Bajeti ofisi ya Makamu wa Rais yapaa, robo kutumika kwenye maendeleo
- Imeongezeka kwa asilimia 2.5 hadi kufikia Sh28.7 bilioni.
- Robo ya bajeti hiyo imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Dar es Salaam. Bajeti ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) kwa mwaka 2021/22 imeongezeka kwa asilimia 2.5 hadi kufikia Sh28.7 bilioni huku takriban robo ya bajeti hiyo imeelekezwa kwenye miradi ya maendeleo.
Ongezeko hilo ni sawa na Sh718.2 milioni ikilinganishwa na bajeti ya Sh27.9 ya mwaka wa fedha wa 2020/21 ambao unaisha Juni 30 mwaka huu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo aliyekuwa akiwasilisha hotuba ya bajeti yake bungeni jijini Dodoma leo Aprili 27, 2021 ameliomba Bunge kuidhinisha kiasi hicho cha fedha ili wizara yake iweze kutekeleza majukumu iliyopanga mwaka ujao.
Amesema katika ya Sh28.7 bilioni zilizopangwa, Sh6.8 bilioni ni fedha za miradi ya maendeleo sawa na asilimia 23.6 ya bajeti yote ya wizara hiyo.
“Fedha za miradi ya maendeleo zinajumuisha fedha za ndani Sh4.28 bilioni na Sh2.57 bilioni ni fedha za nje,” amesema Jafo katika hotuba yake.

Fedha zinazoelekezwa kwenye wizara anayoingoza Jafo zinatumika na Makamu wa Rais na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Licha ya kuwa fedha za maendeleo kutovuka robo ya bajeti yote ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Jafo amesema wizara yake imepanga kutekeleza vipaumbele sita ambavyo ni kuimarisha usimamizi wa shughuli za hifadhi na usimamizi wa mazingira katika ngazi ya Serikali za Mitaa.
Vipaumbele vingine ni kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala; kulinda na kutunza vyanzo vya maji na udhibiti wa taka ngumu.
“Kuendelea kuratibu utekelezaji wa mpango-kazi wa Taifa wa kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo wa dhahabu nchini; na kuendelea kufuatilia utekelezaji wa sheria ya usimamizi wa mazingira katika migodi na viwandani,” amesema Jafo.
Soma zaidi:
- Bajeti ya Wizara ya Ulinzi yapaa kwa mara ya pili mfululizo.
- Bashungwa: Sijapewa fedha za maendeleo wizara ya viwanda, biashara 2019-2020
- Kamwelwe aomba matrilioni kugharamia ujenzi, uchukuzi Tanzania
Utekelezaji wa vipaumbele hivyo utahusisha matumizi ya Sh200 milioni kufanya tathmini ya utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004; kuandaa kanuni 15 na miongozo 15 inayohitajika kwa ajili ya kuboresha usimamizi na utekelezaji wa sheria husika.
Pia kuweka mfumo wa kimtandao wa kutoa vibali vya mazingira (Tathmini ya Mazingira Kimkakati; na vibali vya taka za vifaa vya umeme na kielektroniki),” amesema Jafo.
Mwaka 2020/21, wizara hiyo ndiyo ilitengewa kiasi kidogo cha fedha kuliko wizara zote. Mwaka ujao hali itabaki ile ile au kiasi kilichotengwa kitakuwa juu kidogo ya wizara zingine.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Erick Shigongo ameitaka Serikali kuhakikisha inaongeza kasi ya ulinzi wa mazingira kwa kuwaelimisha wananchi kuzirejeleza taka kuwa bidhaa mbalimbali, kudhibiti matumizi ya kemikali za zebaki kwenye vyanzo vya maji na mazingira.
Pia amesema fedha zilizopangwa zitolewe kwa wakati ili kuharahisisha utekelezaji wa majukumu ya ofisi ya Makamu wa Rais.
Latest
