Bajeti wizara ya habari yaongezeka kwa Sh9.4 bilioni
- Bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2021/2021 imeongezeka hadi Sh40.2 bilioni kutoka Sh30.8 bilioni mwaka huu.
- Itatumika kuratibu na kusimamia maendeleo ya sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo na taasisi zake.
Dar es Salaam. Bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ya mwaka 2021/2021 imeongezeka kwa Sh9.4 bilioni na kufikia Sh40.2 bilioni zitakazotumika kipindi hicho kuratibu na kusimamia maendeleo ya sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo na taasisi zake.
Bajeti hiyo iliyosomwa Bungeni jana (Aprili 22, 2020) na kupitishwa na wabunge imeongezeka kutoka Sh30.8 ya mwaka wa fedha wa 2019/2020 sawa na ongezeko la Sh9.4 bilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe aliyekuwa akisoma hotuba hiyo, amesema kati ya fedha hizo, Sh20.9 zitatumika kulipa mishahara ya watumishi wa wizara huku Sh11.5 bilioni zitaelekezwa katika matumizi mengineyo.
Dk Mwakyembe amesema Sh7.7 bilioni sawa na asilimia 3.1 ya bajeti yote itaenda katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Zinazohusiana:
- Serikali yasema ongezeko la bajeti ya kilimo litategemea mahitaji ya kibajeti ya sekta nyingine
- Serikali yaanika bajeti ya mwaka 2019/2020
- Dk Mpango-Wastani wa pato la kila mtu waongezeka Tanzania
Amesema bajeti hiyo ya mwaka 2020/21 itajikita katika kuratibu na kusimamia maendeleo ya sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo na taasisi zake ambapo majukumu mbalimbali yamepangwa kutekelezwa.
“Tutaimarisha makusanyo ya mapato yatokanayo na shughuli zinazofanyika katika viwanja vya Taifa na Uhuru ambavyo vinamilikiwa na Serikali ikiwemo kuboresha mfumo wa ukusanyaji mapato katika viwanja hivyo,” amesema Dk Mwakyembe.
Mbali na kuidhinishiwa Sh40.2 bilioni, wizara hiyo itatumia vyanzo vyake kukusanya mapato ya Sh960 milioni kupitia Idara ya Habari-MAELEZO na maendeleo ya michezo.
“Aidha, kwa upande wa taasisi saba zilizo chini ya wizara kiasi kinachokadiriwa kukusanywa ni jumla ya Sh40.2 bilioni kwa mwaka 2020/21,” amesema Mwakyembe.