Kifahamu kisa cha kuumiza kinachoihusu kampuni ya Gucci
- Filamu ya “House of Gucci” inasimulia kiundani kisa hicho.
- Ni kisa cha mapenzi kinachosababisha familia ya Gucci kuingia matatani
Dar es Salaam. Ukisikia Gucci, kinachokuja kichwani bila shaka ni pochi, mavazi, viatu na siyo vile vya bei ya mtu mnyonge. Lakini ulishawahi kujiuliza, kwanini hakuna mtu mwenye jina hilo katika umiliki wa kampuni ya Gucci?
Filamu ya ‘House of Gucci’ inakusimulia mabonde na milima yanayoambatana na jina la brand hiyo maarufu kote duniani.
Kabla ya yote, nianze kwa kuuliza swali, hivi umewahi kwenda sehemu halafu jambo baya likakukuta hadi ukajutia kwanini ulienda sehemu hiyo?
Mfano unaweza kuwa ‘umechill’ ‘geto’ kwako alafu rafiki zako wakakubembeleza muende kujirusha.
Mkifika huko unaibiwa simu au kitu chochote cha thamani na hakuna ambaye hata anakutazama usoni kwa kutaka kukusaidia kupata simu yako iliyopotea au kukununulia mpya.
Unaweza ukawalaani kwa nini walikubembeleza muende kwa sababu unaamini kama usingeenda jambo hilo lisingekupata.
Kwa lugha iliyoletwa na meli hicho kisa kinaitwa “fate”. Kwa wazawa kama mimi tunaiita hatma ambayo hata ufanyaje huwezi kuikimbia wala kuihamisha kwa mtu mwingine. Hatma ndiyo inamkuta mwanadada Patrizia.
Mrembo huyu baada ya kuwa na siku ndefu kazini, jambo analowaza ni kwenda kupumzika nyumbani lakini rafiki yake anamwambia waende kwenye party walau wakatoe stress za maisha.
Patrizia anakubaliana na wazo hilo. Huenda ukadhani Patrizia anaenda kukutana na jambo baya huko aendako, lakini ni kinyume chake.
Wakiwa na rafiki yake kwenye party, Patrizia anaangukiwa na bahati njema. Picha| NBC News.
Kwa binti huyu aliyekaa ‘singo’ kwa muda mrefu, usiku huo ulikuwa mwisho wa kulala peke yake au unaweza kusema dakika zake za mitandao yote kuexpire na simu.
Patrizia anavutiwa na kijana mmoja anaekutana naye kwenye party hiyo.
Unaweza kuelezea hisia alizo nazo kama mtu kupata msamaha wa deni la timiza au kuwa zamu katika kupokea hela ya kikoba. Bila shaka unajua hisia hizo.
Nimesikia mara nyingi neno “go getter” lakini nimelielewa kwa mwanadada huyu. Hisia zake hazimruhusu kugugumia na tamaa tu, Patrizia anakata shauri na kujitambulisha kwanza.
Hata hivyo, anachanganyikiwa zaidi anaposikia jina la kijana huyo. Ni kama leo nijitambulishe kwa mtu, naye aniambie ni mtoto wa bilionea yeyote hapa nchini.
Kwa Patrizia, Ni Maurizio Gucci, aka mrithi wa brand ambayo wapenda fasheni hawajaruhusu kupitwa na mitindo yake.
Jambo linalobaki ni je, kukutana kwa wawili hawa kutazaa matunda mema au ni yale matunda ya msimu?
Zinazohusiana
- Unataka kufahamu ukomo wa huruma yako? Tazama filamu ya “1917”
- The Informer: Filamu ya mwisho kuitazama Januari 2020
- Filamu ya “Bad Boys for Life” kuwarudisha Smith na Lawrence ulingoni
Mahaba nigaragaze
Baada ya kujuana kwenye party, Patrizia hawezi tena kuzuia hisia zake kwa Maurizio, anaamua kujiweka karibu kama samaki alivyo karibu na maji.
Kama namba zinavyohesabiwa kuanzia sifuri hadi 100, ukaribu wa wawili hao unaongezeka siku hadi siku n///a mwishowe wanakuwa wapenzi.
Penzi linavyozidi kukolea, Rodolfo Gucci, baba yake Maurizio anamuonya kijana wake juu ya penzi hilo na kumwambia kuwa binti huyo yupo naye kwa sababu ya pesa.
Mzee Gucci ni kama ameuwasha moto kwani anajikuta akiishia kugombana na kijana wake juu ya suala hilo na zaidi Maurizio anaondoka nyumbani hapo na kuhamia kwa akina Patrizia.
Maurizio anaenda mbali zaidi kwa kuamua kufunga ndoa na Patrizia bila kujali onyo alilopewa na baba yake.
Bila kujali onyo la baba yake, Maurizio anamuoa Patrizia. Picha| Brides.
Mwana “kulifind”, mwana “kuliget”
Waswahili husema, tabia ya mtu ni harufu. Hata upake manukato gani, ukioga harufu yako itabaki tu. Baada ya kuingia kwenye ndoa, Patrizia anaanza kuonesha makucha yake ambayo yanaanza kuleta ugomvi ndani ya nyumba kila uchao.
Ni kweli mzee Gucci hakukosea, binti huyu alikuwa amezifuata pesa huku lengo lake kubwa likiwa ni kuimiliki Gucci.
Patrizia anatumia maujanja yake hadi anapata asilimia 50 ya hisa za kampuni hiyo lakini kimbembe kinabaki kwenye 50 zilizobaki ambazo zinamilikiwa na mumewe.
Atazipataje na mumewe ameshakuwa adui yake sasa?
Hilo swali unajiuliza wewe lakini Patrizia mbele ya pesa ni kama Simba mwenye njaa amuonapo Swala, hana huruma hata kidogo.
Unahisi ni nini binti huyu atafanya? Je yule kipofu wa mapenzi Maurizio atailaani siku aliyoenda kwenye party na kukutana na shetani wake?
Nani ataishia kuwa mmiliki wa Gucci?, majibu ya maswali hayo yapo kwenye filamu hii, ambayo sidhani kama utaacha kuitazama.
Ndani humo utakutana na nguli maarufu akiwemo Lady Gaga, Jared Leto, Adam Driver, Salma Hayek na wengine kibao.