BoT yatoa masharti mapya fedha za kigeni Tanzania kutuliza uchumi
- Ni pamoja na kuzuia madalali wasiosajiliwa kufanya biashara hiyo nchini
- Watakaokiuka kuadhibiwa kwa mujibu wa Sheria ya fedha za kigeni ya 1992
Dar es Salaam. Katika kudhibiti soko la fedha la kigeni na kuleta utulivu wa uchumi, Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa maelekezo mapya kwa taasisi zinazojihusisha na fedha za kigeni ikiwemo kuhakikisha barua zote za udhamini za shehena zinazopitia nchini kufanywa na fedha za kigeni kutoka katika nchi husika.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba katika sekula kwa taasisi zinazojihusisha na biashara ya fedha za kigeni iliyotolewa Jumatano hii (Mei 31, 2023) amesema hatua hizo zimelenga kulinda utulivu wa uchumi mpana na udhibiti wa mfumo wa kifedha nchini.
Maelekezo hayo yanakuja ikiwa zimepita siku chache tangu kuibuka kwa taarifa ya kupungua kwa akiba ya fedha za kigeni nchini ikiwemo mahitaji makubwa ya Dola ya Marekani kwa ajili ya kuagiza bidhaa na huduma nje ya nchi.
Taarifa ya sera ya fedha ya BoT ilitolewa hivi karibuni inaeleza kuwa akiba ya fedha za kigeni ilishuka hadi Dola za Marekani bilioni 4.9 (Sh11.4 trilioni) Aprili mwaka huu kutoka Dola za Marekani bilioni 5.5 9 (Sh12.8 trilioni) Aprili mwaka jana ikiathiriwa zaidi na madhara ya vita ya Urusi na Ukraine na Uviko-19.
BOT imeagiza miamala yote ya fedha za kigeni inayozidi thamani ya Dola za Marekani milioni 1 sawa na Sh2.3 bilioni za Tanzania kwa muamala mmoja katika soko la rejareja, kufanyika kwa bei ya soko la fedha za kigeni baina ya benki.
Hata hivyo, BOT imeongeza kuwa miamala yote ya mteja mmoja kwa siku itajumlishwa ili kujua jumla ya kiasi husika kilichobadilishwa.
Mbali na hatua hizo, BoT imewapiga marufuku madalali wa kimataifa ambao hawajasajiliwa kufanya biashara ya fedha za kigeni.
“Madalali au wafanyabiashara wa fedha za kigeni hapa nchini wanatakiwa wakati wote kuzingatia utaratibu wa kumtambua mteja (KYC) kabla ya kufanya naye biashara hiyo,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
BOT imebainisha kuwa kwa sasa kiwango cha juu cha mizania kati ya mali na amana katika fedha za kigeni (foreign exchange Net Open Position (NOP)) kitakuwa asilimia 10 ya mtaji wa msingi (core capital) na kinatakiwa kuzingatiwa wakati wote.
Pamoja na hayo, wafanyabiashara wameagizwa kuwa Barua za Udhamini (Letters of Credit (LCs) za shehena zinazopitia hapa nchini (transit cargoes) zitatokana na fedha za kigeni kutoka katika nchi ambako shehena hizo zinakwenda.
Uamuzi huo wa BoT huenda ukapeleka maumivu zaidi kwa nchi jirani zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam kuingiza mizigo yao hususan zinazokabiliwa na uhaba mkubwa wa Dola za Marekani.
Maelekezo hayo ya BOT, yatakayoanza kutekelezwa Juni Mosi, 2023, yamefuta maelekezo yaliyotolewa Agosti 6, 2020 na benki hiyo huku benki hiyo ikieleza kuwa itafanya ukaguzi wa utekelezaji wake.
Tutuba amesema kukiuka maeleko hayo mapya kutawafanya wafanyabiashara kupigwa adhabu kwa mujibu wa sheria ya fedha za kigeni ya mwaka 1992.
— Bank of Tanzania (@BankOfTanzania) May 31, 2023
Latest