Serikali ya Tanzania yaongeza bajeti ya mifugo, uvuvi kwa Sh99 bilioni

May 25, 2022 2:28 pm · David
Share
Tweet
Copy Link
  • Kiwango kilichoongezwa bado ni kidogo.
  • Serikali imekuwa ikikosolewa vikali kwa kutowekeza ipasavyo katika masuala ya mifugo na uvuvi.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania kwa mara nyingine imeongeza bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa Sh99 bilioni ndani ya mwaka mmoja kutoka  Sh169.1 bilioni  mwaka 2021/2022 hadi Sh268.2 bilioni katika mwaka ujao wa fedha wa 2022/2023, kiwango ambacho kamati ya Bunge inasema bado hakitoshelezi mahitaji.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameliambia Bunge jijini Dodoma leo (Mei 25, 2022) kuwa kati ya fedha hizo Sh92.5 bilioni ni kwa ajili ya sekta ya mifugo na Sh176.2 bilioni zilizosalia zitatumika kukuza sekta ya uvuvi.

Katika makadirio hayo ya mapato na matumizi ya wizara yake, Ndaki amesema Sh45.3 bilioni zilizopangwa kwenye sekta ya mifugo zitatumika kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh.46.7 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Kati ya Sh176 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya sekta ya uvuvi, Sh40.5 bilioni zitatumika kwa ajili matumizi ya kawaida huku Sh135.6 bilioni sawa na asilimia 77 au robo tatu ya fedha hizo zitatumika kugharamia miradi ya maendeleo.

Sekta ya mifugo na uvuvi ni miongoni mwa sekta muhimu katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ikizingatiwa kuwa theluthi mbili ya Watanzania wanategemea shughuli za kilimo kujiendeleza kiuchumi.

Mfugaji akiwapeleka ng’ombe malishoni. Picha|Nuzulack Dausen/Nukta

Hata hivyo, Serikali imekuwa ikikosolewa vikali kwa kutowekeza ipasavyo katika masuala ya mifugo na uvuvi ambayo yanachangia kwa kiwango kikubwa ukuaji wa sekta nyingine zikiwemo za viwanda na biashara.

Ili kukuza sekta hiyo, Serikali imekuwa ikiongeza bajeti mwaka hadi mwaka. Katika mwaka wa fedha 2020/21 Serikali iliongeza bajeti ya wizara hiyo hadi kufikia Sh66.8 bilioni kutoka Sh64.9 bilioni mwaka 2019/20.

Pamoja na Serikali kuongeza bajeti hiyo katika mwaka wa fedha ujao unaoanza Julai, Kamati ya kudumu ya bunge ya kilimo, mifugo na maji imesema licha ya kuongezeka bado kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na majukumu makubwa iliyonayo wizara hiyo.

“Uchambuzi umeonesha kuwa bajeti ya wizara ya mifugo na uvuvi kuna ongezeko la bajeti ya matumizi ya kawaida kwa asilimia 132.15 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022…takwimu hizi zinadhihirisha kuwa uendeshaji wa shughuli za wizara ya mifugo na uvuvi zimeongezewa msukumo katika bajeti.,” amesema Mwenyekiti wa kamati hiyo Dk Christine Ishengoma.

“Hata hivyo, kiasi cha bajeti kilichoongezwa ni kidogo ikilinganishwa na majukumu makubwa iliyonayo wizara katika kuhakikisha tija inaongezeka kwa kuimarisha sekta ya mifugo na uvuvi,” ameongeza wakati akiwasilisha maoni ya kamati kuhusu utekelezaji wa bajeti ya 2021/22 na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk Christine Ishengoma akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mifugo na uvuvi. Picha|Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Baadhi ya wabunge wameeleza kufurahishwa na hatua ya Serikali kuongeza bajeti hiyo licha ya wengine kuwa na wasiwasi iwapo itatekelezwa yote kama mipango inavyobainisha kwa kuwa wizara hiyo haipewi kipaumbele kama nyingine.  

“Kilimo tulikuwa tunapiga kelele kuongezewa bajeti miaka yote lakini bajeti imeongezeka, kwa kweli mimi niwaambie hotuba hii haijanigusa naomba kama mna majibu, kidogo yataamsha ari yangu na kuwa na matumaini mapya mje nayo wakati mnahitimisha mjadala,” amesema Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mariamu Ditopile.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW