ya kimaisha, ikiwemo hata siri zetu, kwa vile tu tunaamini wao ndiyo watu sahihi zaidi kuzijua.
Bahati mbaya, wao ndiyo wamekuwa wanatuumiza. Tena kwa kutumia siri zetu ambazo wanazifahamu.
Wahenga waliliona hilo. Walitukanya kwamba “kikulacho kinguoni mwako”, ikimaanisha kuwa adui wa maisha yako siku zote hatoki mbali.
Filamu ya “Red Notice”, ipo kutukumbusha kuwa makini na wale wageni wanaogonga kwenye milango ya mioyo yetu na kutufanya tuone kuwa dhamira zao juu yetu ni za dhati.
Filamu hii inaanza na John Hartley, polisi wa FBI ambaye kibarua chake kinakaribia kuota nyasi.
Hatley yupo katika mawindo ya kumsaka mwizi anayejiita mwizi mkuu wa vitu vya sanaa duniani.
Kumshinda Bishop, Booth na Hatley inabidi washirikiane lakini ushirikiano huo hauna mwisho mwema kwa mmoja wao. Picha| Los Angeles Times.
Ninamzungumzia Nolan Booth ambaye yupo katika “mission” ya kukusanya mayai matatu yanayoaminika kuwahi kutolewa kama zawadi kwa Malkia Cleopatra kutoka kwa mpenzi wake Anthony. Anaanza kukusanya yai lililopo katika maonesho ya moja ya makumbusho jijini Rome, Italia.
Mara paap! Kufika na kufika, Hartley anagundua ya kuwa yai limeibiwa tayari.
“Fungeni milango yote. Hakuna mtu kutoka nje” anapayuka Hatley lakini wapi!!, Booth tayari yupo mbio mbio.
Tabasamu kwa Hatley ni baada ya kumkamata Booth na kurejesha yai mikononi mwa polisi. Hata hivyo, Polisi hawaoni mikono salama zaidi ya kubaki na yai hilo.
Meza zinageuka pale kunakucha na yai alilokabidhi Hatley linagundulika kuwa ni feki. Nani akamatwe, Jibu unalo!
Hatley anatiwa hatiani na kufungwa gerezani kwa kuhusika na wizi wa yai na huko anakutana na Booth tena kwenye chumba kimoja.
soma zaidi
- Kisasi kinavyogeuka kuwa safari ya penzi jipya
- Utafanya nini elimu inapokutengenisha na mpenzi wako?
- Coming to America: Filamu maalum kwa watu wasiotaka kuvunja viapo
Mwanzo wa urafiki mpya
Wakiwa gerezani, wawili hao wanaitwa na kamanda lakini looo! Wanapofika huko, wanakutana na mwanamama Bishop. Naye anawavunjia siri ya kuwa, yeye ndiye anayehusika na upotevu wa yai la kwanza lakini amekuja na ofa.
Anawapa uchaguzi wa kwenda kuiba yai la pili kwa Doni mmoja anayejulikana kama Sotto Voce na anaahidi kuwapatia asilimia 10 ya fedha atakazozipata baada ya kukamilisha misheni yake.
Booth na Hartley wanakataa. Hata hivyo, wanafanikiwa kutoroka gerezani na kuendelea na safari ya kuiba yai la pili.
Jamani, ninaposema yai, simaanishi yai la kuku au mwewe. Ni dhahabu iliyotengenezwa kwa umbo la yai huku ikizungukwa na vito vya thamani. Ukubwa wa yai hilo la dhahabu unaweza kuufananisha na mpira wa miguu.
Haya wacha tuendelee baada ya kukutoa ukakasi huo.
Wanapoenda kwa Voce, Bishop naye yupo huko. Wanapokutana, kilichopo mbele ni kuona nani ataondoka kwenye nyumba hiyo na yai. Timu Booth au timu Bishop.
Tusimalize uhondo, fahamu kuwa filamu hii imejaa usaliti, siri za kukatisha tamaa na imani inayovunjwa kama kioo cha mwanadada aliyekasirika.
Waigizaji mashuhuri utakaowaona ni pamoja na Dwayne Johson maarufu kama The Roc, Ryan Reynolds ambaye ni nyota wa filamu mbalimbali kama ‘Dead pool’ na “Free Guy” bila kumsahau, mwanadada mwenye miondoko yake, Gal Gadot au wengi tunamfahamu kama ‘Wonder woman’.
Tazama filamu hii kupitia jukwaa la filamu la mtandaoni la Netflix kushuhudia jinsi imani yako juu ya mtu inavyoweza kukuponza.
Mimi nanga yangu nimeishusha hapa.
Latest
