Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari yaomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh291.5 

May 16, 2025 3:50 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Fedha za mishahara zapungua wakati matumizi ya miradi ya maendeleo ikiongezeka.
  • Kamati yaishauri Serikali kutoa fedha zinazoidhinishwa kwa wakati.

Dar es Salaam. Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeliomba Bunge liidhinishe bajeti ya Sh291.5 bilioni kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ambapo robo tatu ya fedha hizo inatarajiwa kutumika kwenye miradi ya maendeleo.

Fedha hizo zimeongezeka kwa asilimia 61.2 sawa na Sh110.63 bilioni kutoka Sh180.9 bilioni iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa, aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara yake katika mwaka wa fedha 2025/26 leo Mei 16, 2025 bungeni jijini Dodoma amewaambia wabunge kuwa, kati ya fedha zinazoombwa Sh14.5 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara na matumizi mengineyo.

“Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2025/26 Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inakadiria kutumia Sh14.5 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kati ya fedha hizo Shi 6.96 bilioni ni kwa ajili ya mishahara (PE) na Sh7.53 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo (OC),” amesema Waziri Silaa.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26. Picha/Bunge la Tanzania/X.

Hata hivyo, bajeti ya matumizi ya kawaida imepungua kwa asilimia 62.7 sawa na Sh24.41 bilioni ikilinganishwa na Sh38.9 bilioni ya mwaka wa fedha 2024/25 unaomalizika mwezi Juni 2025.

Kwa mujibu wa Waziri Silaa, miradi ya maendeleo itagharimu Sh277 bilioni, kati ya fedha hizo Sh98.5 ni fedha za ndani huku Sh178.6 bilioni zikiwa ni fedha za nje.

Aidha, kwa upande wa fedha za miradi ya maendeleo zimeongezeka kwa Sh135.05 bilioni sawa na asilimia 95.1 ukilinganisha na Sh142.0 bilioni zilizoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Miraji Mtaturu aliyemuwakilisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu amewaambia wabunge kuwa kwa wastani hali ya upatikanaji wa fedha kwa wizara unaridhisha kwani hadi kufikia februari 2025 ilikuwa na wastani wa juu wa asilima 66.5.

“Mheshimiwa Naibu Spika, kamati inaendelea kusisitiza serikali kuhakikisha kwamba fedha zote zilizoidhinishwa na bunge zitatolewa kabla ya mwaka wa fedha 2024/25 ,” amesema Mtaturu. 

Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa akiteta jambo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu ) William Lukuvi leo bungeni. Picha/ Bunge la Tanzania/X.

Sanjari na hilo Mtaturu amesema Serikali inapaswa kuendelea kuboresha mifumo ya makusanyo ya mapato na ufuatiliaji ili kuongeza mapato ya Serikali na kutathimini uwezo wa kila taasisi kuhusu upatikanaji wa fedha hadi mwezi februari 2025.

Pia, kulingana na ongezeko la jumbe kwenye mitandao ya simu ambazo baadhi ya watumiaji hawavutiwi nazo kamati imeishauri Serikali kuwa pamoja na hatua zilizoendelea kuchukuliwa na mamlaka husika jitihada zaidi zinahitajika.

“Wizara husika ishirikiane na makampuni ya mitandao ya simu pamoja na wizara ya mambo ya ndani ili kumaliza tatizo,” amesema Mtaturu.

Miongoni mwa majukumu ya wizara hii ni pamoja kuandaa, kusimamia na kuratibu utekelezaji wa sera zinazohusu Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (Tehama), posta na mawasiliano ya simu na kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa sera, mipango na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali kwa wananchi.

Vipaumbele vya bajeti ya wizara 

Katika mwaka 2025/26 wizara itajikita katika utekelezaji wa vipaumbele kama kutunga, kuhuisha na kusimamia utekelezaji wa miongozo inayosimamia Sekta ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na posta kote nchini.

Vipaumbele vingine ni kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kukuza na kuimarisha biashara mtandao nchini, kuimairisha miundombinu itakayowezesha utekelezaji wa uchumi wa kidijitali pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama wa anga ya mtandao kwa kujenga uelewa kwa wananchi juu ya ulinzi wa data na faragha zao na jinsi ya kukabiliana na matukio ya utapeli na wizi mtandaoni.

Vilevile, kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kuchochea ubunifu na kuimarisha ustawi wa kampuni changa (Startups) ikiwemo kusimamia uanzishwaji wa vyuo viwili vya Tehama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks