Benki ya Dunia: Uchumi wa Tanzania kukua 6.1% 2026
- Ukuaji huo wa uchumi kwa sehemu kubwa unategemea kuimarika kwa sekta binafsi na maboresho ya mazingira ya ufanyaji biashara.
Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) inatarajia kuwa uchumi wa Tanzania utakua kwa kasi ya asilimia 6.1 mwaka 2026 ukichochewa zaidi na kuimarika kwa shughuli za sekta binafsi, matarajio yanayotoa mwelekeo chanya licha ya kuongezeka kwa vihatarishi vya kiuchumi.
Katika kipindi cha muda wa kati, benki hiyo inaeleza katika ripoti yake mpya ya hali ya uchumi Tanzania ya Septemba 2026 (Tanzania Economic Update, September 2026) kuwa uchumi huo utakua hadi kufikia asilimia 6.5 ifikapo mwaka 2028.
Hata hivyo, matarajio hayo ya ukuaji wa uchumi kwa mwaka 2026 yapo chini kidogo na ya Serikali ambayo inatarajia pato halisi la Taifa (GDP) litakua kwa asilimia 6.3 kutoka asilimia 5.9 iliyorekodiwa mwaka jana.
Benki ya Dunia inaeleza kuwa sehemu kubwa mafanikio ya ukuaji wa uchumi huo yanategemewa kwa kiwango kikubwa sera rafiki za kibajeti na mwendelezo wa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara.
Benki hiyo imesema kuwa mwaka 2025 uchumi wa Tanzania ulikua kwa kasi ya asilimia 5.9 ukichochewa zaidi na matumizi ya Serikali kuelekea uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 2025.
“Matumizi ya Serikali yalikuwa zaidi ya theluthi mbili ya ukuaji wa pato halisi la Taifa huku matumizi yakiegemea zaidi katika matumizi ya kawaida,” imesema sehemu ya ripoti hiyo iliyozinduliwa leo, Oktoba 2, 2026 jijini Dar es Salaam.
Kazi ipo kutokomeza umaskini
Vigogo wa benki hiyo nchini wamesema kwa sehemu kubwa viashiria vingi vya kiuchumi vya Tanzania ni chanya huku wakieleza kuwa ukuaji wa uchumi kwa wastani wa asilimia sita katika muongo mmoja uliopita haujafanikiwa ipasavyo kupunguza umaskini.
“Bado tuna kazi kubwa sana ya kutokomeza umaskini,” amesema Firas Raad, Mkurugenzi wa Benki ya Dunia kwa Tanzania, Malawi, Zambia, na Zimbabwe.
Licha ya mwenendo chanya wa ukuaji wa uchumi, benki hiyo imesema vihatarishi vikubwa vya kiuchumi vilivyopo kwa sasa ni vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati baina ya Marekani, Israel na Iran na masuala ya mabadiliko ya tabianchi ikiwemo tishio la ujio wa mvua kubwa za El nino.
Katika ripoti hiyo iliyoangazia masuala ya kazi, WB imesema kuwa Tanzania haina changamoto kubwa ya ukosefu wa kazi bali ina tatizo kubwa la ubora wa ajira zilizopo ambazo haziendani na viwango pendekezwa vya ubora ikiwemo mishahara inayoweza kumsaidia mtu kumudu gharama za maisha.
Takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaitaja Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa Afrika yenye kiwango kidogo cha ukosefu wa ajira kwa watu wenye miaka 15 na zaidi cha asilimia 5.9.
Hata hivyo, takwimu hizo zinaonyesha kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kwa vijana wenye miaka 15 hadi 35 cha asilimia 7.5.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof Kitila Mkumbo amesema changamoto kuwa ni ukosefu wa ajira kwa wahitimu wa shule na vyuo (Graduate unemployment).