Dar es Salaam yaongoza pato kwa kila mtu Tanzania mwaka 2025
- Pato la Taifa kwa kila mtu (GDP per capita), ni kiashiria cha kiuchumi kinachopatikana kwa kugawa thamani ya jumla ya bidhaa na huduma zinazozalishwa katika eneo husika kwa idadi ya watu wa eneo hilo ndani ya kipindi maalumu.
Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umeongoza kwa kuwa na pato la Taifa kwa kila mtu lililo juu zaidi Tanzania Bara mwaka 2025, ukirekodi wastani wa Sh6.78 milioni kwa kila mkazi aishie mkoani humo.
Takwimu zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika ripoti ya Tanzania in Figures 2025 zinaonyesha tofauti za thamani ya uzalishaji wa uchumi kwa kila mtu katika mikoa ya Tanzania Bara zinatofautiana
Kwa mujibu wa takwimu hizo, Dar es Salaam ndiyo inayoongoza kwa pato hilo, ikifuatiwa na Iringa iliyorekodi Sh5.71 milioni na Kilimanjaro yenye Sh5.20 milioni kwa kila mtu mwaka 2025.Â
Mbeya imeshika nafasi ya nne kwa kurekodi Sh5.06 milioni kwa kila mtu, huku Njombe ikikamilisha mikoa mitano ya juu kwa kuwa na Sh4.53 milioni.
Arusha imechukua nafasi ya sita kwa kurekodi Sh4.28 milioni, ikifuatiwa na Ruvuma yenye Sh4.16 milioni na Mwanza iliyorekodi Sh4.07 milioni kwa kila mtu.
Mikoa ya Tanga na Manyara imekamilisha orodha ya mikoa 10 inayoongoza, ikiwa na Sh3.80 milioni na Sh3.73 milioni kwa kila mtu, mtawalia.
Pato kwa kila mtu ni nini?Â
Pato la Taifa kwa kila mtu (GDP per capita), ni kiashiria cha kiuchumi kinachopatikana kwa kugawa thamani ya jumla ya bidhaa na huduma zinazozalishwa katika eneo husika kwa idadi ya watu wa eneo hilo ndani ya kipindi maalumu.
Kiashiria hiki hutumika kupima na kulinganisha wastani wa thamani ya uzalishaji wa uchumi kati ya maeneo mbalimbali, lakini hakimaanishi kuwa kila mkazi anapata kiasi hicho cha fedha kama kipato binafsi.
Kwa mfano, pato la Taifa kwa kila mtu la Dar es Salaam lilipofikia Sh6,776,483 mwaka 2025 halimaanishi kuwa kila mkazi wa mkoa huo alipokea fedha hizo kama mshahara, faida ya biashara au mapato mengine.
Hii ni kwa sababu thamani ya uzalishaji wa uchumi hugawanywa kwa idadi ya watu bila kuzingatia jinsi mapato yanavyogawanyika miongoni mwa wakazi.
Kwa hiyo, ingawa takwimu za NBS zinaonyesha mikoa yenye wastani mkubwa wa thamani ya uzalishaji wa uchumi kwa kila mtu, haziwezi kutumika peke yake kuhitimisha kuwa wakazi wa mikoa hiyo wana mishahara au kipato binafsi kikubwa zaidi.