BOT yatoa kanuni mpya kwa maduka ya kubadili fedha za kigeni Tanzania

October 16, 2023 9:12 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Zimeweka madaraja matatu ya leseni za biashara ya maduka ya kubadili fedha za kigeni.
  • Zinafuta rasmi Kanuni za Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni za Mwaka 2019.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa kanuni mpya kwa maduka ya kubadili fedha za kigeni (Bureau de change) za mwaka 2023 ambazo zimeweka madaraja matatu ya leseni za biashara ya maduka ya kubadili fedha za kigeni nchini.

Kanuni hizo mpya, zinafuta rasmi Kanuni za Maduka ya Kubadilisha Fedha za Kigeni za mwaka 2019 ambapo tayari BOT imeshazichapisha kwenye gazeti la Serikali namba 729 la Oktoba 6, 2023.

Taarifa ya Gavana wa BOT, Emmanuel Tutuba iliyotolewa leo Oktoba 16, 2023 imebainisha kuwa makundi hayo ni duka la kubadili fedha za kigeni daraja A, daraja B na daraja C.

“Duka la Kubadilisha Fedha za Kigeni Daraja A ni duka linalomilikiwa na wageni au wenyeji lililoruhusiwa kufungua matawi sehemu yoyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Tutuba.



Tutuba ameongeza kuwa duka la Kubadilisha Fedha za Kigeni Daraja A linalomilikiwa na wageni litatakiwa kuwa na mtaji usiopungua Sh1 bilioni za  Tanzania, wakati duka la kubadilisha fedha za kigeni daraja A linalomilikiwa na wenyeji litatakiwa kuwa na mtaji usiopungua Sh500 milioni za Tanzania.

Aidha, duka la kubadilisha fedha za kigeni daraja A, litaruhusiwa kufanya miamala ya papo kwa papo, kutuma fedha na kufanya biashara kama wakala wa benki, taasisi ya fedha, kampuni ya bima, mtoa huduma wa fedha kwa njia ya simu, au huduma nyingine zozote za fedha kama itakavyoidhinishwa na Benki Kuu ya Tanzania.


Soma zaidi : BOT kununua dhahabu kwa wafanyabiashara, wachimbaji wa ndani


Duka la kubadilisha fedha za kigeni daraja B

Kwa mujibu wa BOT hili ni duka la kubadilisha fedha za kigeni linalomilikiwa na wenyeji ambalo halitaruhusiwa kufungua matawi kwa ajili ya kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni, na litatakiwa kuwa na mtaji usiopungua Sh500 milioni.

Aidha, duka la kubadilisha fedha za kigeni daraja B litaruhusiwa kufanya miamala ya papo kwa papo na kufanya biashara kama wakala wa benki, taasisi ya fedha, kampuni ya bima, mtoa huduma wa fedha kwa njia ya simu, au huduma nyingine zozote za fedha kama itakavyoidhinishwa na BOT.

Duka la kubadilisha fedha za kigeni daraja C

Hili ni duka la kubadilisha fedha za kigeni lililoanzishwa na hoteli yenye hadhi ya nyota tatu au zaidi kwa ajili ya kufanya miamala ya papo kwa papo kwa wateja wa hoteli tu ambapo leseni yake  itatolewa kwa hoteli au kwa mmiliki wa hoteli.

Tutuba amebainisha kuwa daraja hili la duka la kubadilisha fedha za kigeni halitatakiwa kuwa na mtaji wa kufanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW