Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii 2024-25 yapungua kwa asilimia 47

May 31, 2024 3:49 pm · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Yapungua kwa asilimia 47 kulinganisha na Sh654.7 bilioni ya mwaka 2023/24.
  • Fedha za matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo zazidi kupungua.

Dar es Salaam. Wizara ya Maliasili na Utalii imeliomba bunge liidhinishe bajeti ya Sh348.1 bilioni kwa mwaka 2024/25 ikipungua kwa asilimia 47 kulinganisha na ile iliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha unaoishia Juni, 2024.

Mwaka 2023/2024 wizara hiyo iliidhinishiwa Sh654.7 bilioni iliyopungua kwa Sh306.5 bilioni katika mwaka 2024/25.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni leo Mei 31, 2024, amewaambia wabunge kuwa kati ya fedha zilizoombwa, Sh250.8 bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, yakijumuisha mishahara na matumizi mengineyo.

“Mheshimiwa Spika, ndani ya fedha hizo za matumizi ya kawaida kuna Sh125.5 bilioni kwa ajili ya matumizi mengineyo, na Sh125.3 bilioni kwa ajili ya mishahara.” amesema Waziri Kairuki.

Kati ya kiasi hicho kiliichoombwa bungeni na Waziri Kairuki Sh97.2 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa kukabiliana na ujangili.

Hata hivyo fedha hizo kwa ajili ya miradi ya maendeleo zimepungua kwa asilimia 42.2 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. 

Mwaka 2023/24 wizara hiyo ilitengewa Sh168.2 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo iliyopungua zaidi hadi Sh97.2 bilioni kwa mwaka wa fedha utakaoanza Julai, 2024.


Soma zaidi: Mapato yatokanayo na utalii wa kitaifa, kimataifa yapaa Tanzania


Vipaumbele vya Wizara 2024/25

Waziri Kairuki amewaambia wabunge kuwa kwa mwaka 2024/25 wizara yake itatekeleza vipaumbele nane ikiwemo kuendelea kutangaza utalii ndani na nje ya nchi ikiwa ni mwendelezo wa program maalum ya Tanzania The Royal Tour, filamu ya Amazing Tanzania pamoja na mikakati mingine mikubwa ikiwemo matangazo katika ligi kuu za michezo.

“Kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati ikiwemo maeneo ya malikale pamoja na utalii wa fukwe, mikutano ya matukio, meli, michezo, tiba na utamaduni,” amesema Waziri Kairuki.

Vipaumbele vingine ni kuboresha miundombinu katika maeneo ya hifadhi, kuimarisha ulinzi na uhifadhi wa wanyamapori, misitu, nyuki na malikale, kuendelea kutekeleza mipango na mikakati ya uhifadhi pamoja na kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya misitu na nyuki.

Wizara hiyo pia itaelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za wanyamapori, misitu, ufugaji nyuki na malikale, kuendelea kuimarisha mifumo ya upatikanaji wa takwimu mbalimbali zinazohusu rasilimali hizo, pamoja na kutekeleza mikakati ya kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi na mifumo ya ukusanyaji wa mapato hayo.

Enable Notifications OK No thanks