Usipime! Msongamano wa watu Dar

September 20, 2021 11:22 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Moja ya mitaa katika eneo la Kariakoo jijini hapa ambalo husifika zaidi kwa shughuli za kibiashara. Picha| Wanted in Africa.


  • Wastani wa watu 3,878 wanakaa kwa kila kilomita ya mraba.
  • Yafuatiwa na Mkoa wa Mjini Magharibi kwa wastani wa watu 3,191.
  • Upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii na fursa za kiuchumi wachangia.

Dar es Salaam. Licha ya idadi ya watu kuendelea kuongezeka nchini Tanzania, Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaongoza kwa msongamano mkubwa wa watu kuliko mikoa mingine, jambo linalohitaji uboreshaji zaidi wa miundombinu ili kukidhi ongezeko la watu.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), idadi ya watu waliopo Tanzania ikakadiriwa kufikia milioni 59.5 mwaka 2021 huku wanawake wakiwa ni asilimia 50.9 ya watu wote.

Idadi hiyo imeongezeka kutoka makadirio ya watu milioni 57.6 waliorekodiwa mwaka jana, kwa mujibu wa Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020. Makadirio haya yanatokana na maoteo ya idadi ya watu kwa kutumia matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 pamoja na viashiria muhimu vya mabadiliko ya idadi ya watu vikijumuisha uzazi, vifo na uhamiaji.

Licha ya ongezeko hilo la watu, Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaongoza kwa kuwa idadi kubwa ya watu Tanzania.

Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2020 kinaeleza kuwa hadi kufikia Desemba mwaka jana, mkoa huo uliopo Mashariki mwa nchi ulikadiriwa kuwa na watu milioni 5.4 sawa na asilimia 9.7 ya watu wote Tanzania Bara ambayo ni idadi kubwa ikilinganishwa na mikoa mingine.

Wingi wa watu wa Dar es Salaam umechangia mkoa huo kuwa na kiwango cha juu kabisa cha msongamano wa watu kwa kila kilomita moja ya mraba. 

Kwa mwaka 2020, Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na msongamano mkubwa zaidi ukiwa na wastani wa watu 3,878 kwa kila kilomita ya mraba.

Kiwango hicho cha msongamano wa watu wa Dar es Salaam ni zaidi ya takriban mara 10 ya msongamano uliopo Mkoa wa Mwanza ambao unashika nafasi ya pili Tanzania Bara. 

Msongamano wa Mwanza ni wastani wa watu 404 katika kilomita moja ya mraba.  

Dar es Salaam ambayo ina ukubwa wa kilomita za mraba 1,400 iko juu ya wastani wa kitaifa wa msongamano wa watu kwa zaidi ya mara 59.

Msongamano wa watu kwa Tanzania ulikuwa wastani wa watu 65 kwa kila kilometa ya mraba mwaka 2020 ikilinganishwa na wastani wa watu 63 mwaka 2019.

“Idadi kubwa ya watu katika mkoa wa Dar es Salaam ilichangiwa na upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii na fursa za kiuchumi zilizosababisha watu kuhamia kutoka mikoa mingine,” imeeleza sehemu ya kitabu hicho kinachopatikana katika tovuti ya NBS. 

Aidha, Mkoa wa Lindi ulikuwa na msongamano mdogo zaidi ukiwa na wastani wa watu 16 kwa kila kilomita ya mraba, ukifuatiwa na mkoa wa Katavi wastani wa watu 18 kwa kila kilomita ya mraba.

Kwa upande wa Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi ulikuwa na msongamano mkubwa wa wastani wa watu 3,191 kwa kila kilomita ya mraba ukifuatiwa na Mkoa wa Kusini Pemba uliokuwa na wastani wa watu 820 kwa kila kilomita ya mraba. 

Mkoa wa Kusini Unguja ulikuwa na msongamano mdogo zaidi ukiwa na wastani wa watu 162 kwa kila kilomita ya mraba.

Benki ya Dunia inaeleza kuwa idadi ya watu itaendelea kuongezeka kwa kasi katika miji mikubwa duniani ambapo watu saba kati ya 10 watakuwa wanaishi katika majiji makubwa duniani ifikapo 2050.

Benki hiyo imependekeza kuwa Serikali zinatakiwa kuweka mikakati ya kisera na kisheria kuhakikisha zinakabiliana na changamoto za ongezeko la watu ikiwemo mipango miji na uboreshaji wa huduma za kijamii.

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
15 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
15 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
15 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Mwenendo wa deni la serikali

Mwenendo wa deni la serikali

Nukta TV

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Rais Samia: Uchumi wa nchi unapanda , lakini ukifika kwa watu hali si nzuri

Nukta TV

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Gavana Tutuba afichua kiasi cha dhahabu kilichopo BoT thamani yake

Nukta TV