Corona: WHO yawaonya watu kutumia chanjo zaidi ya moja

July 14, 2021 9:26 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Yasema kitendo hicho ni hatari.
  • Yawataka wasubiri ufanyike utafiti kuhusu jambo hilo.
  • Yasisitiza matumizi sahihi ya chanjo kuwakinga watu.

Mwanza. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limewaonya baadhi ya watu ambao wanafikiria kutumia chanjo ya Corona zaidi ya moja na kueleza kuwa tabia hiyo inaweza kuwa na madhara kwa watu hao na pia kwa nchi zao.

Jango la Uviko-19 likiwa na miezi 18 sasa duniani, idadi kubwa ya watu katika nchi zilizoendelea tayari wamepata chanjo ya dhidi ya ugonjwa huo huku nchi zingine zikiendelea kuwatafutia wananchi wao.

Upatikanaji wa chanjo katika nchi hizo zilizoendelea umekuwa rahisi ambapo baadhi ya watu waliokwisha kupata chanjo iwe ile ya dozi mbili ikiwemo Moderna na dozi moja ya Johnson Johnson wanaripotiwa kufikiria kwenda kupata chanjo ya ziada jambo ambalo WHO inasema kitendo hicho kinaweza kuwa tatizo.

Mwanasayansi Mkuu wa WHO, Dk Soumya Swaminathan anasema kuna tabia ya watu katika nchi zenye chanjo za kutosha kwa hiari yao kuanza kufikiria kuongeza dozi. 

“Wengine wanafikiria kuchanganya na kulinganisha, tumeona maswali mengi ya watu waliopata aina moja ya chanjo na wanapanga kuchukua aina nyingine ya chanjo,” amesema Dk Swaminathan. 

Anasema suala hilo ni hatari kwa wanaowaza kufanya hivyo ingawa katika eneo hili kuna takwimu chache juu ya kuchanganya au kulinganisha chanjo.

“Utafiti mdogo wa kubaini suala hili bado unaendelea,” amesema mtaalam huyo kuwa wanafanya utafiti kama inawezekana kwa mtu kuchanganya chanjo.

Lori lililoratibiwa UNICEF Afrika Kusini na idara za afya za nchi hiyo limekuwa likionyesha video na kutoa matangazo ya watu kuelezea hadithi zao kuhusu COVID-19 kote Afrika Kusini kwa kutumia lugha yao ya mama na kuhamasisha ujumbe wa kupokea chanjo. Picha| UNICEF South Afrika.

Dk Swaminathan amewataka watu kusubiri matokeo ya utafiti yatoke na kwa sasa waendelee kutumia chanjo zilizopendekezwa.

“Jambo hili litaleta balaa kwa hizi nchi kama wananchi wake wataanza kujiamulia muda gani na nani anapaswa kuchukua chanjo ya pili, ya tatu na nne,” amesema.

Ili kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa COVID-19, Shirika la Afya Duniani (WHO) mpaka sasa limeidhinisha aina 6 za  chanjo kwa ajili ya matumizi ya dharura.

Chanjo hizo ni Pfizer/BioNTech, AstraZeneca/Oxford, Moderna, Johnson & Johnson, Sinovac na Sinopharm. Chanjo hizo ni miongoni mwa chanjo zaidi ya 200 ambazo ziko kwenye utafiti ili kukabili Corona.

Mkuu wa programu ya chanjo kutoka WHO, Dk Ann Lindstrand amesema bado hakuna takwimu za kuthibitisha uhitaji wa kuongeza nguvu kwenye chanjo watu walizopatiwa.

Amesema jopo la wataalum wa ushauri na mikakati linaendelea kuangalia iwapo kuna uhitaji wa kutumia dozi ya kuongeza nguvu kwenye chanjo ambazo watu wameshapatiwa.

Hata hivyo, WHO inasema Corona bado ni janga ulimwengu hivyo nchi zinapaswa kuwahimiza wananchi wake kujilinda na kuwalinda wale walio katika hatari zaidi ya kupata maambukizi katika jamii zao.

WHO yasisitiza kuwa wasipofanya hivyo hospitali zitazidiwa na nchi hazitakuwa na uwezo kudhibiti maambukizi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW