Wastani wa pato la Mtanzania limeongezeka kwa Sh145,397

June 12, 2025 4:46 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni ongezeko la asilimia 4.8 kutoka kiasi cha Sh3.05 milioni kwa mwaka 2023. 
  • Wananchi wasema kuwa ongezeko hilo halionekani kwenye maisha yao ya kila siku.

Dar es salaam. Wastani wa pato la mtu mmoja mmoja Tanzania limeongezeka kwa kiwango cha zaidi ya Sh145,000 ndani ya mwaka mmoja na kufikia Sh3.2 milioni mwaka 2024. 

Kwa mujibu wa kitabu cha Hali ya Uchumi 2024 wastani wa pato la mtu mmoja mmoja nchini lilikuwa Sh3,204,244 kwa mwaka 2024 kutoka kiasi cha Sh3,058,847 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 4.8.

Wastani huo wa pato la mtu mmoja mmoja umepatikana kwa kugawanya pato la taifa (GDP) kwa idadi ya watu, ambapo Tanzania Bara ilikadiriwa kuwa na watu 64,241,822 mwaka 2024 ikilinganishwa na watu 61,718,700 waliokuwepo mwaka 2023.

Kwa mujibu wa kitabu cha Hali ya Uchumi 2024 wastani wa pato la mtu mmoja mmoja nchini lilikuwa Sh3,204,244 kwa mwaka 2024, Picha | Bunge la Tanzania.

Baadhi ya wataalamu wa uchumi kwa muda sasa wamekuwa wakikosoa kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi nchini haikisi vema ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja kutokana na kuwepo utofauti wa kipato baina ya walionacho na wasionacho. 

Mwaka 2024, takwimu hizo zinaonyesha kuwa pato halisi la taifa (GDP) lilikua na kufikia Sh156.6 trilioni kutoka Sh 148.5 trilioni mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 5.5 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.1 mwaka 2023.

Hali ikoje kwa wananchi

Wakati takwimu wa Serikali zikionyesha kuwa pato la Taifa na pato la Mtanzania mmoja mmoja likiendelea kukua mwaka hadi mwaka, baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam waliohojiwa na Nukta Habari wamesema ongezeko hilo halionekani kwenye maisha yao ya kila siku. 

Edwin Tesha (27) mkazi wa Dar es Salaam amesema haamini kuwa kwa wastani kila Mtanzania anaweza kupata kiasi cha Sh3.2 milioni kwa mwaka na iwapo wapo basi ni wachache ikilinganishwa na idadi ya watu.

Wananchi wasema kuwa ongezeko hilo halionekani kwenye maisha yao ya kila siku. Picha | Mwananchi.

Tesha, anayeendesha Bajaj, amebainisha kuwa hata wanaoweza kupata wanapata kwa ugumu kutokana na gharama za maisha kuwa juu hivyo kufanya upatikanaji wa fedha kuwa mgumu.

“Kuanzia asubuhi mpaka jioni mtu anaweza kupatia abiria safari tatu tu, unadhani hata iyo milioni tatu kwa mwaka anaipata wapi ?” amehoji Tesha.

Bado uchumi si jumuishi

Wataalamu wa uchmi wanasema ukuaji wa pato la Taifa hauakisi uchumi wa mtu mmoja mmoja kwa sababu wastani wa pato la mtu mmoja mmoja hujumuisha kipato cha walionacho na wasionacho.

Mtaalamu wa uchumi na fedha, Profesa Alfred Kinyondo amesema kutokuwepo kwa sera na miongozo mizuri kutoka kwa Serikali kumechangia kwa muda mrefu umasikini uliokubuhu licha ya takwimu kubainisha kuwa pato la taifa na wastani wa pato kwa mtu mmoja mmoja unaongezeka.

“Nikikupa mfano tu kwa kipindi cha tangu mwaka 2000 mpaka 2022, Tanzania imepunguza umasikini uliokubuu kwa asilimia 10 tu,” amesema Prof Kinyondo.

Pamoja na mfumo huu unaotumika duniani kote, amesema, bado bado Serikali ina jukumu la kuhakikisha inatunga sera zitakazowezesha ukuaji huo kuwa ukuaji jumuishi kwa watu wenye kipato na wasionacho.

“Kama Serikali haitatengeneza Sera nzuri, pato litakua, wastani wa pato kwa watanzania utakua lakini bado umaskini uliokubuu utaendelea kuwepo”  amesema Prof Kinyondo.

Sekta zilizochangia kukua kwa uchumi

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, kwa mwaka 2024 Sekta tatu zilichangia zaidi kwa takribani nusu ya pato la Taifa ni sekta ya kilimo ambayo imechangia kwa asilimia 26.3, ujenzi asilimia 12.8 pamoja na uchimbaji wa madini na mawe kwa asilimia 10.1. 

Aidha, sekta zilizoongoza kwa ukuaji mwaka 2024 ni sekta ya sanaa na burudani ambayo imekuwa kwa asilimia 17.1, uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme asilimia 14.4, habari na mawasiliano asilimia 14.3%, fedha na bima asilimia 13.8 na afya asilimia 10.1.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks