Boti 320 zitakavyowasaidia wavuvi kuongeza uzalishaji Tanzania
- Serikali itazinunua na kuwakopesha wavuvi nchini.
- Boti za kisasa zitasaidia kuongeza uzalishaji wa samaki na dagaa.
Dar es Salaam. Huenda wavuvi wadogo na wa kati nchini Tanzania wakaongeza uzalishaji na soko la samaki na dagaa baada ya Serikali kuwaandalia mpango maalum wa kuwapatia vifaa vya kisasa vya uvuvi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amesema Serikali ina mpango wa kuwakopesha wavuvi boti 320 ambazo zitawasaidia kuendeleza shughuli zao za uvuvi.
Mpango huu unaotarajia kuwafikia wavuvi mbalimbali nchini unatazamia kuwanufaisha wavuvi kutumia boti hizo kuvua mazao ya samaki ambayo hutumika kujipatia kipato.
“Mojawapo ya mkakati ni kwenye bajeti mwaka ujao Mheshimiwa Naibu Spika tuna mpango mkakati kununua boti 320 kwa nchi nzima ili tuweze kuzikopesha kwa wavuvi wadogo wadogo na wavuvi wa kati,” amesema Ndaki.
Waziri Ndaki alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Ukerewe Joseph Mkundi Bungeni jijini Dodoma leo (Juni 13, 2022) aliyetaka kujua ni kwa kiasi gani Serikali itasaidia wavuvi kuwa na zana bora katika shughuli za uvuvi.
Waziri Ndaki amebainisha kuwa Serikali katika mwaka ujao wa fedha utakaonza Julai 1, 2022 itanunua boti hizo na kuwakopesha wavuvi wadogo na wa kati wanaofanya shughuli zao katika maziwa na bahari ili kuongeza uzalishaji.
Zinazohusiana:
- Njia zilizotumika kufyekelea mbali uvuvi wa mabomu Dar
- Mpina apania kujenga viwanda vya samaki, nyama nchini
- Ripoti Maalum: Mbinu za kubaini samaki waliovuliwa kwa mabomu
Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi hadi Aprili 30, 2022, jumla ya wavuvi wadogo wapatao 194,804 walishiriki moja kwa moja katika shughuli za uvuvi kwa kutumia vyombo vya uvuvi vipatavyo 57,991.
Wavuvi hao waliweza kuvuna tani 415,880 za samaki zenye thamani ya Sh2.8 trilioni.
Waziri Ndaki amesema juhudi hizo zinazofanywa na Serikali ni kuwasaidia wavuvi ili waweze kuwa na uwezo wa kuvua katika maji marefu upande wa bahari lakini pia upande wa maziwa nchini.
Aidha, Waziri Ndaki ameongeza kuwa mpango mwingine ni kuboresha mialo pamoja na vichanja ili wavuvi wanapovua mazao ya samaki wapate sehemu nzuri za kuanikia.
Katika mwaka ujao wa fedha 2022/23 Wizara ya Mifugo na Uvuvi inakadiriwa kutumia Sh168.2 bilioni ili kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuboresha maslahi ya wavuvi.
Latest