Kisasi kinavyogeuka kuwa safari ya penzi jipya
- Ni filamu ya The Protege, inamhusu mwanadada ambaye waovu wamemaliza familia yake.
- Anaporudi kulipiza kisasi, sukari inamwagikia kwenye chai baada ya kumkuta ampendaye kuhusika.
- Damu kumwagika huku historia ikirudi kuwawinda wahusika ni sehemu ya filamu.
SIKILIZA SIMULI HII HAPA
“Ningependa kukuona tena lakini kwenye hali tofauti”, anasema Rembrandt.
“Hii ndiyo hali nzuri utakayowahi kuiona nayo” anajibu Anna Dutton, sura yake ikionyesha kuwa kinachomfuatia Rembrandt ni kiama.
Wawili hao walikuwa kwenye meza ya mazungumzo ya amani. Vitisho, majibizano ni sehemu ya vitu alivyoambulia Anna, mwanadada mwenye umahiri wa silaha zake.
Mizizi ya filamu hii inaanza kwake Moody Dutton almaarufu kama Samuel Jackson. Unaweza kuwa unamfahamu kupitia filamu mbalimbali ikiwemo The Hitman’s Bodyguard, The Avengers, Shaft na orodha inaweza kumaliza muda mwingi kuitaja.
Kwenye filamu hii, nguli huyo anafahamika kama Moody.
Kwenye harakati zake za kila siku, Moody anakutana na Anna. Binti mdogo ambaye wanafamilia wake wote wameuwawa na yeye ametekwa.
Hata hivyo, binti huyo hakuwa wa mchezo mchezo kwani aliwaua watekaji wake lakini jambo ambalo halibadiliki ni kuwa, hana ndugu tena na hana sehemu pa kuita nyumbani anapoweza kurudi.
Moody anamchukua binti huyo na kuvaa jukumu la kuishi naye kama ndugu na rafiki lakini kubwa zaidi, mchapakazi mwenzake.
“Hii ndiyo hali nzuri utakayowahi kuiona nayo” anajibu Anna Dutton. Picha| Ultimate Action Movie Club.
Kwa miaka na miaka, wawili hao wanaizunguka dunia wakitimiza mikataba ya mauaji ikiwa ndiyo kazi yao inayowaweka mjini.
Kwao kuua siyo ishu, ni leta jina la mtu unayetaka uhai wake urudi kwa muumba wake na kama ilivyo kasi ya kimondo angani, ndivyo ilivyo kasi ya utendaji kazi wao.
Hata hivyo, miaka inaenda na wawili hao wanaona ni muda wa kishi maisha ya kawaida. Wanaamua kustaafu na Anna anafungua duka la vitabu nchini Uingereza ndoto yake ikiwa ni kufungua ukurasa wa maisha mapya.
Kazi inayomrudisha Anna kwenye cheo chake
Kwa mara ya kwanza, Anna anakutana na Rembrandt dukani kwake. Muonekano wake wa kwanza ni ule wa mtu mstaarabu na dukani kwa Anna alikuwa amekuja kununua kitabu kwa ajili ya zawadi kwa mtu.
Siku za ustaafu za Moody zinaongezewa utulivu baada ya kuuliwa. Kwa Anna, Moody ni familia pekee iliyokuwa imebaki na hawezi kuacha muuaji wa mlezi wake apotee hivi hivi.
Inamlazimu arudi nchini Vietnam kuchimbua uzi wa muuaji wa baba yake mlezi. Chimbu na chimbu, uzi huo unaishia kwa Edward Hayes.
Nyepesi nyepesi ni kuwa, Moody aliwahi kufanya kazi na Hayes miaka mingi iliyopita. Mimi na wewe, hatujui ni nini kilienda mrama kati yao.
Kupambana na Hayes, kunamkutanisha Anna na sura ambayo siyo ngeni. Ni sura ya Rembrandt na muktadha huu ni wazi kuwa ni kijakazi wa Hayes.
Kutafuta kisasi kwa aliyemuua mlezi wa baba yake, kunamkutanisha Anna na kinachodhaniwa ni kiberiti cha huba yake.
Usaliti, kutimia kwa msemo wa “what goes around comes back around” ndiyo haswaa, dhima ya filamu hii ya The Protege inayowaleta nguli wa filamu kongwe kama The Terminator, Code Red, The Hooligan Factory na nyingine kibao.
Unaweza kuitazama filamu hiii kupitia kumbi za kuangalizia filamu kama Century Cinemax zilizopo kwenye maduka makubwa yaani “malls” ikiwemo Dar Free Market ya Namanga, Aura mall ya Frire na Mlimany City mkoani Dar es Salaam.
Tufollow kwenye social media @Nukta Tanzania iwe ni Instagram, Facebook na Twitter na pia unaweza kuituma podcast hii kwa rafiki na wengine kama jitihada ya kutuunga mkono.
Nos vemos.
Latest