Ewura: Watanzania wajifunge mkanda kupanda bei ya mafuta
- Serikali yasema vita ya Ukraine, Rusia yachangia.
- Bodaboda kupandisha nauli.
- Serikali yashauri watu kutumia gesi na umeme kupunguza makali.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewataka watumiaji wa vyombo vya moto nchini Tanzania kuendelea kujifunga mkanda kwa kuwa bei ya mafuta ya petroli inatarajiwa kuendelea kupanda kutokana na hali ya soko la dunia.
Kauli ya Ewura imetoka siku chache kabla ya mamlaka hiyo kutangaza bei mpya zinazotarajiwa kuanza Aprili 6 mwaka huu. Ewura hutangaza bei mpya za mafuta kila Jumatano ya kwanza ya mwezi.
Kaimu Mkurugenzi wa EWURA, Godfrey Chibulunje amewaambia wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo (Aprili 2, 2021) kuwa vita inayoendelea kati ya Urusi na Ukraine imesababisha kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia baada ya mifumo ya usafirishaji wa petroli na dizeli katika maeneo mbalimbali duniani kutatizika.
Kutokana na hali hiyo, amesema bei za mafuta zitaendelea kupanda nchini na amewataka Watanzania kufunga mikanda kwa sababu suala hilo linagusa dunia nzima na bei za mafuta zinazotumika Tanzania hutegemea zaidi mwenendo wa bei katika soko la dunia na gharama za usafirishaji.
“Tusijione tuko katika hali mbaya, hatuko peke yetu bidhaa za mafuta zimepanda duniani kote,” amesema Chibulunje.
Kwa mujibu wa Chibulunje, tani moja ya petroli katika soko la dunia kwa Desemba 2021 ilikuwa Dola za Marekani 717 (Sh1.6 milioni) lakini imepanda hadi Dola 1,106 (Sh2.5 milioni) mwezi Machi mwaka huu.
Bei ya mafuta ya petroli katika soko la dunia imekuwa ikipanda tangu katikati mwaka 2021 kutokana na kuanza kurejea kwa shughuli za kiuchumi baada ya athari za Uviko-19 huku vita ya Urusi na Ukraine ikipaisha zaidi.
Mfano, Machi 30, 2022 pipa moja la mafuta ghafi lilikuwa likiuzwa Dola za Marekani 114.27 (Sh262,821) katika soko la dunia kutoka Dola za Marekani 79.86 (Sh183,678) Desemba 30, 2021 kwa mujibu wa tovuti ya Tradingeconomics.
Zinazohusiana:
- Funga mkanda: Maumivu bei ya mafuta kuendelea Tanzania
- Mifuko kutoboka zaidi kwa wamiliki wa magari, petroli ikipanda
- Ahueni bei ya petroli ikishuka Tanzania
Mafuta bado yapo ya kutosha
Hata hivyo, amesema hakutakuwa na upungufu wa mafuta nchini kwa sababu kuna akiba ya kutosha na meli zinaendelea kuleta na kupakua mafuta katika bandari za Mtwara, Dar es Salaam na Tanga.
“Mafuta yapo ya kutosha na meli zinaendelea kuja bandari kwa hiyo hakuna sababu ya wananchi kuhofia upungufu wa mafuta,” amesema Chibulunje huku akibainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kutafuta mbadala wa changamoto za mafuta nchini.
Hatua hizo ni pamoja na kuhimiza matumizi ya gesi asilia na umeme katika shughuli za uzalishaji na magari ili kuwapunguzia wananchi maumivu.
Pia, Serikali inaendelea na jitihada za kuboresha na kupanua miundombinu ya kuhifadhia mafuta ili kuwa na akiba ya kutosha itakayosaidia katika kipindi bei zinapopanda duniani.
Meneja wa Ufundi Kitengo cha Mafuta EWURA, Shabani Suleiman amesema kwa sasa Tanzania ina akiba ya petroli ya kutumia kwa siku 27, dizeli (siku 19) na mafuta ya taa kwa siku 114.
“Hatuna wasiwasi kwa sababu mafuta yanaendelea kuja na wakala wameagiza mengine ili kukidhi mahitaji ya Watanzania,” amesema Suleiman.
Bodaboda, bajaj wajipanga kuongeza nauli
Watumiaji wa vyombo vya moto wameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuendelea kupanda kwa bei ya mafuta kunazidi kuongeza gharama za maisha na biashara jambo linalotishia kuwadidimiza kwenye umaskini.
Dereva wa bodaboda wa kituo cha Makumbusho jijini Dar es Salaam, Said Jumbe amesema kwa hali hiyo atalazimika kupandisha nauli anazowatoza wateja wake ili kujinusuru na maumivu hayo.
“Sina jinsi nitapandisha nauli maana biashara imekuwa ngumu sana, mafuta yako juu na faida niliyokuwa napata zamani imepungua,” amesema Jumbe.
Miezi ya hivi karibuni Serikali iliondoa baadhi ya tozo katika bidhaa za mafuta ya petroli ili kupunguza maumivu kwa wananachi.
Kupanda kwa bei ya petroli kutawaongezea maumivu watumiaji wa vyombo vya moto. Picha| Mariam John.
Hata hivyo, mapema wiki hii Rais Samia Suluhu aliagiza kurejeshwa kwa tozo ya Sh100 kwa lita katika bidhaa hiyo ambayo iliondolewa mwishoni mwa Februari na Waziri Januari Makamba akieleza kuwa hatua hiyo ilikuwa kinyume na taratibu za kibajeti na itapunguza mapato serikalini.
Kurejeshwa kwa tozo hiyo kutafanya bei ya mafuta kupanda kwa Sh100 zaidi kabla ya kusadifu mabadiliko yatokanayo na bei katika soko la dunia.
Hii ina maana kuwa iwapo bei za Machi kwa kuakisi soko la dunia zitabaki kama Machi, watumiaji wa petroli jijini Dar es Salaam watanunua lita moja kwa Sh2,640 kiwango ambacho ni zaidi kwa Sh100.
Waiomba Serikali iondoe tozo
Licha ya Serikali kurejesha tozo hiyo, Allen Kisoka, dereva bajaji Mwananyamala jijini hapa ameiomba Serikali kuendelea kuondoa tozo zote za mafuta ili wananchi wa kawaida wapate ahueni.
Hata hivyo, baadhi ya wadau wa nishati wanaeleza kuwa suluhu ya kudumu ya tatizo la mafuta ni Serikali kuweka sera imara zitakazoongeza matumizi ya gesi asili nchini katika shughuli za usafirishaji.
Latest