Bajeti wizara ya maji yapunguza kibano kwa viongozi

May 13, 2022 8:23 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Rais Samia Suluhu Hassan akizindua mradi wa majisafi na usafi  wa mazingira Misungwi mkoani Mwanza Juni 14, 2021. Mradi huu una thamani ya Sh13.77 bilioni. Picha| Wizara ya Maji.


  • Wizara yapokea asilimia 95 ya fedha zilizopangwa mwaka 2021/22.
  • Yasaidia kuongeza utekelezaji wa miradi ya maji.

Dar es Salaam. Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema hadi kufikia mwezi April mwaka huu, wizara yake imepokea asilimia 95 ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge la Tanzania katika bajeti ya mwaka 2021/22, jambo lililotoa fursa ya kuwapelekea wananchi maji.

Utekelezaji huo huenda sasa ukawapa tabasamu viongozi wa wizara hiyo muhimu kwa ustawi wa maendeleo Tanzania kwa sababu miradi iliyoidhinishwa itakuwa imetekelezwa kwa kiwango cha juu.

Katika bajeti ya mwaka 2021/22, Wizara ya Maji iliidhinishiwa bajeti Sh819.7 bilioni ambapo kati ya fedha hizo Sh785.9 bilioni sawa na asilimia 95.8 zilikuwa ni fedha za maendeleo na kiasi kilichobaki kilielekezwa katika matumizi ya kawaida ikiwemo mishahara ya wafanyakazi wa wizara. 

Aweso aliwaambia wabunge Mei 12, 2022 wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka ujao kuwa hadi mwezi April 2022 wizara hiyo ilikuwa imepokea jumla ya Sh778.9 bilioni ya bajeti yote ya mwaka huu.

Hiyo ni sawa na asilimia 95 ya fedha zote za bajeti zilizoidhinishwa mwaka huu wa fedha wa 2021/22 unaomalizika Juni 30, 2020.

“Kati ya fedha zilizopokelewa, Sh743.7 bilioni ni za kutekeleza miradi ya maendeleo sawa na asilimia 95 ya bajeti ya fedha za maendeleo,” amesema Waziri huyo.

Kiasi hicho cha fedha ambacho kimepokelewa hadi April mwaka huu ni kikubwa ikilinganishwa na asilimia 54.1 zilizokuwa zimepokelewa hadi Aprili 2021 katika bajeti ya mwaka 2020/21.


Soma zaidi:


Mwaka 2020/21, Wizara ya fedha ilidhinishiwa na Bunge bajeti ya Sh733.3 bilioni ambapo kati ya hizo Sh705 bilioni zilikuwa za maendeleo.

Bajeti ya maji ni moja ya bajeti ambazo huwa na mjadala mzito bungeni kabla ya kupitishwa na hufikia wakati baadhi ya wabunge hutishia kushikilia shilingi ili isipitishwe mpaka mahitaji yao yatakaposikilizwa.

Utekelezaji wa miradi na programu kwa mwaka 2021/22 ulijikita katika maeneo matano ambayo ni usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji; huduma za ubora na usafi wa maji; miradi ya huduma za usambazaji maji vijijini; miradi ya huduma za usambazaji majisafi mijini; na miradi ya usafi wa mazingira.

Hata hivyo, katika mwaka wa 2022/23 wizara hiyo ya maji inapanga kutumia bajeti ya Sh709.4 bilioni ambapo kati ya fedha hizo, Sh657.8 bilioni zitatumika katika miradi ya maendeleo.

“Kati ya fedha hizo, Sh407.1 bilioni sawa na asilimia 61.87 ni fedha za ndani na Sh250.8 bilioni sawa na asilimia 38.13 ni fedha za nje,” amesema Waziri Aweso.

Fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni sawa asilimia 92.7 ya bajeti yote wizara hiyo, jambo litakalosaidia kuboresha huduma za upatikanaji wa maji safi na salama. 

Vipaumbele vya Wizara kwa mwaka 2022/23 ni pamoja na kukamilisha ujenzi, ukarabati na upanuzi wa miradi inayoendelea kutekelezwa na kuanza ujenzi wa mabwawa ya kimkakati ya Kidunda na Farkwa na kuanza ujenzi wa miradi ya maji mipya ikiwemo miradi ya maji katika miji 28.

Wizara itaendelea na utunzaji wa vyanzo vya maji ikihusisha kutambua, kuweka mipaka na kutangaza kwenye Gazeti la Serikali ili vyanzo hivyo vilindwe kisheria na kutekeleza miradi ya maji kwa kutumia vyanzo vya uhakika ikiwemo maziwa makuu na mito mikubwa.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Rais Samia azindua minara 758, aacha maagizo mazito juu ya mkongo wa taifa

Nukta TV

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

JAJI MKUU: Njia za asili ni mojawapo ya njia halali za utatuzi wa migogoro

Nukta TV

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Hesabu ya bosi, bei ya mafuta pasua kichwa madereva wa daladala

Nukta TV